Our Lady of Medjugorje Messages containing 'damu'

Total found: 5
Wanangu wapendwa, nawaalika kueneza imani katika Mwanangu, imani yenu. Ninyi wanangu, mlioangazwa na Roho Mtakatifu, mitume wangu, itangazeni imani kwa watu wengine, yaani kwa wasiosadiki, wasioijua na wasiotaka kuijua. Kwa sababu hiyo yawapasa kusali sana kwa ajili ya zawadi ya upendo, maana upendo ndio alama maalum ya imani ya kweli, na ninyi mtakuwa mitume wa upendo wangu. Upendo hufanya upya daima maumivu na furaha ya Ekaristi, hufanya upya maumivu ya Mateso ya Mwanangu, aliyewaonyesha upendo usio na kifani; hufanya upya furaha ya tendo la kuwaachia Mwili wake na Damu yake kwa ajili ya kuwalisha na hivyo kuwa kitu kimoja nanyi. Nikiwaangalia kwa wema nahisi upendo pasipo kiasi, ulioniimarisha katika hamu yangu ya kuwaongoza katika imani thabiti. Imani thabiti itawapa furaha na uchangamfu duniani, na mwishowe kuwaunganisha na Mwanangu. Hiyo ndiyo hamu yake. Kwa hiyo mwishi katika Yeye, na katika upendo, isheni katika nuru iliyowaangaza daima katika Ekaristi. Nawaombeni kusali sana kwa wachungaji wenu, kusali ili kupata upendo mkubwa kwa ajili yao, kwa maana Mwanangu aliwapeni ili waweze kuwalisha kwa Mwili wake na kuwafundisha upendo. Kwa hiyo wapendeni ninyi pia! Lakini, wanangu, kumbukeni: upendo maana yake ni kuvumilia na kutoa na kutohukumu kamwe. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Moyo wangu usio na doa unatoka damu nikiwaangalieni katika dhambi na mazoea mabaya. Nawaalika: mrudieni Mungu na salini ili mpate kufanikiwa duniani. Mungu anawaalika kwa njia yangu ili mioyo yenu iwe tumaini na furaha kwa wale wote walio mbali. Ombi langu liwe kwenu manukato kwa nafsi na moyo ili mtukuze Mungu Mwumbaji anayewapenda na kuwaalika kwa mambo ya milele. Wanangu, maisha ni mafupi, mtumie nafasi hii kwa ajili ya kutenda mema. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Mwanangu, aliye mwanga wa upendo, yote aliyoyafanya na anayoyafanya hufanya kwa ajili ya upendo. Vivyo hivyo nanyi, wanangu, mnapoishi katika upendo, mnapompenda jirani yenu na mnapofanya mapenzi yake. Enyi mitume wa upendo wangu, jifanyeni wadogo! Mfungulieni Mwanangu mioyo yenu safi, ili Yeye aweze kutenda kazi kwa njia yenu. Kwa msaada wa imani, mjijazie upendo. Lakini, wanangu, msisahau ya kuwa Ekaristi ndiyo kiini cha imani. Yeye ndiye Mwanangu anayewalisheni kwa Mwili wake na kuwaimarisheni kwa Damu yake. Yeye ndiye ajabu ya upendo: Mwanangu ajaye tena mwenye uhai ili kuzifufua nafsi. Wanangu, mkiishi katika upendo, ninyi mnafanya mapenzi ya Mwanangu naye huishi ndani yenu. Wanangu, matakwa yangu ya kimama ni kwamba mpendeni zaidi na zaidi, maana Yeye anawapenda kwa upendo wake. Anawapa upendo wake ili muweze kuueneza kwa watu wote kandokando yenu. Kwa njia ya upendo wake, kama mama mimi nipo pamoja nanyi kuwaambieni maneno ya upendo na matumaini, kuwaambieni maneno ya milele na ya kushinda wakati na mauti, kuwaalikeni kuwa mitume wangu wa upendo. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama ninawaalika ili kwa moyo safi na wazi, kwa imani kabisa, mpokee upendo mkubwa wa Mwanangu. Mimi ninajua ukuu wa upendo wake, mimi nilimchukua ndani yangu, Hostia moyoni, Mwanga na Upendo wa ulimwengu. Wanangu, hata kuelekea kwangu kwenu ninyi ni ishara ya upendo na ya huruma ya Baba wa Mbinguni, ni tabasamu kilichojaa upendo wa Mwanangu, ni mwaliko kwa uzima wa milele. Damu ya Mwanangu ilimwagika kwa ajili yenu kwa upendo. Ile Damu yenye thamani ni kwa wokovu wenu, kwa ajili ya uzima wa milele. Baba wa mbinguni aliumba mtu kwa ajili ya furaha ya milele. Haiwezekani ninyi kufa, ninyi mnaojua upendo wa Mwanangu, ninyi mnaomfuata. Uzima umeshinda: Mwanangu yu hai! Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, sala iwaonyeshe njia, jinsi ya kueneza upendo wa Mwanangu kwa jinsi ilivyo bora zaidi. Wanangu, hata wakati mnapojaribu kuishi maneno ya Mwanangu, ninyi mnasali. Wakati mnapowapenda watu mnaokutana nao, mnaeneza upendo wa Mwanangu. Upendo ni neno linalofungua milango ya Uzima. Wanangu, tangu awali nimesali kwa ajili ya Kanisa. Kwa hiyo ninawaalika nanyi, mitume wa upendo wangu, kusali kwa ajili ya Kanisa na watumishi wake, kwa wale ambao Mwanangu amewaita. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nilichaguliwa kuwa mama wa Mungu na mama yenu, kwa maamuzi na upendo wa Bwana, lakini pia kwa mapenzi yangu, kwa upendo wangu usio na kifani kwake Baba wa mbinguni na kwa imani yangu yote Kwake. Mwili wangu ulikuwa kikombe cha Mungu Mtu. Nilikuwa mtumishi wa ukweli, wa upendo na wokovu kama vile nilivyo sasa katikati yenu, ili kuwaalika, wanangu, mitume wa upendo wangu, kuwa waletaji ukweli, ili kuwaalika, kwa njia ya utashi na upendo yenu kumwelekea Mwanangu, ili kueneza maneno Yake, maneno ya wokovu na kuyaonyesha, kwa vitendo vyenu, kwa wale wote ambao hawajamjua mwanangu na upendo Wake. Nguvu mtaipata katika Ekaristi: Mwanangu awalisheni kwa mwili Wake na kuwaimarisha kwa damu Yake. Wanangu, wekeni mikono yenu pamoja kwa sala na tazameni kuelekea msalaba kwa ukimya. Kwa jinsi hii mtapata imani ili muweze kuieneza, mtapata ukweli ili muweze kuupambanua, mtapata upendo ili muweze kuelewa namna ya kupenda kwa uhakika. Wanangu, mitume wa upendo wangu, wekeni mikono yenu pamoja kwa sala na tazameni kuelekea msalaba: katika msalaba tu kuna wokovu. Ninawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`