Our Lady of Medjugorje Messages containing 'kuwasaidieni'

Total found: 8
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama na uvumilivu wa kimama naona kutangatanga kwenu na kuendelea kupotea kwenu. Kwa sababu hiyo mimi nipo pamoja nanyi. Nataka kwanza kabisa kuwasaidieni kupata kujijua ninyi wenyewe, ili baadaye muweze kuelewa na kutambua yote yanayowazuia kujua bila unafiki na kwa moyo wote upendo wa Baba wa Mbinguni. Wanangu, Baba hujulikana kwa njia ya msalaba: kwa hiyo msikatae msalaba: kwa msaada wangu, mkafanye bidii kuuelewa na kuupokea. Mtakapoweza kuupokea msalaba, mtaelewa pia upendo wa Baba wa Mbinguni. Mtatembea pamoja na Mwanangu na mimi. Mtajipambanua na wale ambao hawakujua upendo wa Baba wa Mbinguni, kujitofautisha na wale wanaomsikiliza lakini hawamwelewi, na wale wasioenda pamoja naye, na wasiomjua. Mimi nataka ninyi mjue ukweli wa Mwanangu na muwe mitume wangu; ili, kama wana wa Mungu, muwe na mawazo yaliyo juu ya mawazo ya kibinadamu na siku zote na katika yote mkatafute kila mara mawazo ya Mungu. Wanangu, salini na fungeni ili muweze kuelewa yote ninayowaombeni. Muombee wachungaji wenu mkatamani kujua, mkishirikiana nao, upendo wa Baba wa Mbinguni. Nawashukuruni.
Wanangu wapendwa! Mimi, Mama yenu, nipo pamoja nanyi kwa ajili yenu, kwa mahitaji yenu na mafundisho yenu binafsi. Baba wa Mbinguni amewapa uhuru wa kuamua peke yenu na kujua peke yenu. Mimi nataka kuwasaidieni. Nataka kuwa Mama kwenu, mwalimu wa ukweli, ili kwa unyofu wa moyo wazi mjue usafi usio na mwisho, na mwanga utokao kwa hiyo ukweli ili kutawanya giza, yaani mwanga uletao tumaini. Mimi, wanangu, naelewa maumivu yenu na mateso yenu. Nani aweza kuwaelewa zaidi kuliko Mama mmoja! Lakini enyi wanangu? Mjue kuwa idadi ya wanaonielewa na kunifuata ni ndogo. Pia ni kubwa idadi ya waliopotea, hao ambao hawajajua ukweli ulio katika Mwanangu. Kwa hiyo, enyi mitume wangu, salini na tendeni kazi. Mbebe mwanga, msipoteze tumaini. Mimi nipo nanyi na hasa pamoja na wachungaji wenu. Nawapenda na kuwalinda kwa Moyo wa kimama, ili kusudi wao wanawaongozeni Paradisini alikowaahidia Mwanangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! Sababu ya kukaa kwangu pamoja nanyi, utume wangu, ni kuwasaidieni ili wema ushinde, hata kama kwa sasa haya yaonekana ni kitu kigumu sana. Najua kwamba mambo mengi hamyaelewi, kama vile sikuelewa mengi ambayo Mwanangu alinifundisha akiwa alipokua pamoja nami, lakini mimi nilimsadiki na kumfuata. Haya nawaombea ninyi pia, kunisadiki na kunifuata, lakini, wanangu, kunifuata maana yake ni kupenda mwanangu kuliko wote, kumpenda katika kila mtu pasipo ubaguzi. Ili kuweza kufanya haya yote nawaalikeni tena kujinyima, kusali na kufunga. Nawaalikeni ili maisha ya roho yenu yawe ni Ekaristi. Nawaalikeni muwe mitume wangu wa mwanga, ambao wataueneza upendo na rehema ulimwenguni. Wanangu, maisha yenu ni mpigo tu wa moyo mbele ya uzima wa milele. Mtakapokuwa mbele ya Mwanangu, Yeye ataona katika mioyo yenu kiasi cha upendo mliokuwa nao. Ili kuweza kueneza kwa njia ya haki upendo nitamwomba Mwanangu kusudi kwa njia ya upendo awapeni umoja kati yenu na umoja kati yenu na wachungaji wenu. Mwanangu daima anajitoa upya kwa njia yao na anafanya mioyo yenu mipya. Msisahau hilo. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, wapendwa mitume wangu wa upendo, waletaji wangu wa ukweli, ninawaalika tena na ninawakusanya karibu nami ili mnisaidie, ili muwasaidie wanangu wote wenye kiu ya upendo na ukweli, wenye kiu ya Mwanangu. Mimi ndimi neema ya Baba wa Mbinguni iliyotumwa kuwasaidieni kuishi neno la Mwanangu. Pendaneni. Nimeyaishi maisha yenu duniani. Najua kwamba si kitu rahisi kila mara lakini, mkipendana, mtasali kwa moyo, mtafikia vilele vya maisha ya roho, na njia ya kwenda mbinguni itafunguliwa mbele yenu. Pale nawangojea mimi, Mama yenu, kwa maana mimi nipo pale. Muwe waaminifu kwa Mwanangu na muwafundishe wengine uaminifu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwasaidia. Nitawafundisha imani, ili muweze kuwafikishia wengine kwa njia sahihi. Nitawafundisha ukweli, ili muweze kuufahamu. Nitawafundisha upendo, ili mjue upendo wa kweli ni kitu gani. Wanangu, Mwanangu atafanya yote ili aongee kwa njia ya maneno na matendo yenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ujio wangu kwenu ni zawadi ya Baba wa Mbinguni kwa ajili yenu. Kwa njia ya upendo wake ninakuja kuwasaidieni