Web address of the page: https://www.medjugorje.ws/sw/messages/15 
www.medjugorje.ws » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages

Our Lady of Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa, uwepo wangu halisi na wa uhai katikati yenu uwafanye kuwa wenye furaha kwani huo ni upendo mkuu wa Mwanangu. Yeye ananituma katikati yenu ili, kwa upendo wa kimama, Mimi niwaimarishe; ili muelewe kwamba maumivu na furaha, mateso na mapendo husaidia nafsi yenu kuishi kwa bidii zaidi; ili niwaalike tena kuadhimisha Moyo wa Yesu, moyo wa imani: Ekaristi. Mwanangu, siku kwa siku, hurudi hai katikati yenu: huwarudia, hata kama hakuwaacha kamwe. Wakati mmoja wenu, wanangu, anamrudia, Moyo wangu wa kimama hushtuka kwa furaha. Kwa hiyo Wanangu, irudieni Ekaristi, mrudieni Mwanangu. Njia ya kumrudia Mwanangu ni ngumu na imejaa kujinyima lakini mwishowe, kuna mwanga siku zote. Naelewa maumivu yenu na mateso yenu, na kwa upendo wa kimama, ninapangusa machozi yenu. Mtumainini Mwanangu, kwa maana Yeye atawafanyieni neno msilojua hata kuomba. Ninyi, wanangu, fikirieni nafsi yenu tu, kwani nafsi ni kitu cha pekee mliyo nayo duniani. Chafu ama safi, mtaichukua mbele ya Baba aliye Mbinguni. Kumbukeni: imani katika upendo wa Mwanangu hulipwa siku zote. Nawaambieni kuwaombea hasa wale ambao Mwanangu aliwaita kuishi wakimfuata na kulipenda kundi lao. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Mshukuruni Mungu kwa zawadi ya kuwepo kwangu pamoja nanyi. Salini, wanangu, mkaishi amri za Mungu mweze kuwa na heri duniani. Leo, katika siku hii ya neema nataka kuwapeni baraka yangu ya kimama ya amani na ya upendo wangu. Ninawaombeeni kwa Mwanangu na kuwaalika kudumu katika sala ili pamoja nanyi niweze kutimiza mipango yangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, kama Mama wa Kanisa, kama Mama yenu, ninatabasamu nikiwaona kunijia, kukusanyika kandokando yangu na kunitafuta. Ujio wangu katikati yenu ni onyesho la kadiri Mbingu inavyowapenda. Ujio wangu unawaonyesha njia ya kuelekea kwenye uzima wa milele, kuelekea wokovu. Mitume wangu, ninyi mnaojaribu kuwa na moyo safi na Mwanangu ndani yake, ninyi mpo katika njia njema. Ninyi mnamtafuta Mwanangu, mnatafuta njia njema. Yeye aliacha dalili nyingi za upendo wake. Ameacha tumaini. Ni rahisi kumpata, ikiwa mpo tayari kujitolea na kutubu, ikiwa mtakuwa na uvumilivu, rehema na upendo kwa jirani. Wanangu wengi hawaoni wala hawasikii maana hawataki. Hawapokei maneno na matendo yangu, lakini Mwanangu, kwa njia yangu, anawaalika wote. Roho yake huangaza wote katika mwanga wa Baba wa Mbinguni, katika ushirika kati ya Mbingu na dunia, katika upendano; maana upendo huita upendo na kutenda ili matendo yawe muhimu kuliko maneno. Kwa hiyo, mitume wangu, mliombee Kanisa lenu, lipende na tendeni matendo ya upendo. Ingawa limesalitiwa na kujeruhiwa, lipo hapa kwa sababu hutoka kwa Baba wa Mbinguni. Muwaombeeni wachungaji wenu, ili kuona ndani yao ukuu wa upendo wa Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Uwepo wangu ni zawadi ya Mungu na kichocheo cha uwongofu wenu. Shetani ana nguvu na anataka kutia moyoni na fikirani mwenu fujo na wasiwasi. Kwa hiyo, ninyi wanangu salini ili Roho Mtakatifu awaongoze katika njia iliyonyoka ya furaha na amani. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Moyo wangu wa kimama hutaka wongofu wenu mnyofu na ya kuwa muwe na imani thabiti, ili muweze kuwatangazia watu wote wanaowazunguka upendo na amani. Lakini, wanangu, msisahau: kila mmoja wenu mbele ya Baba aliye Mbinguni ni ulimwengu wa pekee! Kwa hiyo nguvu ya Roho Mtakatifu isiyo kifani iweze kutenda kazi ndani mwenu! Muwe wanangu safi kwa kiroho. Katika karama ya kiroho kuna uzuri. Yote yaliyo ya kiroho ni hai na nzuri ajabu. Msisahau ya kuwa katika Ekaristi, iliyo moyo wa imani, Mwanangu yu daima pamoja nanyi. Yeye anawajia na pamoja nanyi humega mkate maana, Mwanangu, kwa ajili yenu amekufa, amefufuka akaja tena. Haya maneno yangu ni ya muhimu kwa maana ni ukweli, na ukweli haubadiliki: lakini wanangu wengi hawayatambui. Wanangu, maneno yangu si mazee wala mapya, ni ya milele. Kwa hiyo nawaalika ninyi, wanangu, kuangalia alama za nyakati, na "kukusanya misalaba yaliyovunjika" na kuwa mitume wa Ufunuo. