Our Lady of Medjugorje Messages containing 'hupenda'

Total found: 6
Wanangu wapendwa, kwa moyo wa kimama nawaalikeni tena kupenda, kusali bila kukata tamaa kwa zawadi ya upendo, kumpenda Baba wa Mbinguni zaidi ya yote. Mtakapompenda Yeye, mtajipenda wenyewe na jirani zenu. Mambo hayo hayawezi kutengana. Baba wa Mbinguni yumo katika kila mtu, hupenda kila mtu na kumwita kila mtu kwa jina lake. Kwa hiyo, wanangu, kwa njia ya kusali sikilizeni atakalo Baba wa Mbinguni. Ongeeni na Yeye. Muwe na uhusiano wa binafsi pamoja na Baba, atakayeufanya mkubwa zaidi uhusiano wake nanyi, jumuhiya ya wanangu, mitume wangu. Kama Mama napenda kwamba, kwa njia ya upendo kumwelekea Baba wa Mbinguni, inukeni juu ya ubatili wa malimwengu na muwasaidie wengine kujua na kumjongea polepole Baba wa Mbinguni. Wanangu, salini, salini, salini kwa zawadi ya upendo, kwa sababu upendo ndiye Mwanangu. Muwaombee wachungaji wenu, ili wawapende ninyi siku zote, kama vile Mwanangu alivyowapenda ninyi na kuonyesha akitoa maisha yake kwa wokovu wenu. Nawashukuruni.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama nawaombeni: pendaneni! mioyoni mwenu muwe kama Mwanangu alitaka tangu awali: kwanza kabisa kumpenda Baba wa Mbinguni na kuwa na upendo kwa jirani yenu, kuliko yote yaliyopo hapa duniani. Wanangu wapendwa, hamtambui dalili za nyakati hizi? Hamtambui ya kuwa yote yanayotokea kando kando yenu, hutokea kwa sababu hakuna upendo? Fahamuni kwamba wokovu hupatikana katika thamani za kweli, pokeeni uweza wa Baba wa Mbinguni, mpendeni na kumheshimu. Fuateni njia ya Mwanangu. Ninyi, wanangu, mitume wangu wapenzi, mnakusanyika siku zote daima kunizunguka maana mna kiu, mna kiu ya amani, ya upendo na ya furaha. Kateni kiu yenu katika mikono yangu! Mikono yangu yawatolea Mwanangu, aliye chemchemi ya maji safi. Yeye atafufua imani yenu na kusafisha mioyo yenu, kwa sababu Mwanangu hupenda kwa moyo safi na mioyo iliyo safi humpenda Mwanangu. Mioyo safi tu ndiyo minyenyekevu na yenye imani thabiti. Wanangu, nawaombeni ya kuwa na mioyo ya namna hii! Mwanangu aliniambia ya kuwa Mimi ni Mama wa ulimwengu wote: nawaombeni ninyi, mnaonipokea kama Mama, ili kwa maisha yenu, sala na sadaka nisaidieni ili wanangu wote wanipokee kama Mama, niweze kuwaongoza kwenye chemchemi ya maji safi. Nawashukuru! Wanangu wapenzi, wachungaji wenu wanapowatolea mwili wa Mwanangu, mshukuruni Mwanangu daima moyoni mwenu kwa sadaka yake na kwa wachungaji anayewajalia siku zote.
Wanangu wapendwa, ninyi ni nguvu yangu. Ninyi, mitume wangu, ambao, kwa upendo wenu, unyenyekevu na sala ya kimya kimya, mnamwezesha Mwanangu ajulikane. Ninyi mnaishi ndani yangu. Ninyi mnanibeba mioyoni mwenu. Ninyi mnajua ya kuwa mna Mama awapendaye na aliyekuja kuwaletea upendo. Nawatazama katika Baba wa Mbinguni, natazama fikira zenu, maumivu yenu, mateso yenu na kuyaleta kwa Mwanangu. Msiogope! Msipoteze matumaini, maana Mwanangu humsikiliza Mama yake. Yeye hupenda tangu alipozaliwa, na ndio furaha yangu ya kuwa wanangu wote wajue upendo huo; na wote wale ambao, kwa sababu ya maumivu yao na kutoelewa kwao, walimwacha waweze kurudi kwake, na wote wao wasiomjua wamjue. Kwa sababu hiyo ninyi hapa ni mitume wangu, nami pia pamoja nanyi kama Mama yenu. Salini ili kuwa imara katika imani, maana upendo na rehema hutoka katika imani imara. Kwa njia ya upendo na rehema mtawasaidia wale wote wasiofahamu ya kuwa wanachagua giza badala ya nuru. Salini kwa ajili ya wachungaji wenu, maana wao ni nguvu ya Kanisa ambayo Mwanangu aliwaachieni. Kwa njia ya Mwanangu wao ni wachungaji wa roho. