Our Lady of Medjugorje Messages containing 'kujua'

Total found: 10
Wanangu wapendwa, katika wakati huu wa wasiwasi nawaalikeni tena kutembea nyuma ya Mwanangu, na kumfuata. Nayajua maumivu, mateso na taabu zenu, lakini katika Mwanangu mtapumzika, ndani yake mtapata amani na wokovu. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu amewakomboa ninyi kwa msalaba wake akawajalieni kuwa tena wana wa Mungu na kuwafundisha kumwita tena "Baba" yenu, Mungu aliye mbinguni. Ili muwe wapenzi wa Mungu Baba, basi muwe na mapendo na msamaha, kwa kuwa Baba yenu ni upendo na msamaha. Salini na fungeni, kwa maana hii ndiyo njia ya kujua na kumfahamu Baba aliye mbinguni. Mtakapomjua huyo Baba, mtafahamu ya kuwa Yeye tu ni muhimu kwenu (Maria Mtakatifu amenena hayo kwa nguvu na amkazo sana). Mimi, nikiwa Mama, nataka wanangu wawe watu wenye umoja ambamo Neno la Mungu husikilizwa na kutekelezwa. Kwa hiyo, enyi wanangu, mfuateni Mwanangu, muwe kitu kimoja naye, muwe wana wa Mungu. Pendeni wachungaji wenu kama vile Mwanangu alivyowapenda alipowaita kuwatumikia ninyi. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, kwa moyo wa kimama nawaalikeni tena kupenda, kusali bila kukata tamaa kwa zawadi ya upendo, kumpenda Baba wa Mbinguni zaidi ya yote. Mtakapompenda Yeye, mtajipenda wenyewe na jirani zenu. Mambo hayo hayawezi kutengana. Baba wa Mbinguni yumo katika kila mtu, hupenda kila mtu na kumwita kila mtu kwa jina lake. Kwa hiyo, wanangu, kwa njia ya kusali sikilizeni atakalo Baba wa Mbinguni. Ongeeni na Yeye. Muwe na uhusiano wa binafsi pamoja na Baba, atakayeufanya mkubwa zaidi uhusiano wake nanyi, jumuhiya ya wanangu, mitume wangu. Kama Mama napenda kwamba, kwa njia ya upendo kumwelekea Baba wa Mbinguni, inukeni juu ya ubatili wa malimwengu na muwasaidie wengine kujua na kumjongea polepole Baba wa Mbinguni. Wanangu, salini, salini, salini kwa zawadi ya upendo, kwa sababu upendo ndiye Mwanangu. Muwaombee wachungaji wenu, ili wawapende ninyi siku zote, kama vile Mwanangu alivyowapenda ninyi na kuonyesha akitoa maisha yake kwa wokovu wenu. Nawashukuruni.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama na uvumilivu wa kimama naona kutangatanga kwenu na kuendelea kupotea kwenu. Kwa sababu hiyo mimi nipo pamoja nanyi. Nataka kwanza kabisa kuwasaidieni kupata kujijua ninyi wenyewe, ili baadaye muweze kuelewa na kutambua yote yanayowazuia kujua bila unafiki na kwa moyo wote upendo wa Baba wa Mbinguni. Wanangu, Baba hujulikana kwa njia ya msalaba: kwa hiyo msikatae msalaba: kwa msaada wangu, mkafanye bidii kuuelewa na kuupokea. Mtakapoweza kuupokea msalaba, mtaelewa pia upendo wa Baba wa Mbinguni. Mtatembea pamoja na Mwanangu na mimi. Mtajipambanua na wale ambao hawakujua upendo wa Baba wa Mbinguni, kujitofautisha na wale wanaomsikiliza lakini hawamwelewi, na wale wasioenda pamoja naye, na wasiomjua. Mimi nataka ninyi mjue ukweli wa Mwanangu na muwe mitume wangu; ili, kama wana wa Mungu, muwe na mawazo yaliyo juu ya mawazo ya kibinadamu na siku zote na katika yote mkatafute kila mara mawazo ya Mungu. Wanangu, salini na fungeni ili muweze kuelewa yote ninayowaombeni. Muombee wachungaji wenu mkatamani kujua, mkishirikiana nao, upendo wa Baba wa Mbinguni. Nawashukuruni.
