Our Lady of Medjugorje Messages containing 'kumjua'

Total found: 10
Wanangu wapendwa, fungueni mioyo yenu mkajaribu kuhisi jinsi ninavyowapenda na kutaka mpendeni Mwanangu. Nataka mpende zaidi kwa kuwa haiwezekani kumjua pasipo kumpenda, maana Yeye ndiye upendo. Wanangu, mimi nawajueni: najua maumivu yenu na mateso yenu maana niliyaishi. Nafurahi pamoja nanyi kwa furaha zenu. Nalia machozi pamoja nanyi katika maumivu yenu. Sitawaacheni kamwe. Nitaongea nanyi daima kwa upole wa kimama na, kama mama, nahitaji mioyo yenu ifumbuliwe, ili kwa hekima na unyofu mueneze upendo wa Mwanangu. Nawahitaji ninyi mfumbuliwe na kuwa wepesi kupokea mema na huruma. Nahitaji muungano wenu na Mwanangu, kwa maana nataka mpate kufanikiwa na kumsaidia kuleta heri kwa wanangu wote. Mitume wangu, nawahitaji, ili muwaonyeshe wote ukweli wa Mungu, ili moyo wangu, ulioteswa na kuteswa hata leo kupita kiasi, uweze kushinda katika upendo. Salini kwa ajili ya utakatifu wa wachungaji wenu, ili katika jina la Mwanangu, waweze kutenda maajabu, maana utakatifu hutenda maajabu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nimewaalika na ninawaalika tena kumjua Mwanangu, kuujua ukweli. Mimi nipo pamoja nanyi na ninasali ili mfanikiwe. Wanangu, yawapasa kusali sana ili kupata upendo na uvumilivu mwingi kadiri muwezavyo, ili kuweza kuvumilia sadaka na kuwa maskini rohoni. Mwanangu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, yu sikuzote pamoja nanyi. Kanisa lake huzaliwa katika kila moyo unaomjua. Salini ili muweze kumjua Mwanangu, salini ili roho yenu iwe kitu kimoja pamoja naye. Hiyo ndiyo sala na huo ndio upendo wa kuwavutia wengine na kuwafanyeni kuwa mitume wangu. Ninawatazama kwa upendo, kwa upendo wa kimama. Ninawajua, najua maumivu yenu na mateso yenu, kwa maana Mimi nami niliteswa kimya. Imani yangu ilinipa upendo na tumaini. Ninawaambieni tena: Ufufuo wa Mwanangu na Kupokewa kwangu mbinguni ni tumaini na upendo kwa ajili yenu. Kwa hiyo, wanangu, salini ili kujua ukweli, ili kupata imani thabiti, ya kuongoza mioyo yenu na kuweza kugeuza mateso yenu na maumivu yenu kuwa upendo na tumaini. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ujio wangu kwenu ni zawadi ya Baba wa Mbinguni kwa ajili yenu. Kwa njia ya upendo wake ninakuja kuwasaidieni kupata njia inayowangoza kwenye ukweli, na kupata njia inayowaongoza kwa Mwanangu. Ninakuja kuwathibitishia ukweli. Nataka kuwakumbushia maneno ya Mwanangu. Yeye aliyatamka maneno ya wokovu kwa ulimwengu wote, maneno ya upendo kwa watu wote, ule upendo aliouonyesha kwa kujitolea kwake sadaka. Lakini hata leo wanangu wengi hawamjui, hawataki kumjua, hawamjali. Kwa sababu ya kutokujali kwao, moyo wangu unateseka kwa uchungu. Mwanangu amekuwa daima katika Baba. Alipozaliwa duniani, ametuletea Umungu, wakati kutoka kwangu ameuchukua ubinadamu. Kwa njia yake Neno limefika katikati yetu. Kwa njia yake Mwanga, ambao hupenyeza mioyoni, huiangaza, huijaza upendo na faraja, umeingia ulimwenguni. Wanangu, wanaweza kumwona Mwanangu wale wote wanaompenda, kwa kuwa uso wake huonekana kwa njia ya mioyo inayojaa mapendo kumwelekea Yeye. Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, mnisikilize! Acheni uovu na ubinafsi. Msiishi tu kwa ajili ya vitu vya ulimwengu, vinavyoharibika. Mpendeni Mwanangu na muwawezeshe wengine kuutambua uso kwa njia ya mapendo mliyo nayo kwake. Mimi nitawasaidia kumjua zaidi. Mimi nitawaeleza kuhusu Yeye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Roho Mtakatifu, kwa njia ya Baba wa Mbinguni, amenifanya Mama: Mama wa Yesu na, kwa hiyo, Mama yenu vilivile. Kwa hiyo nawajilia niwasikilize, niwafungulie mikono yangu ya kimama, niwapeni Moyo wangu na kuwaalika kukaa pamoja nami, kwa maana kutoka juu ya msalaba Mwanangu amenikabidhi ninyi. Kwa bahati mbaya wanangu wengi hawakujua upendo wa Mwanangu, wengi hawataka kumjua. Loo, wanangu, mabaya mengi yatoka kwa wale ambao hawana budi ya kuona na kuelewa ili kuamini! Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, katika kimya ya moyo wenu sikilizeni sauti ya Mwanangu, ili moyo wenu uwe makazi yake wala usiwe giza na huzuni, bali uangaziwe na mwanga wa Mwanangu. Tafuteni matumaini kwa imani, maana imani ni maisha ya roho. Ninawaalika tena: salini! Salini ili kuishi imani katika unyenyekevu, katika amani ya kiroho na mkiangaziwa na mwanga. Wanangu, msijaribu kuelewa yote mara moja, maana Mimi nami sikuelewa yote mara moja, lakini niliyaamini maneno ya kimungu aliyoyasema Mwanangu, Yeye aliyekuwa mwanga wa kwanza na mwanzo wa Ukombozi. Enyi mitume wa moyo wangu, ninyi mnaosali, mnaojitolea, mnaopenda wala msiohukumu: ninyi nendeni mkaeneze ukweli, maneno ya Mwanangu, Injili. Ninyi kweli, ni Injili iliyo hai, ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu. Mwanangu na mimi tutakuwa karibu nanyi, tutawatia moyo na kuwajaribu. Wanangu, ombeeni daima na hasa baraka ya wale ambao Mwanangu amebariki mikono yao, yaani Wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kuja na kujifunua kwangu kwenu ni furaha kubwa ya Moyo wangu wa kimama. Ni zawadi ya Mwanangu kwa ajili yenu na ya wale watakaokuja. Kama Mama nawaalika: mpendeni Mwanangu kuliko yote! Ili kumpenda kwa moyo wote, yawapaswa kumjua: Mtamjua kwa kusali: Salini kwa moyo na hisia zenu. Kusali maana yake ni kutafakari upendo wake na kujitolea kwake. Kusali maana yake ni kupenda, kutoa, kuteseka na kutolea sadaka. Nawaalika ninyi, wanangu, kuwa mitume ya sala na upendo. Wanangu, ni wakati wa kukesha. Katika kesha hii nawaalika kusali, kupenda na kutumaini. Maadamu Mwanangu ataangalia mioyo yenu, Moyo wangu wa kimama unatamani kwamba Yeye aone ndani ya mioyo yenu tumaini timilifu na upendo. Upendo wa mitume wangu wote pamoja utaishi, utashinda na utafunua maovu. Wanangu, mimi nilikuwa kalisi ya Mtu - Mungu, nilikuwa chombo cha Mungu. Kwa hiyo nawaalika ninyi, mitume wangu, kuwa kalisi ya upendo mnyofu na safi wa Mwanangu. Nawalika kuwa chombo ambacho kwa njia yake wote wasiojua upendo wa Mungu, wasiopenda kamwe, wataelewa, wataupokea na wakaokolewa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kwa mapenzi ya Baba wa mbinguni, kama Mama wa Yule anayewapendeni, nipo hapa pamoja nanyi niwasaidieni kumjua, kumfuata. Mwanangu amewaachieni nyayo za hatua zake, ili iwe rahisi zaidi kwenu kumfuata. Msiogope, msiwe na wasiwasi. Mimi nipo pamoja nanyi! Msichoke, maana sala nyingi na sadaka zinahitajiwa kuwasaidia wale wasiomwomba, wasiompenda na wasiomjua Mwanangu. Muwasaidie mkiona ndani yao ndugu zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, sikilizeni sauti yangu ndani yenu, hisieni upendo wangu. Kwa hiyo salini: salini mkitenda, salini mkitoa. Salini kwa upendo, salini kwa matendo na kwa fikira, kwa jina la Mwanangu. Kadiri mtakavyotoa upendo, ndivyo mtakavyoupokea. Upendo utokao katika Upendo huangaza ulimwengu. Ukombozi ni upendo, na upendo hauna mwisho. Wakati Mwanangu atakapokuja tena duniani, atatafuta upendo katika mioyo yenu. Wanangu, Yeye alifanya kwa ajili yenu matendo mengi ya upendo. Ninawafundisha kuyaona, kuyaelewa na kumshukuru mkimpenda na kumsamehe sikuzote na tena jirani yako. Kwa kuwa kumpenda Mwanangu maana yake ni kusamehe. Mwanangu hapendwi, ikiwa hatuwezi kumsamehe jirani yetu, ikiwa hatuwezi kumwelewa jirani yetu, ikiwa tunamhukumu. Wanangu, faida gani kusali, msipopenda wala msiposamehe? Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kwa njia ya upendo mkubwa wa Baba wa Mbinguni, mimi ni pamoja nanyi kama Mama yenu nanyi ni pamoja nami kama wanangu, kama mitume wa upendo wangu ambao ninakusanya daima karibu nami. Wanangu, ninyi ni wale ambao, mkisali, yawapasa kujitolea kabisa kwa Mwanangu, ili kwamba si ninyi tena mnaoishi, bali ni Mwanangu ndani yenu; ili wale wote wasiomjua wamwone ndani yenu na watake kumjua. Salini ili waone ndani yenu unyenyekevu thabiti na wema, utayari kuwatumikia wengine; waone kwamba mnaishi kwa moyo wito wenu duniani, mkishirikiana na Mwanangu. Waone ndani yenu upole, rehema na upendo kuelekea Mwanangu, kama vile kuelekea ndugu na dada zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, hamna budi kusali sana na kutakasa mioyo yenu, ili ninyi muwe wale wa kwanza waendao katika njia ya Mwanangu; ili ninyi muwe wale wenye haki wanaoungana na haki ya Mwanangu. Wanangu, kama mitume wangu lazima muungane na ushirika utokao katika Mwanangu, ili wanangu wasiomjua Mwanangu watambue ushirika wa upendo na watake kutembea katika njia ya uzima, njia ya umoja na Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, moyo safi na wazi tu utawawezesha ninyi kumjua kweli Mwanangu, na wale wote wasiojua upendo wake kuujua kwa njia yenu. Upendo tu utawawezesha kuelewa kuwa ni wenye nguvu kuliko kifo, maana upendo wa kweli umeshinda kifo na umefanya hata kifo hakipo tena. Wanangu, msamaha ni mtindo bora wa upendo. Ninyi, kama mitume wa upendo wangu, yawapasa kusali kwa kuwa wenye nguvu katika roho na kuweza kuelewa na kusamehe. Ninyi, mitume wa upendo wangu, kwa njia ya ufahamu na msamaha, mnatoa mfano wa upendo na rehema. Kuweza kuelewa na kusamehe ni karama inayotokana na maombi na yatupasa kuitunza. Mkisamehe ninyi mnaonyesha ya kuwa mnajua kupenda. Tazameni, wanangu, kama Baba wa mbinguni anavyowapenda kwa upendo mkubwa, kwa ufahamu, kwa uelewa, msamaha na haki. Kama anavyowatolea mimi, Mama wa mioyo yenu. Na tazama: mimi nipo katikati yenu ili kuwabariki kwa baraka ya kimama; ili kuwaalika kusali na kufunga; ili kuwasihi kuamini, kutumaini, kusamehe, kuwaombea wachungaji wenu na hasa kupenda bila mipaka. Wanangu, nifuateni! Njia yangu ni njia ya amani na upendo, njia ya Mwanangu. Ndiyo njia ya kuongoza katika ushindi wa Moyo wangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, mapenzi na upendo wa Baba wa mbinguni hufanya mimi niwe katikati yenu, ili kusaidia kwa upendo wa kimama ukuaji wa imani katika mioyo yenu, ili kwamba muweze hakika kuelewa lengo la maisha ya kidunia na ukuu wa yale ya kimbingu. Wanangu, maisha ya kidunia ndiyo njia kuelekea umilele, kuelekea ukweli na uzima: kuelekea kwa Mwanangu. Kwa njia hii nataka kuwaongoza. Ninyi, wanangu, ninyi wenye sikuzote kiu ya upendo mkubwa zaidi, ukweli na imani, mjue ya kuwa moja tu ni chemchemi mnakoweza kunywa: imani katika Baba wa mbinguni, imani katika upendo wake. Mtegemee kabisa mapenzi yake wala msiogope: kila lililo bora kwa ajili yenu, kila linalowachukua kwenye uzima wa milele, mtapewa! Mtaelewa ya kuwa lengo la maisha si sikuzote kutaka na kutwaa, lakini kupenda na kutoa; mtakuwa na amani ya kweli na upendo wa kweli, mtakuwa mitume wa upendo. Kwa mfano wenu, mtawafanya wale wanangu wasiomjua Mwanangu na upendo wake watake kumjua. Wanangu, mitume wa upendo wangu, mwabuduni Mwanangu pamoja nami, na mpendeni juu ya vyote. Jaribuni sikuzote kuishi katika ukweli wake. Ninawashukuru.
Mwotaji Mirjana Dragićević-Soldo alikuwa na matukio ya kila siku kutoka Juni 24, 1981 hadi Desemba 25, 1982. Katika hafla ya kutokezwa kwake kwa kila siku, akimfunulia siri ya kumi, Bikira alimfunulia kwamba atakuwa na tukio la kila mwaka mnamo Machi 18 na ndivyo ilivyokuwa katika miaka hii yote. Tukio hilo lilianza saa 1.33 jioni na kudumu hadi saa 1.39.
Wanangu wapendwa, ninawaalika mpate kumjua Mwanangu vizuri iwezekanavyo kwa sala na rehema. Ili kwa mioyo safi na iliyo wazi mjifunze kusikiliza. Sikilizeni Mwanangu anachowaambieni ili mpate kuona tena kiroho. Kama watu wamoja wa Mungu, kwa ushirika na Mwanangu, ishuhudieni kweli kwa maisha yenu. Ombeni, wanangu, ili kwamba pamoja na Mwanangu muweze kuleta amani, furaha na upendo kwa ndugu zenu wote. Mimi ni pamoja nanyi na ninawabariki kwa baraka zangu za kimama.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`