Our Lady of Medjugorje Messages containing 'hawajajua'

Total found: 7
Wanangu wapendwa! Mimi, Mama yenu, nipo pamoja nanyi kwa ajili yenu, kwa mahitaji yenu na mafundisho yenu binafsi. Baba wa Mbinguni amewapa uhuru wa kuamua peke yenu na kujua peke yenu. Mimi nataka kuwasaidieni. Nataka kuwa Mama kwenu, mwalimu wa ukweli, ili kwa unyofu wa moyo wazi mjue usafi usio na mwisho, na mwanga utokao kwa hiyo ukweli ili kutawanya giza, yaani mwanga uletao tumaini. Mimi, wanangu, naelewa maumivu yenu na mateso yenu. Nani aweza kuwaelewa zaidi kuliko Mama mmoja! Lakini enyi wanangu? Mjue kuwa idadi ya wanaonielewa na kunifuata ni ndogo. Pia ni kubwa idadi ya waliopotea, hao ambao hawajajua ukweli ulio katika Mwanangu. Kwa hiyo, enyi mitume wangu, salini na tendeni kazi. Mbebe mwanga, msipoteze tumaini. Mimi nipo nanyi na hasa pamoja na wachungaji wenu. Nawapenda na kuwalinda kwa Moyo wa kimama, ili kusudi wao wanawaongozeni Paradisini alikowaahidia Mwanangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, mimi nipo pamoja nanyi kwa baraka ya Mwanangu, pamoja nanyi mnaonipenda na mnaotafuta kunifuata. Mimi natamani kuwa pia pamoja nanyi ambao hamtaki kunipokea. Kwenu nyote nafungua moyo wangu wote wa mapendo na kuwabariki kwa mikono yangu ya kimama. Mimi ni Mama ninayewaelewa: nilikuwa nimeishi maisha yenu na kujaribu mateso na furaha yenu. Ninyi mnaoishi katika mateso, mnafahamu maumivu yangu na mateso yangu kwa ajili ya wale wanangu wasiokubali kuangazwa na mwanga wa Mwanangu, kwa wale wanangu wanaoishi gizani. Kwa hiyo nawahitaji ninyi, ninyi mlioangazwa na mwanga na kuufahamu ukweli. Nawaalika kumwabudu Mwanangu, ili moyo wenu ukue na kuyafikia kweli maisha ya kiroho. Basi mitume wangu, natumaini mtaweza kunisaidia. Kunisaidia maana yake ni kuwaombea wale ambao hawajajua upendo wa Mwanangu. Mkiwaombea, mtamwonyesha Mwanangu ya kuwa mnampenda na kumfuata. Mwanangu aliniahidi kwamba uovu hautashinda kamwe, kwa sababu hapo mpo ninyi, roho za wenye haki: ninyi mnaojaribu kusali sala zenu kwa moyo wote; ninyi mnaotolea maumivu na mateso yenu kwa Mwanangu; ninyi mnaofahamu ya kuwa maisha ni kufumba na kufumbua tu; ninyi mnaotamani Ufalme wa mbinguni. Hayo yote huwafanya muwe mitume wangu na kuwaongoza kwenye shangwe ya Moyo wangu. Kwa hiyo wanangu, takaseni mioyo yenu mkamwabudu Mwanangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, kulingana na mapenzi ya Mwanangu na upendo wangu wa kimama naja kwenu, wanangu, hasa kwa wale ambao hawajajua bado upendo wa Mwanangu. Ninakuja kwenu mnaonifikiria, mnaoomba msaada wangu. Ninawapa upendo wangu wa kimama na kuwaletea baraka ya Mwanangu. Mnayo mioyo safi na wazi? Mnaona dalili za uwepo wangu na upendo wangu? Wanangu, katika maisha yenu ya dunia igieni moyo na mfano wangu. Maisha yangu yalikuwa maumivu, ukimya, imani na matumaini pasipo mipaka katika Baba wa Mbinguni. Hakuna kitu cha bahati: si maumivu, si furaha, si mateso, si upendo. Hizo zote ni neema ambazo Mwanangu anawapeni na zinazowaongoza kwenye uzima wa milele. Mwanangu anawaomba mapendo na sala ndani yake. Kupenda na kusali ndani yake maana yake — kama Mama nataka kuwafundisha — ni kusali katika ukimya wa nafsi zenu, si kusema kwa midomo tu. Ni tendo dogo zuri litendwalo kwa jina la Mwanangu; ni uvumilivu, rehema, upokeaji wa maumivu na kujitolea kwa ajili ya wengine. Wanangu, Mwanangu huwatazama. Ombeni ili ninyi pia muuone uso wake, na ili uso huo uweze kufunuliwa kwenu. Wanangu, mimi nawafunulia ukweli halisi wa pekee. Salini kwa kuyaelewa na kuweza kueneza mapendo na matumaini, kwa kuweza kuwa mitume wa upendo wangu. Moyo wangu wa kimama hupenda hasa wachungaji. Iombeeni mikono yao iliyobarikiwa. Nawashukuru.