Wanangu wapendwa! Mimi, Mama yenu, nipo pamoja nanyi kwa ajili yenu, kwa mahitaji yenu na mafundisho yenu binafsi. Baba wa Mbinguni amewapa uhuru wa kuamua peke yenu na kujua peke yenu. Mimi nataka kuwasaidieni. Nataka kuwa Mama kwenu, mwalimu wa ukweli, ili kwa unyofu wa moyo wazi mjue usafi usio na mwisho, na mwanga utokao kwa hiyo ukweli ili kutawanya giza, yaani mwanga uletao tumaini. Mimi, wanangu, naelewa maumivu yenu na mateso yenu. Nani aweza kuwaelewa zaidi kuliko Mama mmoja! Lakini enyi wanangu? Mjue kuwa idadi ya wanaonielewa na kunifuata ni ndogo. Pia ni kubwa idadi ya waliopotea, hao ambao hawajajua ukweli ulio katika Mwanangu. Kwa hiyo, enyi mitume wangu, salini na tendeni kazi. Mbebe mwanga, msipoteze tumaini. Mimi nipo nanyi na hasa pamoja na wachungaji wenu. Nawapenda na kuwalinda kwa Moyo wa kimama, ili kusudi wao wanawaongozeni Paradisini alikowaahidia Mwanangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, mimi, Mama yenu, naja tena katikati yenu kwa upendo usio na mwisho, kutoka upendo usio na kipimo wa Baba wa Mbinguni asiye na mwisho. Na, nikitazama mioyoni mwenu, naona ya kuwa wengi wenu wanipokea kama Mama na, kwa moyo thabiti na safi, wataka kuwa mitume wangu. Lakini Mimi ni Mama pia wa ninyi ambao hamnipokei na, katika ugumu wa moyo wenu, hamtaki kujua upendo wa Mwanangu. Hamjui jinsi moyo wangu ulivyoteseka na jinsi nilivyowaombeeni Mwanangu. Namwomba aponye roho yenu, kwa maana najua Yeye ana uwezo wa kuwaponya. Namwomba awaangaze kwa mwujiza wa mwanga wa Roho Mtakatifu, ili mwache kumsaliti, kumtukana na kumwumiza siku zote kwa kuendelea. Nasali kwa Moyo wote ili muweze kuelewa ya kuwa Mwanangu tu ni wokovu na mwanga wa ulimwengu. Nanyi, wanangu, mitume wangu wapenzi, mbebeni daima Mwanangu katika moyo na fikira zenu. Hivyo ninyi mtakuwa mnabeba Upendo. Wale wote wasiomjua watamtambua katika upendo wenu. Mimi nipo sikuzote karibu yenu. Nipo hasa karibu na wachungaji wenu, kwa sababu Mwanangu aliwaita kuwaongozeni katika njia kuelekea milele. Nawashukuru, mitume wangu, kwa sadaka na upendo wenu!
Wanangu wapendwa, nimewaalika na ninawaalika tena kumjua Mwanangu, kuujua ukweli. Mimi nipo pamoja nanyi na ninasali ili mfanikiwe. Wanangu, yawapasa kusali sana ili kupata upendo na uvumilivu mwingi kadiri muwezavyo, ili kuweza kuvumilia sadaka na kuwa maskini rohoni. Mwanangu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, yu sikuzote pamoja nanyi. Kanisa lake huzaliwa katika kila moyo unaomjua. Salini ili muweze kumjua Mwanangu, salini ili roho yenu iwe kitu kimoja pamoja naye. Hiyo ndiyo sala na huo ndio upendo wa kuwavutia wengine na kuwafanyeni kuwa mitume wangu. Ninawatazama kwa upendo, kwa upendo wa kimama. Ninawajua, najua maumivu yenu na mateso yenu, kwa maana Mimi nami niliteswa kimya. Imani yangu ilinipa upendo na tumaini. Ninawaambieni tena: Ufufuo wa Mwanangu na Kupokewa kwangu mbinguni ni tumaini na upendo kwa ajili yenu. Kwa hiyo, wanangu, salini ili kujua ukweli, ili kupata imani thabiti, ya kuongoza mioyo yenu na kuweza kugeuza mateso yenu na maumivu yenu kuwa upendo na tumaini. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, wakati duniani upendo unapopunguka, wakati njia ya wokovu haipatikani, Mimi, Mama yenu, naja kuwasaidieni kujua imani ya kweli, iliyo hai na ya kina, na kuwasaidieni kupenda kabisa. Kama Mama ninatamani mpendane, muwe wema na safi. Ni hamu yangu muwe wenye haki na mpendane. Wanangu, muwe wafurahivu rohoni, muwe safi, muwe watoto. Mwanangu alisema kwamba anapenda kukaa kati ya wenye mioyo safi, maana wenye mioyo safi ni daima vijana na wafurahivu. Mwanangu aliwaambieni msameheane na mpendane. Najua kwamba si rahisi sikuzote. Mateso husababisha kukua rohoni. Ili kukua rohoni kadiri iwezekanavyo, lazima msamehe na kupenda kwa dhati na kwa kweli. Wana wangu wengi duniani hawamjui Mwanangu, hawampendi. Lakini ninyi mnaompenda Mwanangu na kumchukua moyoni salini, salini, na mkisali mumhisi Mwanangu karibu yenu. Nafsi yenu ipumue Roho yake! Mimi nipo kati yenu na kuongea juu ya mambo madogo na makubwa. Sitachoka kuwasimulieni habari ya Mwanangu, aliye upendo wa kweli. Kwa hiyo, wanangu, nifungulieni mioyo yenu, acheni niwaongoze kama mama. Muwe mitume wa upendo wa Mwanangu na wangu. Kama Mama nawasihi: msisahau wale walioitwa na Mwanangu wawaongoze. Wachukueni moyoni na muwaombee. Nawashukuru.
