Our Lady of Medjugorje Messages containing 'kugeuza'

Total found: 4
Wanangu wapendwa, nataka kufanya kazi kwa njia yenu, wanangu, mitume wangu, ili mwishowe niweze kukusanya wanangu wote pale ambapo pameandaliwa tayari kwa ajili ya furaha yenu. Nawaombea, kusudi kwa matendo yenu muweze kugeuza, kwani muda umefika kwa matendo ya kweli, kwa ajili ya Mwanangu. Upendo wangu utafanya kazi ndani mwenu, nitawatumia ninyi. Muwe na imani nami, kwani yote ninayotamani, ninayatamani kwa ajili yenu, wema wa milele, ulioumbwa kwa njia ya Baba wa Mbinguni. Ninyi, wanangu, mitume wangu, muishi maisha ya duniani pamoja na wanangu ambao hawafahamu upendo wa Mwanangu, wale ambao hawaniiti mama. Lakini msiogope kushuhudia ukweli, kwa maana ikiwa ninyi hamtaogopa na kushuhudia ukweli kwa uhodari, ukweli utashinda kimuujiza. Kumbukeni: nguvu iko katika upendo. Wanangu, upendo ndio kutubu, kusamehe, kusali, kujitoa sadaka na rehema, maana mkijua kupenda kwa matendo mtawabadilisha na wengine, mtawezesha mwanga wa Mwanangu uingie katika mioyo yao. Nawashukuru. Muwaombee wachungaji wenu, wao ni mali ya Mwanangu. Yeye aliwaita. Salini ili wawe siku zote na nguvu na uhodari wa kung'aa kwa nuru ya Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nimewaalika na ninawaalika tena kumjua Mwanangu, kuujua ukweli. Mimi nipo pamoja nanyi na ninasali ili mfanikiwe. Wanangu, yawapasa kusali sana ili kupata upendo na uvumilivu mwingi kadiri muwezavyo, ili kuweza kuvumilia sadaka na kuwa maskini rohoni. Mwanangu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, yu sikuzote pamoja nanyi. Kanisa lake huzaliwa katika kila moyo unaomjua. Salini ili muweze kumjua Mwanangu, salini ili roho yenu iwe kitu kimoja pamoja naye. Hiyo ndiyo sala na huo ndio upendo wa kuwavutia wengine na kuwafanyeni kuwa mitume wangu. Ninawatazama kwa upendo, kwa upendo wa kimama. Ninawajua, najua maumivu yenu na mateso yenu, kwa maana Mimi nami niliteswa kimya. Imani yangu ilinipa upendo na tumaini. Ninawaambieni tena: Ufufuo wa Mwanangu na Kupokewa kwangu mbinguni ni tumaini na upendo kwa ajili yenu. Kwa hiyo, wanangu, salini ili kujua ukweli, ili kupata imani thabiti, ya kuongoza mioyo yenu na kuweza kugeuza mateso yenu na maumivu yenu kuwa upendo na tumaini. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, maneno yangu ni manyofu lakini yamejaa upendo wa kimama na mahangaiko. Wanangu, juu yenu vivuli vya giza na vya udanganyifu vinaenea zaidi na zaidi, mimi ninawaiteni kuelekea mwanga na ukweli, mimi ninawaita kuelekea Mwanangu. Yeye peke yake huweza kugeuza kukata tamaa na maumivu yetu kuwa amani na utulivu, Yeye peke yake huweza kutoa matumaini katika maumivu makali sana. Mwanangu ni uzima wa ulimwengu, kwa kadiri mtakavyomjua, ndivyo mtakavyomkaribia na kumpenda maana Mwanangu ni upendo, na upendo unageuza yote. Yeye hufanya la ajabu hata neno lisilo la maana bila upendo machoni penu. Kwa hiyo nawaambieni tena ya kwamba mnapaswa kupenda sana ikiwa mnatamani kukua kiroho. Najua, enyi mitume wa upendo wangu, kwamba si rahisi sikuzote, lakini, wanangu, hata njia ngumu ni njia zinazoongoza kwenye ukuaji wa kiroho, wa kiimani na kwa Mwanangu. Wanangu, salini, mfikirie Mwanangu, nyakati zote za siku zenu inueni nafsi zenu kwake nami nitakusanya sala zenu kama maua kutoka bustani nzuri kuliko zote na kumpa Mwanangu. Muwe hakika mitume wa upendo wangu, wapeni wote upendo wa Mwanangu, muwe bustani zenye maua mazuri kuliko yote. Kwa njia ya sala saidieni wachungaji wenu ili waweze kuwa baba za kiroho waliojaa upendo kwa watu wote. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Salini pamoja Nami kwa maisha mapya ya ninyi nyote. Wanangu, katika mioyo yenu mnajua ni nini lazima kibadilike: rudini kwa Mungu na kwa Amri Zake ili Roho Mtakatifu aweze kugeuza maisha yenu na uso wa dunia hii, inayohitaji kufanywa upya katika Roho. Wanangu, muwe sala kwa wale wote wasiosali, muwe furaha kwa wale wote wasioona njia ya kutokea, muwe waletaji mwanga katika giza za wakati huu wa wasiwasi. Salini na ombeni msaada na ulinzi wa watakatifu ili ninyi pia muweze kutamani mbingu na mambo halisi ya kimbingu. Mimi nipo pamoja nanyi nikiwalinda na kuwabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`