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Moyo wangu usio na doa unatoka damu nikiwaangalieni katika dhambi na mazoea mabaya. Nawaalika: mrudieni Mungu na salini ili mpate kufanikiwa duniani. Mungu anawaalika kwa njia yangu ili mioyo yenu iwe tumaini na furaha kwa wale wote walio mbali. Ombi langu liwe kwenu manukato kwa nafsi na moyo ili mtukuze Mungu Mwumbaji anayewapenda na kuwaalika kwa mambo ya milele. Wanangu, maisha ni mafupi, mtumie nafasi hii kwa ajili ya kutenda mema. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, msiwe na mioyo migumu, iliyofungwa na iliyojaa hofu. Pokeeni upendo wangu wa kimama uiangaze na kuijaza mioyo yenu upendo na matumaini, ili, kama Mama, niyalainishe maumivu yenu: ninayajua, na nimeyaonja. Maumivu huinua nayo ni sala kuu kuliko zote. Mwanangu huwapenda hasa wanaopokea maumivu. Alinituma Mimi niyalainishe na kuwaletea matumaini. Mumwamini Yeye. Najua kuwa ni vigumu kwenu, maana mnaona giza linalozidi kuongeza karibu yenu pande zote. Wanangu, giza mtalivunja kwa njia ya sala na upendo. Yule anayesali na kupenda haogopi, ana matumaini na upendo wenye huruma: Anaona mwanga, na anamwona Mwanangu. Kama mitume wangu nawaalika mjaribu kuwa mfano wa upendo wenye huruma na wenye matumaini. Salini sikuzote tena kwa ajili ya kupata upendo mwingi kadiri muwezavyo, maana upendo huleta mwanga unaovunja kila giza, na humleta Mwanangu. Msiogope, ninyi si peke yenu: Mimi nipo pamoja nanyi! Ninawasihi waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na upendo kila wakati na wawe na matendo ya upendo kwa Mwanangu, kwa njia yake na kwa kumkumbuka Yeye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Leo ninawaletea upendo wangu. Mungu ameniruhusu kuwapenda ninyi na kwa upendo nawaalika mwongoke. Wanangu, ninyi ni maskini katika upendo, na wala hamjaelewa bado ya kuwa Mwanangu Yesu ametolea maisha Yake ili awaokoeni na kuwapa uzima wa milele. Kwa hiyo salini wanangu, salini ili muweze kuelewa katika sala upendo wa Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ujio wangu kwenu ni zawadi ya Baba wa Mbinguni kwa ajili yenu. Kwa njia ya upendo wake ninakuja kuwasaidieni kupata njia inayowangoza kwenye ukweli, na kupata njia inayowaongoza kwa Mwanangu. Ninakuja kuwathibitishia ukweli. Nataka kuwakumbushia maneno ya Mwanangu. Yeye aliyatamka maneno ya wokovu kwa ulimwengu wote, maneno ya upendo kwa watu wote, ule upendo aliouonyesha kwa kujitolea kwake sadaka. Lakini hata leo wanangu wengi hawamjui, hawataki kumjua, hawamjali. Kwa sababu ya kutokujali kwao, moyo wangu unateseka kwa uchungu. Mwanangu amekuwa daima katika Baba. Alipozaliwa duniani, ametuletea Umungu, wakati kutoka kwangu ameuchukua ubinadamu. Kwa njia yake Neno limefika katikati yetu. Kwa njia yake Mwanga, ambao hupenyeza mioyoni, huiangaza, huijaza upendo na faraja, umeingia ulimwenguni. Wanangu, wanaweza kumwona Mwanangu wale wote wanaompenda, kwa kuwa uso wake huonekana kwa njia ya mioyo inayojaa mapendo kumwelekea Yeye. Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, mnisikilize! Acheni uovu na ubinafsi. Msiishi tu kwa ajili ya vitu vya ulimwengu, vinavyoharibika. Mpendeni Mwanangu na muwawezeshe wengine kuutambua uso kwa njia ya mapendo mliyo nayo kwake. Mimi nitawasaidia kumjua zaidi. Mimi nitawaeleza kuhusu Yeye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema nawaalikeni nyote kuongoka. Wanangu, mnapenda kidogo, na bado mnasali kidogo. Mmepotea wala hamjui lengo lenu ni nini. Chukueni msalaba wenu, mwangalieni Yesu mumfuate. Yeye anajitoa kwenu hata kufa msalabani maana anawapenda. Wanangu, nawaalikeni kurudia kusali kwa moyo kwa maana katika sala mnaweza kupata matumaini na maana ya uwepo wenu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.