Our Lady of Medjugorje Messages containing 'mnaokutana'

Total found: 6
Wanangu wapendwa! Salini, salini, salini ili mionzi ya sala yenu iwaguse watu wote mnaokutana nao. Wekeni Biblia Takatifu mahali pa kuonekana katika familia zenu, mkaisome ili maneno ya amani yatiririke ndani ya mioyo yenu. Nasali pamoja nanyi na kwa ajili yenu, wanangu, ili siku hata siku mzidi kuyapokea mapenzi ya Mungu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu kama Mama atakaye kuwasaidia kuujua ukweli. Nilipokuwa nikiishi maisha kama yenu duniani, nilikuwa nikijua ukweli na kwa hivyo kuwa na kipande cha Mbinguni duniani. Kwa hiyo, wanangu, nataka ninyi pia muwe washiriki wa hali hivyo. Baba wa Mbinguni ataka mioyo minyofu, ijaayo ujuzi wa ukweli: Ataka muwapende wote mnaokutana nao, maana mimi pia nampenda Mwanangu katika ninyi nyote. Huo ndio mwanzo wa ujuzi wa ukweli. Mtapewa kweli nyingi za uongo. Mtazitambua kwa mioyo iliyotakaswa kwa kufunga, kusali, kwa kufanya toba pamoja na kuishika Injili: Huo ndiyo ukweli wa pekee, nao ni ule ambao Mwanangu aliwaachieni. Msiufanyie utafiti mwingi sana: mnaombwa kuupenda na kuutoa, kama vile nilivyofanya mimi pia. Wanangu, mkipenda, mioyo yenu itakuwa maskani ya Mwanangu na yangu, na maneno ya Mwanangu yatakuwa mwongozo wa maisha yenu. Wanangu, nitawatumia, ninyi mitume wa upendo, kusaidia wanangu wote kuujua ukweli. Wanangu, mimi nimeliombea sikuzote Kanisa la Mwanangu, kwa hiyo nawasihi ninyi pia kufanya vile vile. Salini ili wachungaji wenu waangazwe kwa upendo wa Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama ninawaalika kuifunua mioyo kwa imani, kuifunua mioyo kwa Mwanangu, ili katika mioyo yenu upendo kwa Mwanangu uimbe. Hakika, kutoka upendo huo tu, amani huingia nafsini. Wanangu, najua kwamba mna wema, najua kwamba mna upendo, upendo wenye rehema. Wanangu wangu wengi, lakini, wana moyo uliofungwa. Wanadhani kuweza kutenda pasipo kumwelekezea mawazo yao Baba wa mbinguni anayeangaza, pasipo kumwelekezea Mwanangu aliye daima pamoja nanyi katika Ekaristi na ataka kuwasikiliza. Wanangu, mbona hamzungumzi naye? Maisha ya kila mmoja wenu ni muhimu na ya thamani, maana ni zawadi ya Baba wa mbinguni kwa umilele. Kwa hiyo msisahau kamwe kumshukuru. Zungumzeni naye! Najua, enyi wanangu, ya kuwa mambo yatakayokuja hayajulikani kwenu lakini, mambo yenu ya mbele yatakapotokea, mtapata majibu yote. Upendo wangu wa kimama unataka muwe tayari. Wanangu, kwa maisha yenu wekeni katika mioyo ya watu mnaokutana hisia za amani, za mema, za upendo na msamaha. Kwa ajili ya sala, sikilizeni yanayowaambieni Mwanangu na tendeni namna hiyo. Ninawaalika tena kuwaombea wachungaji wenu, wale ambao Mwanangu aliwaita. Kumbukeni ya kuwa wanahitaji sala na upendo. Nawashukuru.
