Our Lady of Medjugorje Messages containing 'muwaombee'

Total found: 6
Wanangu wapendwa, nawaalikeni tena kupenda na kutohukumu. Mwanangu, kwa mapenzi ya Baba aliye mbinguni, alikuwapo pamoja nanyi ili awaonyesheni njia ya wokovu, awaokoeni si awahukumuni. Na ikiwa mnataka kumfuata Mwanangu, msihukumu na mpende, kama vile Baba aliye mbinguni anavyowapenda ninyi. Hata wakati mnapoteseka sana, au mnapojikwaa chini ya msalaba, msikate tamaa, msihukumu, bali kumbukeni kwamba mnapendwa, na msifuni Baba aliye mbinguni kwa upendo wake. Wanangu, msiiache njia ninayowaongozeni. Msikimbie kwenye maangamizi. Kusali na kufunga itawapa nguvu zaidi ili mweze kuishi kama vile baba wa Mbinguni atakavyo; ili muwe mitume wangu wa imani na upendo; ili maisha yenu iwe na baraka ya wale mnaowaona; ili muwe kitu kimoja na baba aliye mbinguni na Mwanangu. Wanangu, huu ni ukweli wa pekee, ukweli uletao wongofu wenu na kisha wongofu wa wengine wote wasiojua maana ya neno kupenda. Wanangu, Mwanangu aliwapeni wachungaji: muwalinde, na muwaombee. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! nawapendeni kwa upendo wa kimama, na kwa subira ya kimama nangojea upendo wenu na ushirikiano wenu. Nasali ili muwe jumuiya ya wana wa Mungu na wanangu. Nasali ili muweze kuwa jumuiya inayojihuisha kwa furaha na imani na upendo wa Mwanangu. Wanangu, nawakusanya kama mitume wangu na nitawafundisha jinsi ya kuwajulisha wengine upendo wa Mwanangu, na jinsi ya kuwafikishia habari njema, ambaye ni Mwanangu. Nipeni mioyo yenu iliyo wazi na iliyosafishwa, nami nitaijaza upendo wa Mwanangu. Upendo wake utaipa maisha yenu maana nami nitatembea pamoja nanyi. Nitakuwa pamoja nanyi hata tumfikie Baba wa Mbinguni. Wanangu, wataokoka tu wale ambao watatembea kwa upendo na imani kumwelekea Baba wa Mbinguni. Msiogope, nipo pamoja nanyi! Muwaamini wachungaji wenu kama Mwanangu alivyowaamini wakati alipowachagua, na muwaombee ili waweze kupata nguvu na upendo wa kuwaongozeni. Nawashukuruni.
Wanangu wapendwa, kwa moyo wa kimama nawaalikeni tena kupenda, kusali bila kukata tamaa kwa zawadi ya upendo, kumpenda Baba wa Mbinguni zaidi ya yote. Mtakapompenda Yeye, mtajipenda wenyewe na jirani zenu. Mambo hayo hayawezi kutengana. Baba wa Mbinguni yumo katika kila mtu, hupenda kila mtu na kumwita kila mtu kwa jina lake. Kwa hiyo, wanangu, kwa njia ya kusali sikilizeni atakalo Baba wa Mbinguni. Ongeeni na Yeye. Muwe na uhusiano wa binafsi pamoja na Baba, atakayeufanya mkubwa zaidi uhusiano wake nanyi, jumuhiya ya wanangu, mitume wangu. Kama Mama napenda kwamba, kwa njia ya upendo kumwelekea Baba wa Mbinguni, inukeni juu ya ubatili wa malimwengu na muwasaidie wengine kujua na kumjongea polepole Baba wa Mbinguni. Wanangu, salini, salini, salini kwa zawadi ya upendo, kwa sababu upendo ndiye Mwanangu. Muwaombee wachungaji wenu, ili wawapende ninyi siku zote, kama vile Mwanangu alivyowapenda ninyi na kuonyesha akitoa maisha yake kwa wokovu wenu. Nawashukuruni.
