Our Lady of Medjugorje Messages containing 'moja'

Total found: 6
Wanangu wapendwa, Roho Mtakatifu, kwa njia ya Baba wa Mbinguni, amenifanya Mama: Mama wa Yesu na, kwa hiyo, Mama yenu vilivile. Kwa hiyo nawajilia niwasikilize, niwafungulie mikono yangu ya kimama, niwapeni Moyo wangu na kuwaalika kukaa pamoja nami, kwa maana kutoka juu ya msalaba Mwanangu amenikabidhi ninyi. Kwa bahati mbaya wanangu wengi hawakujua upendo wa Mwanangu, wengi hawataka kumjua. Loo, wanangu, mabaya mengi yatoka kwa wale ambao hawana budi ya kuona na kuelewa ili kuamini! Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, katika kimya ya moyo wenu sikilizeni sauti ya Mwanangu, ili moyo wenu uwe makazi yake wala usiwe giza na huzuni, bali uangaziwe na mwanga wa Mwanangu. Tafuteni matumaini kwa imani, maana imani ni maisha ya roho. Ninawaalika tena: salini! Salini ili kuishi imani katika unyenyekevu, katika amani ya kiroho na mkiangaziwa na mwanga. Wanangu, msijaribu kuelewa yote mara moja, maana Mimi nami sikuelewa yote mara moja, lakini niliyaamini maneno ya kimungu aliyoyasema Mwanangu, Yeye aliyekuwa mwanga wa kwanza na mwanzo wa Ukombozi. Enyi mitume wa moyo wangu, ninyi mnaosali, mnaojitolea, mnaopenda wala msiohukumu: ninyi nendeni mkaeneze ukweli, maneno ya Mwanangu, Injili. Ninyi kweli, ni Injili iliyo hai, ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu. Mwanangu na mimi tutakuwa karibu nanyi, tutawatia moyo na kuwajaribu. Wanangu, ombeeni daima na hasa baraka ya wale ambao Mwanangu amebariki mikono yao, yaani Wachungaji wenu. Nawashukuru.
Katika tokeo la mwisho wa kila siku la tarehe 12 Septemba 1998 Mama Maria alimwambia Yakobo ya kuwa ataona tokeo lake mara moja kila mwaka, tarehe 25 Desemba, siku ya Kristmasi. Hivyo ikatokea na mwaka huu. Mama Maria ametokea pamoja na Mtoto Yesu mikononi mwake. Tokeo likaanza saa nane adhuhuri na dakika ishirini na kudumu dakika kumi. Yakobo, baadaye, akatoa ujumbe ufuatao:
Wanangu wapendwa, Leo katika siku hii ya neema nawaalika hasa kusali kwa ajili ya amani. Wanangu, nimekuja hapa kama Malkia wa Amani na mara nyingi nimewaalika kusali kwa ajili ya amani. Lakini wanangu, mioyo yenu imefadhaika. Dhambi inawazuia kufunguliwa kabisa kwa neema na amani ambayo Mungu ataka kuwapeni. Ili kuishi amani, wanangu, yawapasa kuwa kwanza na amani mioyoni mwenu na kujiachia kabisa kwa Mungu na mapenzi Yake. Msitafute amani na furaha katika mambo ya dunia hii maana haya yote hupita. Muelekee rehema ya kweli, amani itokayo kwa Mungu tu na hivyo mioyo wenu hivyo tu itajaa furaha ya kweli; hivyo tu mtaweza kuwa mashahidi wa amani katika dunia hii ya hofu. Mimi ni mama yenu na ninawaombea kila mmoja wenu mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, nani angeweza kusema nanyi vizuri zaidi kuliko Mimi kuhusu upendo na maumivu ya mwanangu? Niliishi pamoja naye, niliteseka pamoja naye. Nikiishi maisha ya kidunia, nilionja maumivu, maana nilikuwa mama. Mwanangu alipenda michakato na kazi ya Baba wa Mbinguni, Mungu wa kweli; na, kama alivyoniambia, alikuja kusudi awakomboe ninyi. Mimi nilificha maumivu yangu kwa njia ya upendo. Bali ninyi, wanangu, ninyi mnaweka maswali mengi, hamwelewi maumivu, hamwelewi kwamba, kwa njia ya upendo wa Mungu, mnapaswa kupokea maumivu na kuyachukua. Kila mwanadamu, iwe kwa kiwango kikubwa au kidogo, yampasa afanye mang'amuzi. Lakini, tukiwa na amani rohoni na tukiwa na hali ya neema, tumaini moja lipo: ni Mwanangu, Mungu aliyezaliwa na Mungu. Maneno yake ni mbegu ya uzima wa milele: Yanapopandwa katika roho njema, huleta matunda mengi. Mwanangu amechukua maumivu maana amepokea juu yake dhambi zenu. Kwa hiyo ninyi, wanangu, mitume wa upendo wangu, ninyi mnaoteswa: mjue kwamba maumivu yenu yatakuwa mwanga na utukufu. Wanangu, wakati mnapovumilia maumivu, wakati mnapoteswa, Mbingu huingia ndani yenu, nanyi mnawapa watu wote karibu nanyi Mbingu kidogo na matumaini mengi. Nawashukuru.
