Web address of the page: https://www.medjugorje.ws/sw/messages/ 
www.medjugorje.ws » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages by month Desemba

Our Lady of Medjugorje Messages by month Desemba

Wanangu wapendwa, ninawaelekea ninyi kama Mama yenu, Mama wa wenye haki, Mama wa wale wanaopenda na kuteseka, Mama wa watakatifu. Wanangu, ninyi pia mnaweza kuwa watakatifu: ni juu yenu. Watakatifu ni wale wanaompenda Baba wa Mbinguni kupita kiasi, wale wanaompenda kupita chochote. Kwa hivyo, wanangu, jaribuni daima kuboreka. Kama ninyi mnajaribu kuwa wema, mtaweza kuwa watakatifu, hata kama hamfikiri hiyo juu yenu. Kama mnafikiri kuwa wema, ninyi sio wanyenyekevu na kiburi huwatenga kutoka utakatifu. Katika ulimwengu huu wa wasiwasi, umejaa vitisho, mikono yako, mitume wa upendo wangu, inapaswa kuwa imenyoshwa katika maombi na rehema. Kwangu, wanangu, nipeni zawadi ya Rozari, mawaridi ninayopenda sana! Mawaridi yangu ni maombi yenu msemayo kwa moyo wote, na sio yale msemayo kwa midomo yenu tu. Mawaridi yangu ni matendo yenu ya maombi, imani na upendo. Wakati alipokuwa mtoto, mwanangu aliniambia kwamba watoto wangu watakuwa wengi na wataniletea mawaridi mengi. Sikuelewa, sasa najua kwamba ninyi ni watoto wale, wanaoniletea mawaridi wakati mnapompenda mwanangu kupita yote, wakati mnaposali kwa moyo wote, wakati mnapowasaidia walio maskini zaidi. Hayo ndiyo mawaridi yangu! Hii ndiyo imani, inayosababisha kila kitu katika maisha kifanyike kwa upendo; na kiburi hakijulikani; na muwe tayari daima, kusamehe upesi, bila kuhukumu na daima mjaribu kuelewa ndugu yako. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, muwaombeeni wale wasiojua kupenda, wale wasiowapenda, wale waliowatenda mabaya, wale ambao hawakujua upendo wa Mwanangu. Wanangu, ninawaomba haya, kwa sababu kumbukeni: kuomba maana yake ni kupenda na kusamehe. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Kwa furaha kubwa leo nawaletea Mwanangu Yesu ili Yeye awapeni amani Yake. Wanangu, fungueni mioyo yenu na muwe wafurahivu, ili muweze kuipokea. Mbingu ni pamoja nanyi na zinapambana kwa ajili ya amani mioyoni mwenu, katika jamaa na ulimwenguni na ninyi, wanangu, msaidieni kwa sala zenu ili iwe hivyo. Ninawabariki pamoja na Mwanangu Yesu na kuwaomba msikose matumaini, na mtazamo wenu na moyo wenu yaelekee daima mbinguni na uzima wa milele. Hivyo mtafunguliwa kwa Mungu na mipango Yake. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Katika tokeo la mwisho wa kila siku la tarehe 12 Septemba 1998 Mama Maria alimwambia Yakobo ya kuwa ataona tokeo lake mara moja kila mwaka, tarehe 25 Desemba, siku ya Kristmasi. Hivyo ikatokea na mwaka huu. Mama Maria ametokea pamoja na Mtoto Yesu mikononi mwake. Tokeo likaanza saa nane adhuhuri na dakika ishirini na kudumu dakika kumi. Yakobo, baadaye, akatoa ujumbe ufuatao:
