Web address of the page: https://www.medjugorje.ws/sw/messages/20 
www.medjugorje.ws » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages

Our Lady of Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa! Salini na mfahamu ya kwamba pasipo Mungu ninyi ni mavumbi. Kwa hiyo geuzeni fikira zenu na mioyo yenu kwa Mungu na kwa sala. Tegemeeni upendo Wake. Katika Roho ya Mungu ninyi nyote mnaalikwa kuwa mashahidi. Ninyi mna thamani mbele ya Mungu, nami nawaalika, wanangu, kuwa watakatifu, ili mweze kupata uzima wa milele. Kwa hiyo mfahamu ya kwamba maisha haya hupita. Nawapendeni na kuwaalika kwa maisha mapya ya kutubu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Mimi, Mama yenu, nipo pamoja nanyi kwa ajili yenu, kwa mahitaji yenu na mafundisho yenu binafsi. Baba wa Mbinguni amewapa uhuru wa kuamua peke yenu na kujua peke yenu. Mimi nataka kuwasaidieni. Nataka kuwa Mama kwenu, mwalimu wa ukweli, ili kwa unyofu wa moyo wazi mjue usafi usio na mwisho, na mwanga utokao kwa hiyo ukweli ili kutawanya giza, yaani mwanga uletao tumaini. Mimi, wanangu, naelewa maumivu yenu na mateso yenu. Nani aweza kuwaelewa zaidi kuliko Mama mmoja! Lakini enyi wanangu? Mjue kuwa idadi ya wanaonielewa na kunifuata ni ndogo. Pia ni kubwa idadi ya waliopotea, hao ambao hawajajua ukweli ulio katika Mwanangu. Kwa hiyo, enyi mitume wangu, salini na tendeni kazi. Mbebe mwanga, msipoteze tumaini. Mimi nipo nanyi na hasa pamoja na wachungaji wenu. Nawapenda na kuwalinda kwa Moyo wa kimama, ili kusudi wao wanawaongozeni Paradisini alikowaahidia Mwanangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! Fungueni mioyo yenu kwa neema ambayo Mungu anawapa kwa njia yangu kama vile ua linalojifungua kwa miali ya joto la jua. Muwe sala na upendo kwa wale wote walio mbali na Mungu na upendo Wake. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawaombea nyote kwa Mwanangu Yesu na ninawapenda kwa upendo usio na mipaka. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Kwa upendo wa kimama nataka kuwasaidia ili maisha yenu ya kusali na kutubu iwe juhudi ya kweli ya kumjongea Mwanangu na nuru yake ya kimungu, ili muweze kutengana na dhambi. Kila sala, kila Misa na kila mfungo ni juhudi ya kumjongea Mwanangu, msukumo kwa utukufu wake na kuepukana na dhambi. Ni njia ya muungano mpya wa Baba mwema na wanao. Kwa hiyo, wanangu wapendwa, kwa unyofu wa moyo uliojaa upendo mliite jina la Baba wa Mbinguni, ili awatie nuru ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu mtakuwa chemchemi ya upendo wa Mungu: kwenye chemchemi hiyo wale wote wasiomjua Mwanangu watakunywa, wote wenye kiu ya upendo na amani ya Mwanangu. Nawashukuru! Salini kwa ajili ya wachungaji wenu. Mimi nawaombee na nataka waonje siku zote baraka ya mikono yangu na tegemeo la Moyo wangu wa kimama.
