Web address of the page: https://www.medjugorje.ws/sw/messages/ 
www.medjugorje.ws » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages by month Mei

Our Lady of Medjugorje Messages by month Mei

Wanangu wapendwa! Uwepo wangu ni zawadi ya Mungu na kichocheo cha uwongofu wenu. Shetani ana nguvu na anataka kutia moyoni na fikirani mwenu fujo na wasiwasi. Kwa hiyo, ninyi wanangu salini ili Roho Mtakatifu awaongoze katika njia iliyonyoka ya furaha na amani. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Moyo wangu wa kimama hutaka wongofu wenu mnyofu na ya kuwa muwe na imani thabiti, ili muweze kuwatangazia watu wote wanaowazunguka upendo na amani. Lakini, wanangu, msisahau: kila mmoja wenu mbele ya Baba aliye Mbinguni ni ulimwengu wa pekee! Kwa hiyo nguvu ya Roho Mtakatifu isiyo kifani iweze kutenda kazi ndani mwenu! Muwe wanangu safi kwa kiroho. Katika karama ya kiroho kuna uzuri. Yote yaliyo ya kiroho ni hai na nzuri ajabu. Msisahau ya kuwa katika Ekaristi, iliyo moyo wa imani, Mwanangu yu daima pamoja nanyi. Yeye anawajia na pamoja nanyi humega mkate maana, Mwanangu, kwa ajili yenu amekufa, amefufuka akaja tena. Haya maneno yangu ni ya muhimu kwa maana ni ukweli, na ukweli haubadiliki: lakini wanangu wengi hawayatambui. Wanangu, maneno yangu si mazee wala mapya, ni ya milele. Kwa hiyo nawaalika ninyi, wanangu, kuangalia alama za nyakati, na "kukusanya misalaba yaliyovunjika" na kuwa mitume wa Ufunuo. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Hata leo mimi nipo pamoja nanyi na kwa furaha nawaalikeni nyote: salini na aminini nguvu ya sala. Fungueni mioyo yenu, wanangu, ili Mungu awajaze upendo wake, nanyi mtakuwa furaha ya watu wengine. Ushahidi wenu utakuwa na nguvu na lote mfanyalo litaendana na mapenzi ya Mungu. Mimi nipo pamoja nanyi, nikisali kwa ajili yenu na kwa ajili ya wokovu wenu hata mtakapomweka Mungu mahali pa kwanza. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, fungueni mioyo yenu mkajaribu kuhisi jinsi ninavyowapenda na kutaka mpendeni Mwanangu. Nataka mpende zaidi kwa kuwa haiwezekani kumjua pasipo kumpenda, maana Yeye ndiye upendo. Wanangu, mimi nawajueni: najua maumivu yenu na mateso yenu maana niliyaishi. Nafurahi pamoja nanyi kwa furaha zenu. Nalia machozi pamoja nanyi katika maumivu yenu. Sitawaacheni kamwe. Nitaongea nanyi daima kwa upole wa kimama na, kama mama, nahitaji mioyo yenu ifumbuliwe, ili kwa hekima na unyofu mueneze upendo wa Mwanangu. Nawahitaji ninyi mfumbuliwe na kuwa wepesi kupokea mema na huruma. Nahitaji muungano wenu na Mwanangu, kwa maana nataka mpate kufanikiwa na kumsaidia kuleta heri kwa wanangu wote. Mitume wangu, nawahitaji, ili muwaonyeshe wote ukweli wa Mungu, ili moyo wangu, ulioteswa na kuteswa hata leo kupita kiasi, uweze kushinda katika upendo. Salini kwa ajili ya utakatifu wa wachungaji wenu, ili katika jina la Mwanangu, waweze kutenda maajabu, maana utakatifu hutenda maajabu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Salini na mfahamu ya kwamba pasipo Mungu ninyi ni mavumbi. Kwa hiyo geuzeni fikira zenu na mioyo yenu kwa Mungu na kwa sala. Tegemeeni upendo Wake. Katika Roho ya Mungu ninyi nyote mnaalikwa kuwa mashahidi. Ninyi mna thamani mbele ya Mungu, nami nawaalika, wanangu, kuwa watakatifu, ili mweze kupata uzima wa milele. Kwa hiyo mfahamu ya kwamba maisha haya hupita. Nawapendeni na kuwaalika kwa maisha mapya ya kutubu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Mimi, Mama yenu, nipo pamoja nanyi kwa ajili yenu, kwa mahitaji yenu na mafundisho yenu binafsi. Baba wa Mbinguni amewapa uhuru wa kuamua peke yenu na kujua peke yenu. Mimi nataka kuwasaidieni. Nataka kuwa Mama kwenu, mwalimu wa ukweli, ili kwa unyofu wa moyo wazi mjue usafi usio na mwisho, na mwanga utokao kwa hiyo ukweli ili kutawanya giza, yaani mwanga uletao tumaini. Mimi, wanangu, naelewa maumivu yenu na mateso yenu. Nani aweza kuwaelewa zaidi kuliko Mama mmoja! Lakini enyi wanangu? Mjue kuwa idadi ya wanaonielewa na kunifuata ni ndogo. Pia ni kubwa idadi ya waliopotea, hao ambao hawajajua ukweli ulio katika Mwanangu. Kwa hiyo, enyi mitume wangu, salini na tendeni kazi. Mbebe mwanga, msipoteze tumaini. Mimi nipo nanyi na hasa pamoja na wachungaji wenu. Nawapenda na kuwalinda kwa Moyo wa kimama, ili kusudi wao wanawaongozeni Paradisini alikowaahidia Mwanangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! Leo nawaalikeni kuwa na nguvu na imara katika imani na katika sala, ili sala zenu ziwe zenye nguvu za kuweza hata kufungua moyo wa Mwanangu mpendwa Yesu. Salini enyi wanangu wadogo, bila kukoma, ili moyo wenu ujifungue kwa upendo wa Mungu. Mimi nipo pamoja nanyi, nawaombea ninyi nyote nikasali kwa ajili ya uwongofu wenu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, nawaalikeni tena kupenda na kutohukumu. Mwanangu, kwa mapenzi ya Baba aliye mbinguni, alikuwapo pamoja nanyi ili awaonyesheni njia ya wokovu, awaokoeni si awahukumuni. Na ikiwa mnataka kumfuata Mwanangu, msihukumu na mpende, kama vile Baba aliye mbinguni anavyowapenda ninyi. Hata wakati mnapoteseka sana, au mnapojikwaa chini ya msalaba, msikate tamaa, msihukumu, bali kumbukeni kwamba mnapendwa, na msifuni Baba aliye mbinguni kwa upendo wake. Wanangu, msiiache njia ninayowaongozeni. Msikimbie kwenye maangamizi. Kusali na kufunga itawapa nguvu zaidi ili mweze kuishi kama vile baba wa Mbinguni atakavyo; ili muwe mitume wangu wa imani na upendo; ili maisha yenu iwe na baraka ya wale mnaowaona; ili muwe kitu kimoja na baba aliye mbinguni na Mwanangu. Wanangu, huu ni ukweli wa pekee, ukweli uletao wongofu wenu na kisha wongofu wa wengine wote wasiojua maana ya neno kupenda. Wanangu, Mwanangu aliwapeni wachungaji: muwalinde, na muwaombee. Nawashukuru!