Our Lady of Medjugorje Messages containing 'aliniambia'

Total found: 4
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama nawaombeni: pendaneni! mioyoni mwenu muwe kama Mwanangu alitaka tangu awali: kwanza kabisa kumpenda Baba wa Mbinguni na kuwa na upendo kwa jirani yenu, kuliko yote yaliyopo hapa duniani. Wanangu wapendwa, hamtambui dalili za nyakati hizi? Hamtambui ya kuwa yote yanayotokea kando kando yenu, hutokea kwa sababu hakuna upendo? Fahamuni kwamba wokovu hupatikana katika thamani za kweli, pokeeni uweza wa Baba wa Mbinguni, mpendeni na kumheshimu. Fuateni njia ya Mwanangu. Ninyi, wanangu, mitume wangu wapenzi, mnakusanyika siku zote daima kunizunguka maana mna kiu, mna kiu ya amani, ya upendo na ya furaha. Kateni kiu yenu katika mikono yangu! Mikono yangu yawatolea Mwanangu, aliye chemchemi ya maji safi. Yeye atafufua imani yenu na kusafisha mioyo yenu, kwa sababu Mwanangu hupenda kwa moyo safi na mioyo iliyo safi humpenda Mwanangu. Mioyo safi tu ndiyo minyenyekevu na yenye imani thabiti. Wanangu, nawaombeni ya kuwa na mioyo ya namna hii! Mwanangu aliniambia ya kuwa Mimi ni Mama wa ulimwengu wote: nawaombeni ninyi, mnaonipokea kama Mama, ili kwa maisha yenu, sala na sadaka nisaidieni ili wanangu wote wanipokee kama Mama, niweze kuwaongoza kwenye chemchemi ya maji safi. Nawashukuru! Wanangu wapenzi, wachungaji wenu wanapowatolea mwili wa Mwanangu, mshukuruni Mwanangu daima moyoni mwenu kwa sadaka yake na kwa wachungaji anayewajalia siku zote.
Wanangu wapendwa, nimekuja kwenu, katikati yenu, ili mnipe mahangaiko yenu, niweze kuyaleta mbele ya Mwanangu na kuwaombeeni kwake kwa manufaa yenu. Najua kuwa kila mmoja wenu ana mahangaiko yake, majaribu yake. Kwa hiyo kwa moyo wa kimama nawaalikeni: Njooni kwenye Meza ya Mwanangu! Yeye humega mkate kwa ajili yenu, huwapa Yeye mwenyewe. Huwapa matumaini. Anawaomba kuwa na imani zaidi, matumaini zaidi, utulivu zaidi. Anawaomba mpigane ndani yenu dhidi ya ubinafsi, hukumu na udhaifu wa kibinadamu. Kwa hiyo Mimi, kama Mama, nawaambieni: salini, maana sala huwapa nguvu ya kupigana ndani yenu. Mwanangu, alipokuwa mtoto, aliniambia mara nyingi ya kuwa wengi watanipenda na kuniita "Mama". Mimi hapa, katikati yenu, nasikia upendo na kuwashukuru! Kwa njia ya upendo huu namwomba Mwanangu ili hakuna hata mmoja wenu, wanangu, arudiye nyumbani jinsi alivyokuja. Ili mlete matumaini, rehema na upendo kadiri muwezavyo; ili muwe mitume wa upendo wangu, wanaoshuhudia kwa maisha yao kwamba Baba aliye Mbinguni ni chemchemi ya uzima si ya mauti. Wanangu wapendwa, nawaomba tena kwa moyo wa kimama: waombeeni wateule wa Mwanangu, kwa ajili ya mikono yao iliyobarikiwa, kwa ajili ya wachungaji wenu, ili waweze kumhubiri Mwanangu kwa upendo mwingi wawezavyo, na hivyo kusababisha wongofu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninaongea nanyi kama Mama, kwa maneno rahisi, lakini yamejaa wingi wa upendo na wa bidii kwa wanangu, ambao