Wanangu wapendwa! Nawaalikeni tena: anzeni kupambana na dhambi kama vile katika siku za mwanzo, nendeni kuungama dhambi zenu na kateni shauri ya kuwa watakatifu. Kwa njia yenu upendo wa Mungu utaenea ulimwenguni na amani itatawala mioyoni mwenu na baraka ya Mungu itawajaza. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombeeni mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Naja kwenu kama Mama na ninatamani kuwa kwangu kama Mama mtapata maskani, faraja na mapumziko. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, salini! Salini kwa moyo mkunjufu, utii na uaminifu kamili kwa Baba wa Mbinguni. Muwe na uaminifu, kama vile mimi pia nilivyokuwa mwaminifu nilipoambiwa ya kuwa nitachukua baraka za ahadi. Basi kutoka mioyo yenu yafike siku zote midomoni mwenu maneno haya "Utakalo lifanyike". Kwa hiyo muwe na uaminifu na salini, ili mimi niweze kuwaombeeni kwa Bwana, ili awape Baraka ya Mbinguni na kuwajaza Roho Mtakatifu. Hapo mtaweza kuwasaidia wale wote wasiomjua Bwana. Ninyi, mitume wa upendo wangu, mtawasaidia kumwita "Baba" kwa uaminifu wote. Salini kwa ajili ya wachungaji wenu na mujiaminishe katika mikono yao iliyobarikiwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Mnaona, mnasikia na kuhisi kwamba katika mioyo ya watu wengi hakuna Mungu. Hawamtaki kwa maana wapo mbali na sala na hawana amani mioyoni. Ninyi, wanangu, salini, na isheni kadiri ya amri za Mungu. Muwe sala, enyi mlioitikia "naam" tangu mwanzo wa mwaliko wangu. Mshuhudieni Mungu na mtambue uwepo wangu wala msisahau, wanangu, ya kuwa mimi ni pamoja nanyi na ninawapenda. Siku hata siku nawachukua kwa Mwanangu Yesu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Kwa upendo wa kimama nataka kuwafundisha uadilifu, natamani kwamba katika kutenda kwenu kazi kama mitume wangu muwe wenye haki, maamuzi na hasa waadilifu. Natamani kwamba, kwa neema ya Mungu, muweze kupokea Baraka ya Mungu. Natamani, kwa njia ya kufunga na kusali, muweze kupata kutoka kwa Baba wa Mbinguni ujuzi, uhalali, utakatifu wa kimungu. Kwa ulinzi wa Mwanangu na wangu mtakuwa mitume wangu, ambao wanaweza kueneza neno la Mungu kwa wote wasiolijua, na mtaweza kushinda mapingamizi mtakayokutana nayo njiani. Wanangu, kwa njia ya baraka neema itawashukia, nanyi mtaweza kuilinda neema hiyo kwa kufunga na kusali, kwa kujitakasa na kujipatanisha. Mtakuwa na utendaji fanisi ninaohitaji kutoka kwenu. Waombeeni wachungaji wenu ili mionzi ya neema ya Mungu iangaze njia yao. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Salini, salini, salini ili mionzi ya sala yenu iwaguse watu wote mnaokutana nao. Wekeni Biblia Takatifu mahali pa kuonekana katika familia zenu, mkaisome ili maneno ya amani yatiririke ndani ya mioyo yenu. Nasali pamoja nanyi na kwa ajili yenu, wanangu, ili siku hata siku mzidi kuyapokea mapenzi ya Mungu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Ili mpate kuwa mitume wangu na kuweza kusaidia wale walioko katika giza, ili waweze kuujua mwanga wa upendo wa Mwanangu, mnapaswa kuwa na moyo safi na mnyenyekevu. Hamwezi kusaidia ili Mwanangu azaliwe na kutawala mioyoni mwa wale wasiomjua, iwapo Yeye hatawali moyoni mwenu. Mimi nipo pamoja nanyi, natembea pamoja nanyi kama mama, nabisha hodi katika moyo wenu, usioweza kufunguka bila ya kuwa mnyenyekevu. Mimi nasali, lakini salini nanyi pia, wanangu wapendwa, ili muweze kumfungulia Mwanangu moyo wenu safi na mnyenyekevu na hivyo kuweza kupokea vipaji nilivyowaahidi. Hapo ndipo mtakapoongozwa kwa upendo na nguvu za Mwanangu, hapo ndipo mtakuwa mitume wangu, ambao wanaweza kueneza kwa walio karibu yao matunda ya upendo wa Mungu. Kutokana na ninyi na kwa njia yenu Mwanangu atafanya kazi, maana mtakuwa na Yeye kitu kimoja. Moyo wangu wa kimama unatamani muungano wa wanangu wote, kwa njia ya Mwanangu. Kwa upendo mkuu nawabariki na kuwaombea wateule wa Mwanangu, wachungaji wenu, Nawashukuru.