Wanangu wapendwa, Leo katika siku hii ya neema nawaalika hasa kusali kwa ajili ya amani. Wanangu, nimekuja hapa kama Malkia wa Amani na mara nyingi nimewaalika kusali kwa ajili ya amani. Lakini wanangu, mioyo yenu imefadhaika. Dhambi inawazuia kufunguliwa kabisa kwa neema na amani ambayo Mungu ataka kuwapeni. Ili kuishi amani, wanangu, yawapasa kuwa kwanza na amani mioyoni mwenu na kujiachia kabisa kwa Mungu na mapenzi Yake. Msitafute amani na furaha katika mambo ya dunia hii maana haya yote hupita. Muelekee rehema ya kweli, amani itokayo kwa Mungu tu na hivyo mioyo wenu hivyo tu itajaa furaha ya kweli; hivyo tu mtaweza kuwa mashahidi wa amani katika dunia hii ya hofu. Mimi ni mama yenu na ninawaombea kila mmoja wenu mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Moyo wangu wa kimama unalia machozi ninapoyaona yale wanayoyafanya wanangu. Dhambi zinaongezeka, usafi wa moyo unaendelea kupoteza umuhimu wake. Mwanangu amesahauliwa na upendo kwake unaendelea kupunguka na wanangu wanateswa. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa moyo wangu, iteni jina la Mwanangu kwa nafsi na kwa moyo: Yeye atakuwa na maneno ya mwanga kwenu. Naye atajionyesha kwenu, anashiriki Mkate pamoja nanyi na anawapa maneno ya upendo, ili myageuze kuwa matendo ya huruma na muwe hivyo mashahidi ya ukweli. Kwa hiyo, wanangu, msiogope! Acheni Mwanangu awe ndani yenu. Yeye atawatumia ninyi ili kuzitibu nafsi zinazojeruhiwa na kuziongoka zile zinazopotea. Kwa hiyo, wanangu, rudieni kusali Rozari. Mwisali kwa roho ya ukarimu, ya sadaka na ya huruma. Salini si kwa maneno tu, ila kwa matendo ya huruma. Salini kwa upendo kwa watu wote. Mwanangu amekuza kimaadili upendo kwa njia ya sadaka yake. Kwa hiyo isheni pamoja naye mpate nguvu na matumaini, mpate upendo ulio uhai wa kuongoza kwenye uzima wa milele. Kwa njia ya upendo wa Mungu mimi nami ni pamoja nanyi, na nitawaongoza kwa upendo wa kimama. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Leo pia nawaletea Mwanangu Yesu katika mikono yangu, na kwa mikono hiyo nawapeni amani Yake na hamu ya Mbinguni. Ninasali pamoja nanyi kwa ajili ya amani na ninawaalika muwe amani. Nawabariki wote kwa baraka yangu ya kimama na ya amani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, miaka hii yote ambapo Mungu ananijalia kuwepo pamoja nanyi ni ishara ya upendo mwingi sana wa Mungu kwa kila mmoja wenu na ishara ya jinsi alivyowapenda. Wanangu, Yeye Aliye Juu amewapeni neema nyingi na anataka kuwapa neema nyingi zaidi. Lakini, wanangu, mioyo yenu imefungwa, inaishi katika hofu na hayaruhusu upendo wa Yesu na amani yake yapate nafasi katika mioyo yenu na kutawala maisha yenu. Kuishi pasipo Mungu ni kuishi gizani wala kutoujua kamwe upendo wa Baba na ulinzi wake kwa kila mmoja wenu. Kwa hiyo wanangu, leo hasa mwombeni Yesu ili tangu leo maisha yenu yapate kuzaliwa upya katika Mungu, na maisha yenu iwe nuru itokayo kwenu. Namna hii mtakuwa mashahidi wa uwepo wa Mungu ulimwenguni hasa kwa kila mtu aishiye gizani. Wanangu, nawapenda na kuwaombeeni kila siku kwake Yeye Aliye Juu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, mimi ni sikuzote pamoja nanyi, kwa maana Mwanangu alinikabidhi ninyi. Nanyi, wanangu, mnanihitaji mimi, mnitafute, mnijie na mfurahishe Moyo wangu wa kimama. Mimi ninawapenda na nitawapenda ninyi mnaoteseka na kutolea mateso yenu kwa ajili ya Mwanangu na kwa ajili yangu. Upendo wangu hutafuta upendo wa wanangu wote na wanangu wote hutafuta upendo wangu. Kwa njia ya upendo Yesu hutafuta ushirika kati ya Mbingu na dunia, kati ya Baba wa mbinguni na ninyi, wanangu, Kanisa