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kama Mama nafurahi ya kuwa katikati yenu, kwa maana nataka kuongea nanyi tena kuhusu maneno ya Mwanangu na upendo wake. Natumaini mtanipokea kwa upendo, maana maneno ya Mwanangu na upendo wake ni nuru na tumaini la pekee katika giza la siku hizi. Huu ni ukweli wa pekee, nanyi mtakaoupokea na kuuishi, mtakuwa na mioyo safi na minyenyekevu. Mwanangu hupenda mioyo safi na minyenyekevu. Mioyo safi na minyenyekevu inahuisha maneno ya Mwanangu: inayaishi, inayaeneza na kufanya hata wote wayasikie. Maneno ya Mwanangu yanaamsha maisha ya wale wanaoyasikiliza, maneno ya Mwanangu hurudisha upendo na matumaini. Kwa hiyo, mitume wangu wapenzi, wanangu, isheni maneno ya Mwanangu. Pendaneni kama Yeye alivyowapenda. Pendaneni katika jina lake na kumbukumbu lake. Kanisa huendelea na kukua kwa ajili ya wale wanaosikiliza maneno ya Mwanangu, kwa sababu ya wanaohuzunika na kuteseka kimyakimya katika tumaini la kukombolewa milele. Kwa hiyo wanangu wapendwa, maneno ya Mwanangu na upendo wake yawe wazo la kwanza na la mwisho la siku yenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kulingana na mapenzi ya Mwanangu na upendo wangu wa kimama naja kwenu, wanangu, hasa kwa wale ambao hawajajua bado upendo wa Mwanangu. Ninakuja kwenu mnaonifikiria, mnaoomba msaada wangu. Ninawapa upendo wangu wa kimama na kuwaletea baraka ya Mwanangu. Mnayo mioyo safi na wazi? Mnaona dalili za uwepo wangu na upendo wangu? Wanangu, katika maisha yenu ya dunia igieni moyo na mfano wangu. Maisha yangu yalikuwa maumivu, ukimya, imani na matumaini pasipo mipaka katika Baba wa Mbinguni. Hakuna kitu cha bahati: si maumivu, si furaha, si mateso, si upendo. Hizo zote ni neema ambazo Mwanangu anawapeni na zinazowaongoza kwenye uzima wa milele. Mwanangu anawaomba mapendo na sala ndani yake. Kupenda na kusali ndani yake maana yake — kama Mama nataka kuwafundisha — ni kusali katika ukimya wa nafsi zenu, si kusema kwa midomo tu. Ni tendo dogo zuri litendwalo kwa jina la Mwanangu; ni uvumilivu, rehema, upokeaji wa maumivu na kujitolea kwa ajili ya wengine. Wanangu, Mwanangu huwatazama. Ombeni ili ninyi pia muuone uso wake, na ili uso huo uweze kufunuliwa kwenu. Wanangu, mimi nawafunulia ukweli halisi wa pekee. Salini kwa kuyaelewa na kuweza kueneza mapendo na matumaini, kwa kuweza kuwa mitume wa upendo wangu. Moyo wangu wa kimama hupenda hasa wachungaji. Iombeeni mikono yao iliyobarikiwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Mwanangu alikuwa chemchemi ya upendo na mwanga alipoongea na watu wa mataifa yote. Mitume wangu, fuateni mwanga wake, si rahisi, yawapasa kuwa wadogo, yawapasa kuwa wadogo kuliko wengine wote na kwa msaada wa imani kujazwa na upendo wake. Hakuna mtu duniani, pasipo imani, awezaye kuwa na uzoefu wa mwujiza. Mimi nipo pamoja nanyi, ninajionyesha kwa matokeo hayo, kwa maneno hayo, nataka kuwashuhudia upendo wangu na utunzaji wangu wa kimama. Wanangu, msipoteze wakati mkiweka maswali ambayo hamtapata kamwe majibu, maisha yenu duniani yatakapomalizika Baba wa Mbinguni atawajibu. Mjue daima ya kuwa Mungu hujua yote, Mungu huona, Mungu hupenda. Mwanangu mpenzi sana huangaza maisha na kupasua giza. Upendo wa kimama unaonileta kwenu hauelezeki, umefichwa lakini ni halisi, ninawaonyesheni hisia zangu, upendo, hisani na ukarimu wangu wa kimama. Kutoka kwenu, mitume wangu, ninatafuta sala zenu: mawaridi yaliyo matendo ya upendo, hizo ndizo kwa moyo wangu wa kimama sala za kunipendeza sana, haya ninayaletea Mwanangu aliyezaliwa kwa ajili yenu. Yeye anawatazama ninyi na kuwasikia. Sisi tupo kila siku karibu nanyi kwa upendo wenu ambao huita, huunga, huongoa, hutia moyo na kujaza. Kwa hiyo mitume wangu pendaneni daima, lakini hasa mpende Mwanangu, hii ni njia ya pekee ya wokovu kuelekea uzima wa milele, hiyo ni sala ya kunipendeza ambayo kama harufu nzuri ajabu ya mawaridi, hujaa moyo wangu. Ombeni daima, waombeeni wachungaji wenu ili wapate nguvu ya kuwa mwanga wa Mwanangu. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`