Our Lady of Medjugorje Messages containing 'muda'

Total found: 6
Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu. Ninawatazama, ninawapa tabasamu na kuwapenda kama mama peke yake awezavyo kufanya. Kwa neema ya Roho Mtakatifu ajaye kwa njia ya usafi wangu, ninaona mioyo yenu na kuitolea kwa Mwanangu. Tangu muda mrefu nawaombeni muwe mitume wangu, na kusali kwa ajili ya wale wasioujua upendo wa Mungu. Naomba sala inayotokana na upendo, sala itoayo matunda na sadaka. Msipotee muda kutaka kuelewa kama mnastahili kuwa mitume wangu, Baba aliye Mbinguni atahukumu wote, lakini ninyi mpendeni na msikilizeni. Najua ya kuwa mambo hayo yote yanawafadhaisha, hata ujio wangu katikati yenu, lakini upokeeni kwa furaha na salini ili muelewe kwamba mnastahili kufanya kazi kwa ajili ya ufalme wa mbingu. Upendo wangu ni juu yenu. Salini ili upendo wangu udumu ndani ya kila moyo, kwa maana upendo huo unaosamehe ujitolea bila kukata tamaa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nataka kufanya kazi kwa njia yenu, wanangu, mitume wangu, ili mwishowe niweze kukusanya wanangu wote pale ambapo pameandaliwa tayari kwa ajili ya furaha yenu. Nawaombea, kusudi kwa matendo yenu muweze kugeuza, kwani muda umefika kwa matendo ya kweli, kwa ajili ya Mwanangu. Upendo wangu utafanya kazi ndani mwenu, nitawatumia ninyi. Muwe na imani nami, kwani yote ninayotamani, ninayatamani kwa ajili yenu, wema wa milele, ulioumbwa kwa njia ya Baba wa Mbinguni. Ninyi, wanangu, mitume wangu, muishi maisha ya duniani pamoja na wanangu ambao hawafahamu upendo wa Mwanangu, wale ambao hawaniiti mama. Lakini msiogope kushuhudia ukweli, kwa maana ikiwa ninyi hamtaogopa na kushuhudia ukweli kwa uhodari, ukweli utashinda kimuujiza. Kumbukeni: nguvu iko katika upendo. Wanangu, upendo ndio kutubu, kusamehe, kusali, kujitoa sadaka na rehema, maana mkijua kupenda kwa matendo mtawabadilisha na wengine, mtawezesha mwanga wa Mwanangu uingie katika mioyo yao. Nawashukuru. Muwaombee wachungaji wenu, wao ni mali ya Mwanangu. Yeye aliwaita. Salini ili wawe siku zote na nguvu na uhodari wa kung'aa kwa nuru ya Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, mimi, kama Mama apendaye wanawe, natambua jinsi ulivyo mgumu muda huu mnaouishi. Naona mateso yenu, lakini jueni kwamba hamko peke yenu: Mwanangu yu pamoja nanyi! Yeye yupo popote, asiyeonekana, lakini mtaweza kumwona ikiwa mtamwishi. Yeye ndiye nuru inayoangaza roho yenu na kuleta amani. Yeye ndiye Kanisa, mnalopaswa kulipenda, kuliombea na kulilinda daima: si kwa maneno tu, bali kwa matendo ya upendo. Wanangu, fanyeni yote ili Mwanangu ajulikane kwa watu wote, na aweze kupendwa, kwa maana ukweli ni katika Mwanangu, aliyezaliwa na Mungu, Mwana wa Mungu. Msipoteze muda kwa kufikiri mno; mtajitenganisha na ukweli. Pokeeni Neno lake kwa moyo mnyofu na kuliishi. Mkiishi Neno lake, mtasali. Mkiishi Neno lake, mtapenda kwa upendo wenye huruma, na mtapendana. Kwa kadiri mtakavyokuwa na upendo hivyo ndivyo mtakavyokuwa mbali na kifo. Kwa wale watakaoishi na kulipenda Neno la Mwanangu, kifo kitakuwa uhai kwao. Nawashukuru! Salini kwa ajili ya kuweza kuona Mwanangu katika wachungaji wenu. Salini kwa ajili ya kuweza kumkumbatia katika wao.
Wanangu wapendwa, ninaongea nanyi kama Mama, kwa maneno rahisi, lakini yamejaa wingi wa upendo na wa bidii kwa wanangu, ambao kwa njia ya Mwanangu wamekabidhiwa kwangu. Mwanangu, ambaye anakuja kutoka umilele na hata sasa, anaongea nanyi kwa maneno ya uzima na anapanda upendo katika mioyo wazi. Kwa hiyo nawaomba, mitume wa upendo wangu: muwe na mioyo iliyo wazi sikuzote kurehemu na kusamehe. Wasameheni sikuzote wenzenu kama Mwanangu, kwa vile hivyo amani itakuwa ndani yenu. Wanangu, lindeni nafsi yenu, maana hiyo ndiyo ukweli wa pekee ulio wenu bila shaka. Mmeanza kusahau umuhimu wa familia. Familia haipaswi kuwa mahali pa mateso na maumivu, bali mahali pa uelewano na huruma. Familia wanaojaribu kuishi kama apendavyo Mwanangu, wanaishi wakipendana. Tangu alipokuwa angali mtoto, Mwanangu aliniambia ya kuwa watu wote kwake ni ndugu zake. Kwa hiyo kumbukeni, enyi mitume wa upendo wangu, watu wote mnaowaona ni kwenu familia yenu, ndugu kama apendavyo Mwanangu. Wanangu, msipoteze muda kufikiria na kuhangaikia mambo yajayo. Kitu chenu kimoja cha kuhangaikia kwenu kiwe vipi kuishi vema kila dakika kadiri ya Mwanangu, na tazama hiyo ndiyo ni amani! Wanangu, msisahau kabisa kuwaombea wachungaji wenu. Salini ili waweze kupokea watu wote kama wanao, ili, kama apendavyo Mwanangu, wawe kwao kama baba za kiroho. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Mimi ni pamoja nanyi kwa muda mrefu kwa maana Mungu ni mkuu katika upendo wake na katika uwepo wangu. Wanangu, ninawaalika kurudi kwa Mungu na kwa sala. Kipimo cha kuishi kwenu kiwe upendo na msisahau, wanangu, kwamba maombi na kufunga hufanya miujiza ndani yenu na kuwazunguka. Yote mnayoyafanya yawe kwa ajili ya utukufu wa Mungu na hapo Mbingu itajaza moyo wenu na furaha mkahisi ya kuwa Mungu anawapenda na kunituma ili kuokoa ninyi na Dunia ambayo juu yake mnaishi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu ninawaita kumrudia Mungu na sala. Waiteni watakatifu wote wawasaidie ili wawe mfano na msaada kwenu. Shetani ni mwenye nguvu na anapigania kuivutia kwake mioyo mingi zaidi awezavyo. Anataka vita na chuki. Kwa sababu hiyo Mimi ni pamoja nanyi muda mrefu ili niwaongoze kwenye njia ya wokovu, kwa Yule aliye njia, kweli na uzima. Wanangu, rudini kwa upendo kumwelekea Mungu naye atakuwa nguvu yenu na kimbilio lenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`