Our Lady of Medjugorje Messages containing 'kukua'

Total found: 8
Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu kuwatieni moyo, kuwajaza kwa upendo wangu, kuwaalika tena kuwa mashahidi wa upendo wa Mwanangu. Wanangu wengi hawana tumaini, hawana amani, hawana upendo. Wao wanatafuta Mwanangu lakini hawajui jinsi wala wapi ya kumpata. Mwanangu awafungulia mikono Yake, nanyi wasaidieni ili waje mikononi Mwake. Wanangu, kwa hiyo ni lazima msali kwa upendo, lazima msali sana, sana, ili kupata upendo zaidi na zaidi, kwa maana upendo hushinda mauti na hudumisha maisha. Watume wa upendo wangu, wanangu wenye moyo mnyofu na safi, jiungeni zaidi na zaidi katika kusali. Mnatengana sana! Jipeni moyo katika kukua kiroho, kama vile Mimi ninawapeni moyo. Ninawaangalia na nipo karibu nanyi kila mnaponifikiria. Waombeeni wachungaji wenu, wale walioacha yote kwa ajili ya Mwanangu. Wapendeni na waombeeni, Baba wa Mbinguni husikiliza sala zenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, mimi ni sikuzote pamoja nanyi, kwa maana Mwanangu alinikabidhi ninyi. Nanyi, wanangu, mnanihitaji mimi, mnitafute, mnijie na mfurahishe Moyo wangu wa kimama. Mimi ninawapenda na nitawapenda ninyi mnaoteseka na kutolea mateso yenu kwa ajili ya Mwanangu na kwa ajili yangu. Upendo wangu hutafuta upendo wa wanangu wote na wanangu wote hutafuta upendo wangu. Kwa njia ya upendo Yesu hutafuta ushirika kati ya Mbingu na dunia, kati ya Baba wa mbinguni na ninyi, wanangu, Kanisa lake. Kwa hiyo lazima kusali sana, kusali na kulipenda Kanisa ambalo ninyi ni wake. Sasa Kanisa linateseka na kuhitaji mitume ambao, wakipenda ushirika, wanaposhuhudia na kutoa, waonyeshe njia za Mungu. Kanisa linahitaji mitume ambao, wakiishi Ekaristi kwa moyo, watende matendo makuu. Kanisa linawahitaji ninyi, mitume wangu wa upendo. Wanangu, Kanisa limeteswa na kusalitiwa tangu siku zake za awali, lakini linazidi kukua siku hata siku. Kanisa halitaharibiki, kwa maana Mwanangu alilipa moyo: Ekaristi. Nuru ya ufufuo wake imeng’aa na itang’aa juu yake. Kwa hiyo msiogope! Waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na nguvu na upendo kwa kuwa madaraja ya wokovu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kama Mama nafurahi ya kuwa katikati yenu, kwa maana nataka kuongea nanyi tena kuhusu maneno ya Mwanangu na upendo wake. Natumaini mtanipokea kwa upendo, maana maneno ya Mwanangu na upendo wake ni nuru na tumaini la pekee katika giza la siku hizi. Huu ni ukweli wa pekee, nanyi mtakaoupokea na kuuishi, mtakuwa na mioyo safi na minyenyekevu. Mwanangu hupenda mioyo safi na minyenyekevu. Mioyo safi na minyenyekevu inahuisha maneno ya Mwanangu: inayaishi, inayaeneza na kufanya hata wote wayasikie. Maneno ya Mwanangu yanaamsha maisha ya wale wanaoyasikiliza, maneno ya Mwanangu hurudisha upendo na matumaini. Kwa hiyo, mitume wangu wapenzi, wanangu, isheni maneno ya Mwanangu. Pendaneni kama Yeye alivyowapenda. Pendaneni katika jina lake na kumbukumbu lake. Kanisa huendelea na kukua kwa ajili ya wale wanaosikiliza maneno ya Mwanangu, kwa sababu ya wanaohuzunika na kuteseka kimyakimya katika tumaini la kukombolewa milele. Kwa hiyo wanangu wapendwa, maneno ya Mwanangu na upendo wake yawe wazo la kwanza na la mwisho la siku yenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Leo nataka kushirikiana pamoja nanyi furaha ya mbinguni. Ninyi wanangu fungueni mlango wa moyo ili katika moyo wenu matumaini, amani na mapendo ambazo Mungu peke yake anaweza kutoa ziweze kukua. Wanangu, mnapenda mno dunia na mambo ya dunia, kwa hiyo Shetani huwatikisa kama upepo ufanyavyo na mawimbi ya bahari. Kwa hiyo mnyororo wa maisha yenu uwe sala ya moyo na kumwabudu Mwanangu Yesu. Kwake mtolee maisha yenu yajayo ili muwe ndani Yake furaha na mfano kwa watu wengine kwa njia ya matendo yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, wakati duniani upendo unapopunguka, wakati njia ya wokovu haipatikani, Mimi, Mama yenu, naja kuwasaidieni kujua imani ya kweli, iliyo hai na ya kina, na kuwasaidieni kupenda kabisa. Kama Mama ninatamani mpendane, muwe wema na safi. Ni hamu yangu muwe wenye haki na mpendane. Wanangu, muwe wafurahivu rohoni, muwe safi, muwe watoto. Mwanangu alisema kwamba anapenda kukaa kati ya wenye mioyo safi, maana wenye mioyo safi ni daima vijana na wafurahivu. Mwanangu aliwaambieni msameheane na mpendane. Najua kwamba si rahisi sikuzote. Mateso husababisha kukua rohoni. Ili kukua rohoni kadiri iwezekanavyo, lazima msamehe na kupenda kwa dhati na kwa kweli. Wana wangu wengi duniani hawamjui Mwanangu, hawampendi. Lakini ninyi mnaompenda Mwanangu na kumchukua moyoni salini, salini, na mkisali mumhisi Mwanangu karibu yenu. Nafsi yenu ipumue Roho yake! Mimi nipo kati yenu na kuongea juu ya mambo madogo na makubwa. Sitachoka kuwasimulieni habari ya Mwanangu, aliye upendo wa kweli. Kwa hiyo, wanangu, nifungulieni mioyo yenu, acheni niwaongoze kama mama. Muwe mitume wa upendo wa Mwanangu na wangu. Kama Mama nawasihi: msisahau wale walioitwa na Mwanangu wawaongoze. Wachukueni moyoni na muwaombee. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, maneno yangu ni manyofu lakini yamejaa upendo wa kimama na mahangaiko. Wanangu, juu yenu vivuli vya giza na vya udanganyifu vinaenea zaidi na zaidi, mimi ninawaiteni kuelekea mwanga na ukweli, mimi ninawaita kuelekea Mwanangu. Yeye peke yake huweza kugeuza kukata tamaa na maumivu yetu kuwa amani na utulivu, Yeye peke yake huweza kutoa matumaini katika maumivu makali sana. Mwanangu ni uzima wa ulimwengu, kwa kadiri mtakavyomjua, ndivyo mtakavyomkaribia na kumpenda maana Mwanangu ni upendo, na upendo unageuza yote. Yeye hufanya la ajabu hata neno lisilo la maana bila upendo machoni penu. Kwa hiyo nawaambieni tena ya kwamba mnapaswa kupenda sana ikiwa mnatamani kukua kiroho. Najua, enyi mitume wa upendo wangu, kwamba si rahisi sikuzote, lakini, wanangu, hata njia ngumu ni njia zinazoongoza kwenye ukuaji wa kiroho, wa kiimani na kwa Mwanangu. Wanangu, salini, mfikirie Mwanangu, nyakati zote za siku zenu inueni nafsi zenu kwake nami nitakusanya sala zenu kama maua kutoka bustani nzuri kuliko zote na kumpa Mwanangu. Muwe hakika mitume wa upendo wangu, wapeni wote upendo wa Mwanangu, muwe bustani zenye maua mazuri kuliko yote. Kwa njia ya sala saidieni wachungaji wenu ili waweze kuwa baba za kiroho waliojaa upendo kwa watu wote. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Upendo wa Mwanangu ni mkubwa. Laiti mngeweza kujua ukuu wa upendo Wake, msingeacha kamwe kumwabudu na kumshukuru. Yeye ni sikuzote hai pamoja nanyi katika Ekaristi, maana Ekaristi ni moyo Wake, Ekaristi ni moyo wa imani. Yeye hakuwaacha kamwe: hata wakati ninyi mlipojaribu kwenda mbali Naye, Yeye hakuwaacha kamwe.