Wanangu, ninawaomba kuwa hodari wala kutowayawaya, maana hata mema madogo zaidi, ishara ya upendo mdogo zaidi hushinda maovu yanayoonekana zaidi na zaidi. Wanangu nisikilizeni ili mema yashinde, ili muweze kujua upendo wa Mwanangu ulio furaha mkubwa zaidi kuliko zote. Mikono ya mwanangu inawakumbatia, Yeye, apendaye nafsi, Yeye ambaye amejitolea kwa ajili yenu na kunajitolea sikuzote tena katika Ekaristi, Yeye aliye na maneno ya Uzima wa milele; kujua upendo wake, kufuata hatua zake, maana yake ni kuwa na mali ya kiroho. Huo ni utajiri unaojaza hisia iliyo njema, na unaoona upendo na mema popote. Mitume wa upendo wangu, wanangu, muwe kama mionzi ya jua ambayo kwa joto la upendo wa Mwanangu inawapasha joto wote wale wanaoizunguka. Wanangu, ulimwengu unahitaji mitume wa upendo, ulimwengu unahitaji sala nyingi, lakini sala zinazosaliwa kwa moyo na roho, si kwa midomo tu. Wanangu, muwe na hamu ya utakatifu mkiwa na unyenyekevu unaomwezesha Mwanangu kufanya kazi kwa njia yenu, kama Yeye apendavyo. Wanangu, sala zenu, fikira zenu na matendo yenu, haya yote yawafungulia ama kuwafungia mlango wa Ufalme wa Mbinguni. Mwanangu aliwaonyesha njia na kuwapa tumaini, mimi ninawafariji na kuwapa moyo maana, wanangu, mimi nilijua maumivu, lakini nilikuwa na imani na tumaini, sasa nimepata thawabu ya uzima katika Ufalme wa Mwanangu. Kwa hiyo, nisikilizeni, jipeni moyo, msiwayawaye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninawaita mitume wa upendo wangu. Ninawaonyesha Mwanangu, aliye amani ya kweli na upendo wa kweli. Kama Mama, kwa ajili ya neema ya kimungu, ninatamani kuwaongoza kwendea Yeye. Wanangu, kwa hiyo ninawaalika kujitazama ninyi wenyewe mkianzia kwa Mwanangu, kumtazama kwa moyo na kuona kwa moyo mahali mlipo na maisha yenu yanakwenda wapi. Wanangu, ninawaalika kuelewa ya kuwa mnaishi kwa ajili ya Mwanangu, kwa njia ya upendo wake na sadaka yake. Ninyi mnamwomba Mwanangu kuwa mwenye rehema nanyi, lakini mimi ninawaalika ninyi kuwa na rehema. Mnamwomba kuwa mwema nanyi na kuwasamehe, lakini tangu lini mimi ninawasihi ninyi, wanangu, kusamehe na kupenda watu wote mnaokutana nao! Mtakapoelewa kwa moyo maneno yangu, mtaelewa na kujua upendo wa kweli, na mtaweza kuwa mitume wa upendo ule, enyi mitume wangu, wanangu wapendwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Upendo wa Mwanangu ni mkubwa. Laiti mngeweza kujua ukuu wa upendo Wake, msingeacha kamwe kumwabudu na kumshukuru. Yeye ni sikuzote hai pamoja nanyi katika Ekaristi, maana Ekaristi ni moyo Wake, Ekaristi ni moyo wa imani. Yeye hakuwaacha kamwe: hata wakati ninyi mlipojaribu kwenda mbali Naye, Yeye hakuwaacha kamwe.

Kwa hiyo, moyo wangu wa kimama unafurahi wakati unapotazama jinsi mlivyojaa upendo mnapomrudia, wakati unapoona ya kuwa mnamrudia kwa njia ya upatanisho, upendo na matumaini. Moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa ikiwa mngetembea katika njia ya imani, mngekuwa kama machipukizi, kama matumba na kwa njia ya sala na kufunga mngekuwa kama matunda, kama maua, mitume wa upendo wangu, mngekuwa waleta mwanga na mngeangaza kwa upendo na hekima pande zote karibu nanyi.

Wanangu, kama mama, ninawaomba: salini, fikirini na kutafakari. Yote yanayowatokea, mazuri, ya kuumiza na ya kufurahisha, hayo yote yawasababisha kukua kiroho, yawafanya kuwa Mwanangu akue ndani yenu. Wanangu mkabidhi kwake. Mumwamini na mtumainie upendo Wake. Na Yeye awaongoze. Na Ekaristi iwe mahali mtakapolisha roho zenu ili kueneza upendo na ukweli. Shuhudieni Mwanangu. Ninawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`