kupata njia inayowangoza kwenye ukweli, na kupata njia inayowaongoza kwa Mwanangu. Ninakuja kuwathibitishia ukweli. Nataka kuwakumbushia maneno ya Mwanangu. Yeye aliyatamka maneno ya wokovu kwa ulimwengu wote, maneno ya upendo kwa watu wote, ule upendo aliouonyesha kwa kujitolea kwake sadaka. Lakini hata leo wanangu wengi hawamjui, hawataki kumjua, hawamjali. Kwa sababu ya kutokujali kwao, moyo wangu unateseka kwa uchungu. Mwanangu amekuwa daima katika Baba. Alipozaliwa duniani, ametuletea Umungu, wakati kutoka kwangu ameuchukua ubinadamu. Kwa njia yake Neno limefika katikati yetu. Kwa njia yake Mwanga, ambao hupenyeza mioyoni, huiangaza, huijaza upendo na faraja, umeingia ulimwenguni. Wanangu, wanaweza kumwona Mwanangu wale wote wanaompenda, kwa kuwa uso wake huonekana kwa njia ya mioyo inayojaa mapendo kumwelekea Yeye. Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, mnisikilize! Acheni uovu na ubinafsi. Msiishi tu kwa ajili ya vitu vya ulimwengu, vinavyoharibika. Mpendeni Mwanangu na muwawezeshe wengine kuutambua uso kwa njia ya mapendo mliyo nayo kwake. Mimi nitawasaidia kumjua zaidi. Mimi nitawaeleza kuhusu Yeye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama naja kuwasaidieni kuwa na upendo zaidi, maana yake imani zaidi. Naja kuwasaidieni kuishi kwa upendo maneno ya Mwanangu, ili ulimwengu uwe tofauti. Kwa sababu hiyo nawakusanya, mitume wa mapendo yangu, karibu nami. Niangalieni kwa upendo, ongeeni nami kama vile na Mama kuhusu mateso yenu, maumivu yenu, furaha zenu. Ombeni ili nisali Mwanangu kwa ajili yenu. Mwanangu ni mwenye rehema na haki. Moyo wangu wa kimama ungependa ninyi pia muwe hivyo. Moyo wangu wa kimama ungependa ya kuwa ninyi, mitume wa mapendo yangu, mngeongea kwa maisha yetu juu ya Mwanangu na juu yangu pamoja na watu wote walio karibu nanyi, ili ulimwengu uwe tofauti, ili wairudie imani na tumaini. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini kwa moyo. Salini kwa upendo, salini kwa matendo mema. Salini ili wote wamjue Mwanangu, ili ulimwengu ugeuke, ulimwengu uokoke. Ishini kwa upendo maneno ya Mwanangu. Msihukumu, lakini mpendaneni, ili Moyo wangu uweze kushinda. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nawaalika kusali pasipo kuomba, bali mkitoa sadaka, mkijitolea wenyewe. Nawaalika kuleta habari ya ukweli na upendo wenye rehema. Ninamwomba Mwanangu kwa ajili yenu, kwa imani yenu, inayoendelea kupunguka katika mioyo yenu. Ninamwomba awasaidieni kwa Roho ya Mungu, kama vile mimi nami ninavyotaka kuwasaidieni kwa roho ya kimama. Wanangu, itawabidi kujiboresha! Wale tu walio safi, wanyenyekevu na wamliojaa upendo wanautegemeza ulimwengu, wanaokoa ulimwengu na wao wenyewe. Wanangu, Mwanangu ndiye moyo wa ulimwengu: lazima kumpenda na kumwomba, na si kumsaliti daima tena. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, mstawishe imani katika mioyo ya watu kwa mfano wenu, kwa sala yenu na kwa upendo wenye rehema. Mimi nipo karibu nanyi na nitawasaidia. Salini ili wachungaji wenu wapate mwanga zaidi kadiri wawezavyo, ili waweze kuangaza wale wote wanaoishi gizani. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, wakati duniani upendo unapopunguka, wakati njia ya wokovu haipatikani, Mimi, Mama yenu, naja kuwasaidieni kujua imani ya kweli, iliyo hai na ya kina, na kuwasaidieni kupenda kabisa. Kama Mama ninatamani mpendane, muwe wema na safi. Ni hamu yangu muwe wenye haki na mpendane. Wanangu, muwe wafurahivu rohoni, muwe safi, muwe watoto. Mwanangu alisema kwamba anapenda kukaa kati ya wenye mioyo safi, maana wenye mioyo safi ni daima vijana na wafurahivu. Mwanangu aliwaambieni msameheane na mpendane. Najua kwamba si rahisi sikuzote. Mateso husababisha kukua rohoni. Ili kukua rohoni kadiri iwezekanavyo, lazima msamehe na kupenda kwa dhati na kwa kweli. Wana wangu wengi duniani hawamjui Mwanangu, hawampendi. Lakini ninyi mnaompenda Mwanangu na kumchukua moyoni salini, salini, na mkisali mumhisi Mwanangu karibu yenu. Nafsi yenu ipumue Roho yake! Mimi nipo kati yenu na kuongea juu ya mambo madogo na makubwa. Sitachoka kuwasimulieni habari ya Mwanangu, aliye upendo wa kweli. Kwa hiyo, wanangu, nifungulieni mioyo yenu, acheni niwaongoze kama mama. Muwe mitume wa upendo wa Mwanangu na wangu. Kama Mama nawasihi: msisahau wale walioitwa na Mwanangu wawaongoze. Wachukueni moyoni na muwaombee. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`