lake. Kwa hiyo lazima kusali sana, kusali na kulipenda Kanisa ambalo ninyi ni wake. Sasa Kanisa linateseka na kuhitaji mitume ambao, wakipenda ushirika, wanaposhuhudia na kutoa, waonyeshe njia za Mungu. Kanisa linahitaji mitume ambao, wakiishi Ekaristi kwa moyo, watende matendo makuu. Kanisa linawahitaji ninyi, mitume wangu wa upendo. Wanangu, Kanisa limeteswa na kusalitiwa tangu siku zake za awali, lakini linazidi kukua siku hata siku. Kanisa halitaharibiki, kwa maana Mwanangu alilipa moyo: Ekaristi. Nuru ya ufufuo wake imeng’aa na itang’aa juu yake. Kwa hiyo msiogope! Waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na nguvu na upendo kwa kuwa madaraja ya wokovu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, zingatieni akilini, kwa maana nawaambia: upendo utashinda! Najua ya kuwa wengi wenu wanapoteza matumaini kwa kuwa wanaona wamezungukwa na mateso, maumivu, husuda na wivu, hata hivyo mimi ni Mama yenu. Mimi nipo katika Ufalme, lakini hata hapa nipo pamoja nanyi. Mwanangu ananituma tena ili niwasaidieni, kwa hiyo msipoteze matumaini ila nifuateni, kwa maana ushindi wa Moyo wangu ni kwa jina la Mungu. Mwanangu mpendwa anawafikiria, kama alivyofanya siku zote: mwaminini na mwishi kama Yeye! Yeye ni uzima wa ulimwengu. Wanangu, kumwishi Mwanangu maana yake ni kuishi Injili. Si kitu rahisi. Ni jambo linalodai upendo, rehema na sadaka. Hayo huwatakasa na kufungua Ufalme: Sala nyofu, isiyo maneno bali itokayo moyoni, itawasaidieni. Vivyo hivyo kufunga, maana hayo huleta ongezeko la upendo, rehema na sadaka. Kwa hiyo msipoteze matumaini, ila nifuateni. Nawaomba tena msali kwa ajili ya wachungaji wenu, ili wamtazame daima Mwanangu, aliyekuwa Mchungaji wa kwanza wa ulimwengu, na ambaye familia yake ilikuwa ulimwengu wote. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! Ninawaletea Mfalme wa amani ili Yeye awapatie amani Yake. Ninyi, wanangu, salini, salini, salini. Matunda ya sala yatajionyesha kwenye nyuso za watu waliojitoa kwa Mungu na Ufalme wake. Mimi pamoja na mwanangu Yesu tunawabariki nyote kwa baraka ya amani. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama na uvumilivu wa kimama naona kutangatanga kwenu na kuendelea kupotea kwenu. Kwa sababu hiyo mimi nipo pamoja nanyi. Nataka kwanza kabisa kuwasaidieni kupata kujijua ninyi wenyewe, ili baadaye muweze kuelewa na kutambua yote yanayowazuia kujua bila unafiki na kwa moyo wote upendo wa Baba wa Mbinguni. Wanangu, Baba hujulikana kwa njia ya msalaba: kwa hiyo msikatae msalaba: kwa msaada wangu, mkafanye bidii kuuelewa na kuupokea. Mtakapoweza kuupokea msalaba, mtaelewa pia upendo wa Baba wa Mbinguni. Mtatembea pamoja na Mwanangu na mimi. Mtajipambanua na wale ambao hawakujua upendo wa Baba wa Mbinguni, kujitofautisha na wale wanaomsikiliza lakini hawamwelewi, na wale wasioenda pamoja naye, na wasiomjua. Mimi nataka ninyi mjue ukweli wa Mwanangu na muwe mitume wangu; ili, kama wana wa Mungu, muwe na mawazo yaliyo juu ya mawazo ya kibinadamu na siku zote na katika yote mkatafute kila mara mawazo ya Mungu. Wanangu, salini na fungeni ili muweze kuelewa yote ninayowaombeni. Muombee wachungaji wenu mkatamani kujua, mkishirikiana nao, upendo wa Baba wa Mbinguni. Nawashukuruni.