Web address of the page: https://www.medjugorje.ws/sw/messages/highlight?find=kupenda&page=2 
www.medjugorje.ws » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages containing 'kupenda'

Our Lady of Medjugorje Messages containing 'kupenda'

Total found: 26
Katika tokeo la mwisho la kila siku tarehe 12 Septemba 1998 Bikira Maria alimwambia Yakobo Kolo ya kuwa ataona tokeo mara moja kila mwaka, tarehe 25 Decemba, siku ya Noeli. Hivyo kumekuwa na tokea hata mwaka huu. Tokeo limeanza saa 7 na dakika 38 na likadumu dakika 9. Bikira Maria amekuja pamoja na Mtoto Yesu mikononi mwake. Bikira Maria kwa njia ya Yakobo alipitisha ujumbe huu:
Wanangu wapendwa, katika siku hii ya neema ninawaalika kupenda. Wanangu, Mungu anawapenda kupita kiasi na kwa hiyo wanangu, mmejaa imani, bila kutazama nyuma na bila hofu mwachieni kabisa mioyo yenu ili Mungu aijaze kwa upendo wake. Msiwe na hofu kuamini upendo Wake na rehema Yake maana upendo Wake ni mwenye nguvu kuliko kila udhaifu wenu na hofu. Kwa hiyo, wanangu, mmejaa upendo katika mioyo yenu mwamini Yesu na mseme Ndiyo yenu maana Yeye ni njia ya pekee ya kuwaongoza kwa Baba wa milele.
Wanangu wapendwa, inasikitisha kwamba katikati yenu, wanangu, yapo mashindano mengi, chuki, masilahi yenu wenyewe na ubinafsi. Wanangu, hivi kwa urahisi mnamsahau Mwanangu, maneno Yake na upendo Wake. Imani inazimika katika roho nyingi na mioyo imetekwa na vitu vya ulimwenguni. Lakini moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa katikati yenu kuna wale wanaoamini na kupenda, wale ambao wanajaribu kumkaribia Mwanangu zaidi na zaidi, ambao wanamtafuta bila kuchoka na namna hii, wananitafuta hata mimi. Hawa ndio wanyenyekevu na wapole ambao, pamoja na maumivu na mateso wanayoyachukua katika kimya, pamoja na tumaini lao na hasa pamoja na imani yao, ni mitume wa upendo wangu. Wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawafundisha ya kuwa Mwanangu hatafuti sala tu pasipo kuchoka bali hata matendo na hisia. Salini ili katika sala mpate kuzidi katika imani na katika upendo. Mpendane wenyewe kwa wenyewe: hilo ndilo analotaka Yeye, hiyo ndiyo ni njia ya uzima wa milele. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu ameleta mwanga kwa ulimwengu huu. Ameuleta kwa wale ambao walitaka kuuona na kuupokea. Hawa muwe ninyi, maana huu ndio mwanga wa ukweli, wa amani na wa upendo. Mimi ninawaongoza kama mama kumwabudu Mwanangu, kumpenda pamoja nami. Fikira zenu, maneno na matendo yenu yamwelekee Mwanangu, yawe katika jina Lake: hapo tu moyo wangu utajazwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninawaita mitume wa upendo wangu. Ninawaonyesha Mwanangu, aliye amani ya kweli na upendo wa kweli. Kama Mama, kwa ajili ya neema ya kimungu, ninatamani kuwaongoza kwendea Yeye. Wanangu, kwa hiyo ninawaalika kujitazama ninyi wenyewe mkianzia kwa Mwanangu, kumtazama kwa moyo na kuona kwa moyo mahali mlipo na maisha yenu yanakwenda wapi. Wanangu, ninawaalika kuelewa ya kuwa mnaishi kwa ajili ya Mwanangu, kwa njia ya upendo wake na sadaka yake. Ninyi mnamwomba Mwanangu kuwa mwenye rehema nanyi, lakini mimi ninawaalika ninyi kuwa na rehema. Mnamwomba kuwa mwema nanyi na kuwasamehe, lakini tangu lini mimi ninawasihi ninyi, wanangu, kusamehe na kupenda watu wote mnaokutana nao! Mtakapoelewa kwa moyo maneno yangu, mtaelewa na kujua upendo wa kweli, na mtaweza kuwa mitume wa upendo ule, enyi mitume wangu, wanangu wapendwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, moyo safi na wazi tu utawawezesha ninyi kumjua kweli Mwanangu, na wale wote wasiojua upendo wake kuujua kwa njia yenu. Upendo tu utawawezesha kuelewa kuwa ni wenye nguvu kuliko kifo, maana upendo wa kweli umeshinda kifo na umefanya hata kifo hakipo tena. Wanangu, msamaha ni mtindo bora wa upendo. Ninyi, kama mitume wa upendo wangu, yawapasa kusali kwa kuwa wenye nguvu katika roho na kuweza kuelewa na kusamehe. Ninyi, mitume wa upendo wangu, kwa njia ya ufahamu na msamaha, mnatoa mfano wa upendo na rehema. Kuweza kuelewa na kusamehe ni karama inayotokana na maombi na yatupasa kuitunza. Mkisamehe ninyi mnaonyesha ya kuwa mnajua kupenda. Tazameni, wanangu, kama Baba wa mbinguni anavyowapenda kwa upendo mkubwa, kwa ufahamu, kwa uelewa, msamaha na haki. Kama anavyowatolea mimi, Mama wa mioyo yenu. Na tazama: mimi nipo katikati yenu ili kuwabariki kwa baraka ya kimama; ili kuwaalika kusali na kufunga; ili kuwasihi kuamini, kutumaini, kusamehe, kuwaombea wachungaji wenu na hasa kupenda bila mipaka. Wanangu, nifuateni! Njia yangu ni njia ya amani na upendo, njia ya Mwanangu. Ndiyo njia ya kuongoza katika ushindi wa Moyo wangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, mapenzi na upendo wa Baba wa mbinguni hufanya mimi niwe katikati yenu, ili kusaidia kwa upendo wa kimama ukuaji wa imani katika mioyo yenu, ili kwamba muweze hakika kuelewa lengo la maisha ya kidunia na ukuu wa yale ya kimbingu. Wanangu, maisha ya kidunia ndiyo njia kuelekea umilele, kuelekea ukweli na uzima: kuelekea kwa Mwanangu. Kwa njia hii nataka kuwaongoza. Ninyi, wanangu, ninyi wenye sikuzote kiu ya upendo mkubwa zaidi, ukweli na imani, mjue ya kuwa moja tu ni chemchemi mnakoweza kunywa: imani katika Baba wa mbinguni, imani katika upendo wake. Mtegemee kabisa mapenzi yake wala msiogope: kila lililo bora kwa ajili yenu, kila linalowachukua kwenye uzima wa milele, mtapewa! Mtaelewa ya kuwa lengo la maisha si sikuzote kutaka na kutwaa, lakini kupenda na kutoa; mtakuwa na amani ya kweli na upendo wa kweli, mtakuwa mitume wa upendo. Kwa mfano wenu, mtawafanya wale wanangu wasiomjua Mwanangu na upendo wake watake kumjua. Wanangu, mitume wa upendo wangu, mwabuduni Mwanangu pamoja nami, na mpendeni juu ya vyote. Jaribuni sikuzote kuishi katika ukweli wake. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, nilichaguliwa kuwa mama wa Mungu na mama yenu, kwa maamuzi na upendo wa Bwana, lakini pia kwa mapenzi yangu, kwa upendo wangu usio na kifani kwake Baba wa mbinguni na kwa imani yangu yote Kwake. Mwili wangu ulikuwa kikombe cha Mungu Mtu. Nilikuwa mtumishi wa ukweli, wa upendo na wokovu kama vile nilivyo sasa katikati yenu, ili kuwaalika, wanangu, mitume wa upendo wangu, kuwa waletaji ukweli, ili kuwaalika, kwa njia ya utashi na upendo yenu kumwelekea Mwanangu, ili kueneza maneno Yake, maneno ya wokovu na kuyaonyesha, kwa vitendo vyenu, kwa wale wote ambao hawajamjua mwanangu na upendo Wake. Nguvu mtaipata katika Ekaristi: Mwanangu awalisheni kwa mwili Wake na kuwaimarisha kwa damu Yake. Wanangu, wekeni mikono yenu pamoja kwa sala na tazameni kuelekea msalaba kwa ukimya. Kwa jinsi hii mtapata imani ili muweze kuieneza, mtapata ukweli ili muweze kuupambanua, mtapata upendo ili muweze kuelewa namna ya kupenda kwa uhakika. Wanangu, mitume wa upendo wangu, wekeni mikono yenu pamoja kwa sala na tazameni kuelekea msalaba: katika msalaba tu kuna wokovu. Ninawashukuru.