Wanangu, Wakati mnaponijia kama Mama kwa moyo safi na wazi, mjue ya kuwa ninawasikiliza, ninawatia moyo, ninawafariji na hasa ninawaombeeni kwa Mwanangu. Najua ya kuwa mnataka kuwa na imani thabiti na kuionyesha kwa njia inayofaa. Neno analotaka Mwanangu kutoka kwenu ni imani ya kweli, thabiti na kubwa. Hivyo kila njia mnavyoielezea ni ya kufaa. Imani ni fumbo la ajabu tunalohifadhi moyoni. Inakaa baina ya Baba wa Mbinguni na wana wake wote. Hutambulika kwa matunda na kwa upendo ambao sisi tunao kwa viumbe vyote vya Mungu. Enyi mitume wa upendo wangu, wanangu, mtumaini Mwanangu! Saidieni ili wanangu wote wajue upendo wake. Ninyi ni matumaini yangu, ninyi mnaojitahidi kupenda Mwanangu pasipo unafiki. Kwa jina la upendo, kwa wokovu wenu, kulingana na mapenzi ya Baba wa Mbinguni na kwa njia ya Mwanangu, nipo hapa katikati yenu. Mitume wa upendo wangu, kwa njia ya sala na sadaka mioyo yenu iangazwe na upendo na mwanga wa Mwanangu. Mwanga ule na upendo ule uangaze wote wale mnaokutana na uwarudishe kwa Mwanangu! Mimi nipo nanyi. Hasa nipo pamoja na wachungaji wenu: kwa upendo wangu wa kimama ninawaangaza na kuwatia moyo, ili, kwa njia ya mikono iliyobarikiwa na Mwanangu, wabariki ulimwengu mzima. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninawaita mitume wa upendo wangu. Ninawaonyesha Mwanangu, aliye amani ya kweli na upendo wa kweli. Kama Mama, kwa ajili ya neema ya kimungu, ninatamani kuwaongoza kwendea Yeye. Wanangu, kwa hiyo ninawaalika kujitazama ninyi wenyewe mkianzia kwa Mwanangu, kumtazama kwa moyo na kuona kwa moyo mahali mlipo na maisha yenu yanakwenda wapi. Wanangu, ninawaalika kuelewa ya kuwa mnaishi kwa ajili ya Mwanangu, kwa njia ya upendo wake na sadaka yake. Ninyi mnamwomba Mwanangu kuwa mwenye rehema nanyi, lakini mimi ninawaalika ninyi kuwa na rehema. Mnamwomba kuwa mwema nanyi na kuwasamehe, lakini tangu lini mimi ninawasihi ninyi, wanangu, kusamehe na kupenda watu wote mnaokutana nao! Mtakapoelewa kwa moyo maneno yangu, mtaelewa na kujua upendo wa kweli, na mtaweza kuwa mitume wa upendo ule, enyi mitume wangu, wanangu wapendwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama ninawaalika ili kwa moyo safi na wazi, kwa imani kabisa, mpokee upendo mkubwa wa Mwanangu. Mimi ninajua ukuu wa upendo wake, mimi nilimchukua ndani yangu, Hostia moyoni, Mwanga na Upendo wa ulimwengu. Wanangu, hata kuelekea kwangu kwenu ninyi ni ishara ya upendo na ya huruma ya Baba wa Mbinguni, ni tabasamu kilichojaa upendo wa Mwanangu, ni mwaliko kwa uzima wa milele. Damu ya Mwanangu ilimwagika kwa ajili yenu kwa upendo. Ile Damu yenye thamani ni kwa wokovu wenu, kwa ajili ya uzima wa milele. Baba wa mbinguni aliumba mtu kwa ajili ya furaha ya milele. Haiwezekani ninyi kufa, ninyi mnaojua upendo wa Mwanangu, ninyi mnaomfuata. Uzima umeshinda: Mwanangu yu hai! Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, sala iwaonyeshe njia, jinsi ya kueneza upendo wa Mwanangu kwa jinsi ilivyo bora zaidi. Wanangu, hata wakati mnapojaribu kuishi maneno ya Mwanangu, ninyi mnasali. Wakati mnapowapenda watu mnaokutana nao, mnaeneza upendo wa Mwanangu. Upendo ni neno linalofungua milango ya Uzima. Wanangu, tangu awali nimesali kwa ajili ya Kanisa. Kwa hiyo ninawaalika nanyi, mitume wa upendo wangu, kusali kwa ajili ya Kanisa na watumishi wake, kwa wale ambao Mwanangu amewaita. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`