Katika tokeo la mwisho la kila siku tarehe 12 Septemba 1998 Bikira Maria alimwambia Yakobo Kolo ya kuwa ataona tokeo mara moja kila mwaka, tarehe 25 Decemba, siku ya Noeli. Hivyo kumekuwa na tokea hata mwaka huu. Tokeo limeanza saa 7 na dakika 38 na likadumu dakika 9. Bikira Maria amekuja pamoja na Mtoto Yesu mikononi mwake. Bikira Maria kwa njia ya Yakobo alipitisha ujumbe huu:
Wanangu wapendwa, katika siku hii ya neema ninawaalika kupenda. Wanangu, Mungu anawapenda kupita kiasi na kwa hiyo wanangu, mmejaa imani, bila kutazama nyuma na bila hofu mwachieni kabisa mioyo yenu ili Mungu aijaze kwa upendo wake. Msiwe na hofu kuamini upendo Wake na rehema Yake maana upendo Wake ni mwenye nguvu kuliko kila udhaifu wenu na hofu. Kwa hiyo, wanangu, mmejaa upendo katika mioyo yenu mwamini Yesu na mseme Ndiyo yenu maana Yeye ni njia ya pekee ya kuwaongoza kwa Baba wa milele.
Wanangu wapendwa, Salini kila siku Tasbihi, taji lile la maua linaloniungana moja kwa moja kama Mama kwa maumivu yenu, mateso, mahitaji na matumaini. Mitume wa upendo wangu, Mimi nipo pamoja nanyi kwa njia ya neema na upendo wa Mwanangu, nanyi ninawaombeni sala. Sala zenu zinahitajika sana ulimwenguni, ili roho ziongoke! Fungueni wazi kwa imani timilifu mioyo yenu kwa Mwanangu, na yeye ataandika ndani yao muhtasari wa Neno lake, yaani upendo. Ishini muungano usiotenganika na Moyo Mtakatifu sana wa Mwanangu! Wanangu, kama Mama nawaambieni ya kwamba hakuna wakati wa kupoteza ili kupiga magoti mbele ya Mwanangu, kumkiri kama Mungu wenu, aliye kitovu cha maisha yenu. Mtoeni karama, zile anazozipenda zaidi, yaani upendo kwa jirani yako, rehema na mioyo safi. Mitume wa upendo wangu, wanangu wengi bado hawajamkiri Mwanangu kama Mungu wao, bado hawajajua upendo wake. Lakini ninyi, kwa njia ya sala yenu inayosema kwa moyo safi na wazi, pamoja na karama mnazotoa kwa Mwanangu, mtasababisha kwamba hata mioyo migumu zaidi ifunguke. Mitume wa upendo wangu, nguvu ya sala inayosemwa kutokana na moyo, ya sala yenye nguvu na iliyojaa upendo, hugeuza ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini! Mimi nipo pamoja nanyi.. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, mapenzi na upendo wa Baba wa mbinguni hufanya mimi niwe katikati yenu, ili kusaidia kwa upendo wa kimama ukuaji wa imani katika mioyo yenu, ili kwamba muweze hakika kuelewa lengo la maisha ya kidunia na ukuu wa yale ya kimbingu. Wanangu, maisha ya kidunia ndiyo njia kuelekea umilele, kuelekea ukweli na uzima: kuelekea kwa Mwanangu. Kwa njia hii nataka kuwaongoza. Ninyi, wanangu, ninyi wenye sikuzote kiu ya upendo mkubwa zaidi, ukweli na imani, mjue ya kuwa moja tu ni chemchemi mnakoweza kunywa: imani katika Baba wa mbinguni, imani katika upendo wake. Mtegemee kabisa mapenzi yake wala msiogope: kila lililo bora kwa ajili yenu, kila linalowachukua kwenye uzima wa milele, mtapewa! Mtaelewa ya kuwa lengo la maisha si sikuzote kutaka na kutwaa, lakini kupenda na kutoa; mtakuwa na amani ya kweli na upendo wa kweli, mtakuwa mitume wa upendo. Kwa mfano wenu, mtawafanya wale wanangu wasiomjua Mwanangu na upendo wake watake kumjua. Wanangu, mitume wa upendo wangu, mwabuduni Mwanangu pamoja nami, na mpendeni juu ya vyote. Jaribuni sikuzote kuishi katika ukweli wake. Ninawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`