Monthly Medjugorje Messages - Karibuni of year 2015

Wanangu wapendwa, Leo pia nawaletea Mwanangu Yesu katika mikono yangu, na kwa mikono hiyo nawapeni amani Yake na hamu ya Mbinguni. Ninasali pamoja nanyi kwa ajili ya amani na ninawaalika muwe amani. Nawabariki wote kwa baraka yangu ya kimama na ya amani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, leo ninawaalika nyote: salini kwa ajili ya nia zangu. Amani ipo hatarini kwa hiyo wanangu, salini na muwe waletaji wa amani na matumani katika ulimwengu huu wa wasiwasi ambamo shetani anashambulia na kuleta majaribu ya kila aina. Wanangu muwe thabiti katika sala na imara katika imani. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi nyote mbele ya Mwanangu, Yesu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, sala yangu hata leo ni kwa ajili yenu nyote, hasa kwa wale walio na mioyo migumu kuitikia wito wangu. Mnaishi katika siku za neema wala hamtambui fadhili ambazo Mungu anawapeni kwa njia ya uwepo wangu. Wanangu, amueni hata leo kuwa watakatifu na jifunzeni kutokana na mifano ya watakatifu wa siku hizi na mtatambua ya kuwa utakatifu ni ukweli uliopo kwa ajili yenu nyote. Wanangu, furahini katika upendo kwa maana machoni pa Mungu ninyi ni wa pekee na hakuna atakayechukua nafasi ya mwingine, kwa maana ninyi ni furaha ya Mungu duniani hapa. Mshuhudieni amani, sala na upendo. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, hata leo ninamwomba Roho Mtakatifu ili ajaze mioyo yenu kwa imani thabiti. Sala na imani zitajaza mioyo yenu kwa upendo na furaha, nanyi mtakuwa ishara kwa wale walio mbali na Mungu. Wanangu, mpeane moyo wenyewe kwa wenyewe ili kufanya sala ya moyo, ili sala iweze kujaza maisha yenu na ninyi, wanangu, kila siku muwe mashahidi wa utumishi: kwa Mungu katika kuabudu na kwa majirani zenu katika mahitaji yao. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi nyote. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, hata leo ninawaalika: muwe sala. Sala iwe mabawa kwa ajili ya mkutano kati yenu na Mungu. Ulimwengu upo katika wakati wa kujaribiwa, kwa maana umemsahau na kumwacha Mungu. Kwa hiyo wanangu, muwe wale wanaomtafuta na kupenda Mungu kuliko yote. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaongoza kwa Mwanangu, lakini ninyi hamna budi kunena "NDIYO" yenu katika uhuru wa wana wa Mungu. Nawaombeeni na kuwapenda, wanangu, kwa upendo usio na mwisho. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, hata leo kwa furaha nipo pamoja nanyi na ninawaalika wote, wanangu, salini, salini, salini, ili muweze kuelewa upendo nilio nao kwenu. Upendo wangu una nguvu kuliko uovu, kwa hiyo wanangu mjongeeni Mungu ili muweze kuonja furaha yangu kwa Mungu. Pasipo Mungu, wanangu, hamtakuwa na wakati ujao, wala tumaini, wala wokovu, kwa hiyo acheni uovu na chagueni wema: Mimi nipo pamoja nanyi na pamoja nanyi namwomba Mungu kwa mahitaji yenu yote. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Hata leo Yeye Aliye Juu ananipa neema ya kuweza kuwapenda na kuwaalika muweze kuongoka. Wanangu, Mungu awe kesho yenu, vita, wasiwasi, huzuni yasiwatawale, ila furaha na amani zitawale mioyoni mwa watu wote, na mjue kuwa pasipo Mungu hamtapata kamwe amani. Kwa hiyo, wanangu, mrudieni Mungu na sala ili mioyo yenu iimbe kwa furaha. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawapenda kwa upendo usio na kipimo. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Hata leo mimi nipo pamoja nanyi na kwa furaha nawaalikeni nyote: salini na aminini nguvu ya sala. Fungueni mioyo yenu, wanangu, ili Mungu awajaze upendo wake, nanyi mtakuwa furaha ya watu wengine. Ushahidi wenu utakuwa na nguvu na lote mfanyalo litaendana na mapenzi ya Mungu. Mimi nipo pamoja nanyi, nikisali kwa ajili yenu na kwa ajili ya wokovu wenu hata mtakapomweka Mungu mahali pa kwanza. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Mimi nipo pamoja nanyi hata leo niwaongozeni kwenye wokovu. Moyo wenu una wasiwasi maana roho yenu ni dhaifu na imechoka kwa mambo yote ya dunia. Ninyi wanangu, ombeni Roho Mtakatifu awageuze na kuwajaza nguvu yake ya imani na tumaini ili muweze kuwa imara katika kupambana kwenu na maovu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea kwenye Mwanangu Yesu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Hata leo pia Yeye Aliye Juu ameniruhusu kuwa pamoja nanyi na kuwaongoza katika njia ya uwongofu. Mioyo mingi imejifunga kwa neema wala haitaki kusikiliza mwaliko wangu. Ninyi wanangu salini na pambaneni na kishawishi na mipango yote ya uovu ambayo anayowapatia shetani kwa njia ya mambo ya kisasa. Muwe hodari katika kusali na mkishika msalaba mikononi salini ili maovu yasiwatumie wala kuwashinda. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema ninawaalika nyote: salini zaidi na muongee kidogo. Katika kusali tafuteni mapenzi ya Mungu na yaishini kadiri ya amri ambazo Mungu anawaalika kuziishi. Mimi nipo pamoja nanyi na kusali pamoja nanyi. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Hata leo ninawaalika: ishini katika sala mwito wenu. Leo, kama bado haijatokea awali, Shetani atamani kumfunga pumzi binadamu na roho yake kwa njia ya upepo wake unaoambukiza chukio na hofu. Katika mioyo mingi hakuna furaha kwa sababu hakuna Mungu wala sala. Uadui na vita zinaongezeka siku hata siku. Ninawaalika, wanangu, anzisheni upya kwa ari mwelekeo wa kutafuta utakatifu na upendo kwa maana nimekuja katikati yenu kwa ajili hiyo. Tuwe upendo na msamaha kwa wale wote wanaofahamu na kutaka kupenda kwa mapendo ya kibinadamu tu wala siyo kwa ule upendo mkubwa sana wa kimungu ambao Mungu anatualikia. Wanangu, matumaini ya kesho iliyo bora zaidi yawe daima mioyoni mwenu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`