kwa njia ya Mwanangu wamekabidhiwa kwangu. Mwanangu, ambaye anakuja kutoka umilele na hata sasa, anaongea nanyi kwa maneno ya uzima na anapanda upendo katika mioyo wazi. Kwa hiyo nawaomba, mitume wa upendo wangu: muwe na mioyo iliyo wazi sikuzote kurehemu na kusamehe. Wasameheni sikuzote wenzenu kama Mwanangu, kwa vile hivyo amani itakuwa ndani yenu. Wanangu, lindeni nafsi yenu, maana hiyo ndiyo ukweli wa pekee ulio wenu bila shaka. Mmeanza kusahau umuhimu wa familia. Familia haipaswi kuwa mahali pa mateso na maumivu, bali mahali pa uelewano na huruma. Familia wanaojaribu kuishi kama apendavyo Mwanangu, wanaishi wakipendana. Tangu alipokuwa angali mtoto, Mwanangu aliniambia ya kuwa watu wote kwake ni ndugu zake. Kwa hiyo kumbukeni, enyi mitume wa upendo wangu, watu wote mnaowaona ni kwenu familia yenu, ndugu kama apendavyo Mwanangu. Wanangu, msipoteze muda kufikiria na kuhangaikia mambo yajayo. Kitu chenu kimoja cha kuhangaikia kwenu kiwe vipi kuishi vema kila dakika kadiri ya Mwanangu, na tazama hiyo ndiyo ni amani! Wanangu, msisahau kabisa kuwaombea wachungaji wenu. Salini ili waweze kupokea watu wote kama wanao, ili, kama apendavyo Mwanangu, wawe kwao kama baba za kiroho. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninawaelekea ninyi kama Mama yenu, Mama wa wenye haki, Mama wa wale wanaopenda na kuteseka, Mama wa watakatifu. Wanangu, ninyi pia mnaweza kuwa watakatifu: ni juu yenu. Watakatifu ni wale wanaompenda Baba wa Mbinguni kupita kiasi, wale wanaompenda kupita chochote. Kwa hivyo, wanangu, jaribuni daima kuboreka. Kama ninyi mnajaribu kuwa wema, mtaweza kuwa watakatifu, hata kama hamfikiri hiyo juu yenu. Kama mnafikiri kuwa wema, ninyi sio wanyenyekevu na kiburi huwatenga kutoka utakatifu. Katika ulimwengu huu wa wasiwasi, umejaa vitisho, mikono yako, mitume wa upendo wangu, inapaswa kuwa imenyoshwa katika maombi na rehema. Kwangu, wanangu, nipeni zawadi ya Rozari, mawaridi ninayopenda sana! Mawaridi yangu ni maombi yenu msemayo kwa moyo wote, na sio yale msemayo kwa midomo yenu tu. Mawaridi yangu ni matendo yenu ya maombi, imani na upendo. Wakati alipokuwa mtoto, mwanangu aliniambia kwamba watoto wangu watakuwa wengi na wataniletea mawaridi mengi. Sikuelewa, sasa najua kwamba ninyi ni watoto wale, wanaoniletea mawaridi wakati mnapompenda mwanangu kupita yote, wakati mnaposali kwa moyo wote, wakati mnapowasaidia walio maskini zaidi. Hayo ndiyo mawaridi yangu! Hii ndiyo imani, inayosababisha kila kitu katika maisha kifanyike kwa upendo; na kiburi hakijulikani; na muwe tayari daima, kusamehe upesi, bila kuhukumu na daima mjaribu kuelewa ndugu yako. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, muwaombeeni wale wasiojua kupenda, wale wasiowapenda, wale waliowatenda mabaya, wale ambao hawakujua upendo wa Mwanangu. Wanangu, ninawaomba haya, kwa sababu kumbukeni: kuomba maana yake ni kupenda na kusamehe. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`