Wanangu wapendwa, nataka kufanya kazi kwa njia yenu, wanangu, mitume wangu, ili mwishowe niweze kukusanya wanangu wote pale ambapo pameandaliwa tayari kwa ajili ya furaha yenu. Nawaombea, kusudi kwa matendo yenu muweze kugeuza, kwani muda umefika kwa matendo ya kweli, kwa ajili ya Mwanangu. Upendo wangu utafanya kazi ndani mwenu, nitawatumia ninyi. Muwe na imani nami, kwani yote ninayotamani, ninayatamani kwa ajili yenu, wema wa milele, ulioumbwa kwa njia ya Baba wa Mbinguni. Ninyi, wanangu, mitume wangu, muishi maisha ya duniani pamoja na wanangu ambao hawafahamu upendo wa Mwanangu, wale ambao hawaniiti mama. Lakini msiogope kushuhudia ukweli, kwa maana ikiwa ninyi hamtaogopa na kushuhudia ukweli kwa uhodari, ukweli utashinda kimuujiza. Kumbukeni: nguvu iko katika upendo. Wanangu, upendo ndio kutubu, kusamehe, kusali, kujitoa sadaka na rehema, maana mkijua kupenda kwa matendo mtawabadilisha na wengine, mtawezesha mwanga wa Mwanangu uingie katika mioyo yao. Nawashukuru. Muwaombee wachungaji wenu, wao ni mali ya Mwanangu. Yeye aliwaita. Salini ili wawe siku zote na nguvu na uhodari wa kung'aa kwa nuru ya Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, wakati duniani upendo unapopunguka, wakati njia ya wokovu haipatikani, Mimi, Mama yenu, naja kuwasaidieni kujua imani ya kweli, iliyo hai na ya kina, na kuwasaidieni kupenda kabisa. Kama Mama ninatamani mpendane, muwe wema na safi. Ni hamu yangu muwe wenye haki na mpendane. Wanangu, muwe wafurahivu rohoni, muwe safi, muwe watoto. Mwanangu alisema kwamba anapenda kukaa kati ya wenye mioyo safi, maana wenye mioyo safi ni daima vijana na wafurahivu. Mwanangu aliwaambieni msameheane na mpendane. Najua kwamba si rahisi sikuzote. Mateso husababisha kukua rohoni. Ili kukua rohoni kadiri iwezekanavyo, lazima msamehe na kupenda kwa dhati na kwa kweli. Wana wangu wengi duniani hawamjui Mwanangu, hawampendi. Lakini ninyi mnaompenda Mwanangu na kumchukua moyoni salini, salini, na mkisali mumhisi Mwanangu karibu yenu. Nafsi yenu ipumue Roho yake! Mimi nipo kati yenu na kuongea juu ya mambo madogo na makubwa. Sitachoka kuwasimulieni habari ya Mwanangu, aliye upendo wa kweli. Kwa hiyo, wanangu, nifungulieni mioyo yenu, acheni niwaongoze kama mama. Muwe mitume wa upendo wa Mwanangu na wangu. Kama Mama nawasihi: msisahau wale walioitwa na Mwanangu wawaongoze. Wachukueni moyoni na muwaombee. Nawashukuru.
Wanangu, Moyo wangu wa kimama unateseka wakati ninapotazama wanangu wasiopenda ukweli, wanaouficha; wakati ninapotazama wanangu wasiosali kwa moyo wala kwa matendo. Nimesikitika wakati ninapomwambia Mwanangu ya kuwa wana wangu wengi hawana imani tena, ya kuwa hawamjui Yeye, Mwanangu. Kwa hiyo ninawaalika, mitume wa upendo wangu: mjaribu kutazama mpaka ndani ya mioyo ya watu, na kule bila shaka mtapata hazina ndogo iliyofichwa. Kutazama hivyo ni rehema ya Baba wa mbinguni. Kutafuta mema hata palipo maovu makubwa zaidi, kutafuta kuwaelewana wala kutohukumiana: hilo ni neno ambalo Mwanangu anawaombeni. Nami, kama Mama, ninawaalika kumsikiliza. Wanangu, roho ni yenye nguvu kuliko mwili na, ikichukuliwa na upendo na matendo hushinda vikwazo vyote. Msisahau: Mwanangu aliwapendeni na anawapenda. Upendo wake ni pamoja nanyi na ndani yenu, wakati mpo kitu kimoja pamoja naye. Yeye ni mwanga wa ulimwengu, na hakuna mtu wala kitu kiwezacho kumsimamisha katika utukufu wa mwisho. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, msiwe na hofu ya kushuhudia ukweli! Ushuhudieni kwa hamu, kwa matendo, kwa upendo, kwa sadaka yenu, lakini hasa kwa unyenyekevu. Shuhudieni ukweli kwa wale ambao hawajajua Mwanangu. Mimi nitakuwa karibu nanyi, mimi nitawatia moyo. Shuhudieni upendo usioishi tena, maana huja kutoka Baba wa mbinguni ambaye ni wa milele na anawatolea wana wangu wote umilele. Roho wa Mwanangu itakuwa karibu nanyi. Ninawaalika tena, wanangu: muwaombee wachungaji wenu, ombeni ili upendo wa Mwanangu uweze kuwaongoza. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`