Wanangu, Moyo wangu wa kimama unateseka wakati ninapotazama wanangu wasiopenda ukweli, wanaouficha; wakati ninapotazama wanangu wasiosali kwa moyo wala kwa matendo. Nimesikitika wakati ninapomwambia Mwanangu ya kuwa wana wangu wengi hawana imani tena, ya kuwa hawamjui Yeye, Mwanangu. Kwa hiyo ninawaalika, mitume wa upendo wangu: mjaribu kutazama mpaka ndani ya mioyo ya watu, na kule bila shaka mtapata hazina ndogo iliyofichwa. Kutazama hivyo ni rehema ya Baba wa mbinguni. Kutafuta mema hata palipo maovu makubwa zaidi, kutafuta kuwaelewana wala kutohukumiana: hilo ni neno ambalo Mwanangu anawaombeni. Nami, kama Mama, ninawaalika kumsikiliza. Wanangu, roho ni yenye nguvu kuliko mwili na, ikichukuliwa na upendo na matendo hushinda vikwazo vyote. Msisahau: Mwanangu aliwapendeni na anawapenda. Upendo wake ni pamoja nanyi na ndani yenu, wakati mpo kitu kimoja pamoja naye. Yeye ni mwanga wa ulimwengu, na hakuna mtu wala kitu kiwezacho kumsimamisha katika utukufu wa mwisho. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, msiwe na hofu ya kushuhudia ukweli! Ushuhudieni kwa hamu, kwa matendo, kwa upendo, kwa sadaka yenu, lakini hasa kwa unyenyekevu. Shuhudieni ukweli kwa wale ambao hawajajua Mwanangu. Mimi nitakuwa karibu nanyi, mimi nitawatia moyo. Shuhudieni upendo usioishi tena, maana huja kutoka Baba wa mbinguni ambaye ni wa milele na anawatolea wana wangu wote umilele. Roho wa Mwanangu itakuwa karibu nanyi. Ninawaalika tena, wanangu: muwaombee wachungaji wenu, ombeni ili upendo wa Mwanangu uweze kuwaongoza. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Salini kila siku Tasbihi, taji lile la maua linaloniungana moja kwa moja kama Mama kwa maumivu yenu, mateso, mahitaji na matumaini. Mitume wa upendo wangu, Mimi nipo pamoja nanyi kwa njia ya neema na upendo wa Mwanangu, nanyi ninawaombeni sala. Sala zenu zinahitajika sana ulimwenguni, ili roho ziongoke! Fungueni wazi kwa imani timilifu mioyo yenu kwa Mwanangu, na yeye ataandika ndani yao muhtasari wa Neno lake, yaani upendo. Ishini muungano usiotenganika na Moyo Mtakatifu sana wa Mwanangu! Wanangu, kama Mama nawaambieni ya kwamba hakuna wakati wa kupoteza ili kupiga magoti mbele ya Mwanangu, kumkiri kama Mungu wenu, aliye kitovu cha maisha yenu. Mtoeni karama, zile anazozipenda zaidi, yaani upendo kwa jirani yako, rehema na mioyo safi. Mitume wa upendo wangu, wanangu wengi bado hawajamkiri Mwanangu kama Mungu wao, bado hawajajua upendo wake. Lakini ninyi, kwa njia ya sala yenu inayosema kwa moyo safi na wazi, pamoja na karama mnazotoa kwa Mwanangu, mtasababisha kwamba hata mioyo migumu zaidi ifunguke. Mitume wa upendo wangu, nguvu ya sala inayosemwa kutokana na moyo, ya sala yenye nguvu na iliyojaa upendo, hugeuza ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini! Mimi nipo pamoja nanyi.. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, Mwanangu mpenzi alimwomba sikuzote na kumtukuza Baba wa Mbinguni. Sikuzote alikuwa amemwambia yote na kujiachia katika mapenzi yake. Hivyo mnapaswa kufanya hata ninyi, wanangu, maana Baba wa Mbinguni anawasikiliza sikuzote wanawe. Moyo wa umoja katika moyo mmoja: upendo, mwanga na uhai. Baba wa Mbinguni amejitolea kwa njia ya sura ya kibinadamu, na sura ile ndiyo sura ya Mwanangu. Ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnapaswa sikuzote kupokea sura ya Mwanangu katika mioyo yenu na katika fikira zenu. Ninyi mnapaswa sikuzote kuufikiria upendo wake na sadaka yake. Mnapaswa kusali ili kusudi mwone uwepo wake sikuzote. Maana, enyi mitume wa upendo wangu, hii ni jinsi ya kuwasaidia wale wote wasiomjua Mwanangu, wale ambao hawajajua upendo wake. Wanangu, someni kitabu cha Injili: ni sikuzote kitu kipya, ni kinachowaunganisha na Mwanangu, aliyezaliwa kwa kuwaletea maneno ya uzima wanangu wote na kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya wote. Mitume wa upendo wangu, mkisukumwa na upendo kumwelekea Mwanangu, leteni upendo na amani kwa ndugu zenu wote. Msimhukumu mtu, pendeni kila mtu kwa njia ya upendo kwa kumwelekea Mwanangu. Hivyo mtashughulika hata na roho zenu, nayo ni yenye thamani kuliko kitu chochote mlicho nacho. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, upendo wenu safi na wa kweli unavuta Moyo wangu wa kimama. Imani yenu na usadiki wenu katika Baba wa mbinguni ni mawaridi yenye harufu nzuri mnayonitolea: shada la mawaridi mazuri sana, lililotengenezwa kwa sala zenu, kwa matendo ya rehema na ya upendo. Mitume wa upendo wangu, ninyi mnaojaribu kumfuata Mwanangu pasipo unafiki na kwa moyo safi, ninyi ambao pasipo unafiki mnampenda, muwe ninyi wenyewe kusaidia: muwe mfano kwa wale ambao hawajajua upendo wa Mwanangu. Lakini, wanangu, siyo kwa maneno tu, bali hata kwa matendo na hisia safi, ambayo kwa njia yake mnamtukuza Baba wa mbinguni. Mitume wa upendo wangu, ni wakati wa kukesha na ninawaombeni upendo; na msihukumu mtu yeyote, kwa maana Baba wa mbinguni atahukumu wote. Ninawaombeni mpende, na mueneze ukweli, kwa maana ukweli ni wa kale: Ukweli siyo mpya, Ukweli ni wa milele, Ukweli ndiyo ukweli! Ukweli unatolea ushuhuda wa umilele wa Mungu. Bebeni mwanga wa Mwanangu na mpasue giza ambalo linataka kuwakandamiza zaidi na zaidi. Msiwe na hofu: kwa ajili ya neema na upendo wa Mwanangu, mimi nipo pamoja nanyi! Ninawashukuru. ”
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`