Kwa hiyo, moyo wangu wa kimama unafurahi wakati unapotazama jinsi mlivyojaa upendo mnapomrudia, wakati unapoona ya kuwa mnamrudia kwa njia ya upatanisho, upendo na matumaini. Moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa ikiwa mngetembea katika njia ya imani, mngekuwa kama machipukizi, kama matumba na kwa njia ya sala na kufunga mngekuwa kama matunda, kama maua, mitume wa upendo wangu, mngekuwa waleta mwanga na mngeangaza kwa upendo na hekima pande zote karibu nanyi.

Wanangu, kama mama, ninawaomba: salini, fikirini na kutafakari. Yote yanayowatokea, mazuri, ya kuumiza na ya kufurahisha, hayo yote yawasababisha kukua kiroho, yawafanya kuwa Mwanangu akue ndani yenu. Wanangu mkabidhi kwake. Mumwamini na mtumainie upendo Wake. Na Yeye awaongoze. Na Ekaristi iwe mahali mtakapolisha roho zenu ili kueneza upendo na ukweli. Shuhudieni Mwanangu. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa! Rudieni kusali maana wanaosali hawaogopi wakati ujao. Wale wanaosali wako wazi kwa uzima na wanaheshimu maisha ya wengine. Yeyote anayesali, wanangu, anahisi uhuru wa wana wa Mungu na kwa moyo wa furaha hutumikia kwa manufaa ya ndugu yake. Kwa sababu Mungu ni upendo na uhuru. Kwa hiyo, wanangu, wanapotaka kuwafunga kwa minyororo na kuwatumia hilo halitoki kwa Mungu maana Mungu ni upendo na humpa kila kiumbe amani yake. Kwa hiyo amenituma niwasaidie ninyi kukua katika njia ya utakatifu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`