Our Lady of Medjugorje Messages containing 'alivyowapenda'

Total found: 4
Wanangu wapendwa, katika wakati huu wa wasiwasi nawaalikeni tena kutembea nyuma ya Mwanangu, na kumfuata. Nayajua maumivu, mateso na taabu zenu, lakini katika Mwanangu mtapumzika, ndani yake mtapata amani na wokovu. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu amewakomboa ninyi kwa msalaba wake akawajalieni kuwa tena wana wa Mungu na kuwafundisha kumwita tena "Baba" yenu, Mungu aliye mbinguni. Ili muwe wapenzi wa Mungu Baba, basi muwe na mapendo na msamaha, kwa kuwa Baba yenu ni upendo na msamaha. Salini na fungeni, kwa maana hii ndiyo njia ya kujua na kumfahamu Baba aliye mbinguni. Mtakapomjua huyo Baba, mtafahamu ya kuwa Yeye tu ni muhimu kwenu (Maria Mtakatifu amenena hayo kwa nguvu na amkazo sana). Mimi, nikiwa Mama, nataka wanangu wawe watu wenye umoja ambamo Neno la Mungu husikilizwa na kutekelezwa. Kwa hiyo, enyi wanangu, mfuateni Mwanangu, muwe kitu kimoja naye, muwe wana wa Mungu. Pendeni wachungaji wenu kama vile Mwanangu alivyowapenda alipowaita kuwatumikia ninyi. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, kwa moyo wa kimama nawaalikeni tena kupenda, kusali bila kukata tamaa kwa zawadi ya upendo, kumpenda Baba wa Mbinguni zaidi ya yote. Mtakapompenda Yeye, mtajipenda wenyewe na jirani zenu. Mambo hayo hayawezi kutengana. Baba wa Mbinguni yumo katika kila mtu, hupenda kila mtu na kumwita kila mtu kwa jina lake. Kwa hiyo, wanangu, kwa njia ya kusali sikilizeni atakalo Baba wa Mbinguni. Ongeeni na Yeye. Muwe na uhusiano wa binafsi pamoja na Baba, atakayeufanya mkubwa zaidi uhusiano wake nanyi, jumuhiya ya wanangu, mitume wangu. Kama Mama napenda kwamba, kwa njia ya upendo kumwelekea Baba wa Mbinguni, inukeni juu ya ubatili wa malimwengu na muwasaidie wengine kujua na kumjongea polepole Baba wa Mbinguni. Wanangu, salini, salini, salini kwa zawadi ya upendo, kwa sababu upendo ndiye Mwanangu. Muwaombee wachungaji wenu, ili wawapende ninyi siku zote, kama vile Mwanangu alivyowapenda ninyi na kuonyesha akitoa maisha yake kwa wokovu wenu. Nawashukuruni.
Wanangu wapendwa, miaka hii yote ambapo Mungu ananijalia kuwepo pamoja nanyi ni ishara ya upendo mwingi sana wa Mungu kwa kila mmoja wenu na ishara ya jinsi alivyowapenda. Wanangu, Yeye Aliye Juu amewapeni neema nyingi na anataka kuwapa neema nyingi zaidi. Lakini, wanangu, mioyo yenu imefungwa, inaishi katika hofu na hayaruhusu upendo wa Yesu na amani yake yapate nafasi katika mioyo yenu na kutawala maisha yenu. Kuishi pasipo Mungu ni kuishi gizani wala kutoujua kamwe upendo wa Baba na ulinzi wake kwa kila mmoja wenu. Kwa hiyo wanangu, leo hasa mwombeni Yesu ili tangu leo maisha yenu yapate kuzaliwa upya katika Mungu, na maisha yenu iwe nuru itokayo kwenu. Namna hii mtakuwa mashahidi wa uwepo wa Mungu ulimwenguni hasa kwa kila mtu aishiye gizani. Wanangu, nawapenda na kuwaombeeni kila siku kwake Yeye Aliye Juu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, kama Mama nafurahi ya kuwa katikati yenu, kwa maana nataka kuongea nanyi tena kuhusu maneno ya Mwanangu na upendo wake. Natumaini mtanipokea kwa upendo, maana maneno ya Mwanangu na upendo wake ni nuru na tumaini la pekee katika giza la siku hizi. Huu ni ukweli wa pekee, nanyi mtakaoupokea na kuuishi, mtakuwa na mioyo safi na minyenyekevu. Mwanangu hupenda mioyo safi na minyenyekevu. Mioyo safi na minyenyekevu inahuisha maneno ya Mwanangu: inayaishi, inayaeneza na kufanya hata wote wayasikie. Maneno ya Mwanangu yanaamsha maisha ya wale wanaoyasikiliza, maneno ya Mwanangu hurudisha upendo na matumaini. Kwa hiyo, mitume wangu wapenzi, wanangu, isheni maneno ya Mwanangu. Pendaneni kama Yeye alivyowapenda. Pendaneni katika jina lake na kumbukumbu lake. Kanisa huendelea na kukua kwa ajili ya wale wanaosikiliza maneno ya Mwanangu, kwa sababu ya wanaohuzunika na kuteseka kimyakimya katika tumaini la kukombolewa milele. Kwa hiyo wanangu wapendwa, maneno ya Mwanangu na upendo wake yawe wazo la kwanza na la mwisho la siku yenu. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`