Our Lady of Medjugorje Messages containing 'mwingi'

Total found: 7
Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu kama Mama atakaye kuwasaidia kuujua ukweli. Nilipokuwa nikiishi maisha kama yenu duniani, nilikuwa nikijua ukweli na kwa hivyo kuwa na kipande cha Mbinguni duniani. Kwa hiyo, wanangu, nataka ninyi pia muwe washiriki wa hali hivyo. Baba wa Mbinguni ataka mioyo minyofu, ijaayo ujuzi wa ukweli: Ataka muwapende wote mnaokutana nao, maana mimi pia nampenda Mwanangu katika ninyi nyote. Huo ndio mwanzo wa ujuzi wa ukweli. Mtapewa kweli nyingi za uongo. Mtazitambua kwa mioyo iliyotakaswa kwa kufunga, kusali, kwa kufanya toba pamoja na kuishika Injili: Huo ndiyo ukweli wa pekee, nao ni ule ambao Mwanangu aliwaachieni. Msiufanyie utafiti mwingi sana: mnaombwa kuupenda na kuutoa, kama vile nilivyofanya mimi pia. Wanangu, mkipenda, mioyo yenu itakuwa maskani ya Mwanangu na yangu, na maneno ya Mwanangu yatakuwa mwongozo wa maisha yenu. Wanangu, nitawatumia, ninyi mitume wa upendo, kusaidia wanangu wote kuujua ukweli. Wanangu, mimi nimeliombea sikuzote Kanisa la Mwanangu, kwa hiyo nawasihi ninyi pia kufanya vile vile. Salini ili wachungaji wenu waangazwe kwa upendo wa Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, miaka hii yote ambapo Mungu ananijalia kuwepo pamoja nanyi ni ishara ya upendo mwingi sana wa Mungu kwa kila mmoja wenu na ishara ya jinsi alivyowapenda. Wanangu, Yeye Aliye Juu amewapeni neema nyingi na anataka kuwapa neema nyingi zaidi. Lakini, wanangu, mioyo yenu imefungwa, inaishi katika hofu na hayaruhusu upendo wa Yesu na amani yake yapate nafasi katika mioyo yenu na kutawala maisha yenu. Kuishi pasipo Mungu ni kuishi gizani wala kutoujua kamwe upendo wa Baba na ulinzi wake kwa kila mmoja wenu. Kwa hiyo wanangu, leo hasa mwombeni Yesu ili tangu leo maisha yenu yapate kuzaliwa upya katika Mungu, na maisha yenu iwe nuru itokayo kwenu. Namna hii mtakuwa mashahidi wa uwepo wa Mungu ulimwenguni hasa kwa kila mtu aishiye gizani. Wanangu, nawapenda na kuwaombeeni kila siku kwake Yeye Aliye Juu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, nimewaalika na ninawaalika tena kumjua Mwanangu, kuujua ukweli. Mimi nipo pamoja nanyi na ninasali ili mfanikiwe. Wanangu, yawapasa kusali sana ili kupata upendo na uvumilivu mwingi kadiri muwezavyo, ili kuweza kuvumilia sadaka na kuwa maskini rohoni. Mwanangu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, yu sikuzote pamoja nanyi. Kanisa lake huzaliwa katika kila moyo unaomjua. Salini ili muweze kumjua Mwanangu, salini ili roho yenu iwe kitu kimoja pamoja naye. Hiyo ndiyo sala na huo ndio upendo wa kuwavutia wengine na kuwafanyeni kuwa mitume wangu. Ninawatazama kwa upendo, kwa upendo wa kimama. Ninawajua, najua maumivu yenu na mateso yenu, kwa maana Mimi nami niliteswa kimya. Imani yangu ilinipa upendo na tumaini. Ninawaambieni tena: Ufufuo wa Mwanangu na Kupokewa kwangu mbinguni ni tumaini na upendo kwa ajili yenu. Kwa hiyo, wanangu, salini ili kujua ukweli, ili kupata imani thabiti, ya kuongoza mioyo yenu na kuweza kugeuza mateso yenu na maumivu yenu kuwa upendo na tumaini. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, msiwe na mioyo migumu, iliyofungwa na iliyojaa hofu. Pokeeni upendo wangu wa kimama uiangaze na kuijaza mioyo yenu upendo na matumaini, ili, kama Mama, niyalainishe maumivu yenu: ninayajua, na nimeyaonja. Maumivu huinua nayo ni sala kuu kuliko zote. Mwanangu huwapenda hasa wanaopokea maumivu. Alinituma Mimi niyalainishe na kuwaletea matumaini. Mumwamini Yeye. Najua kuwa ni vigumu kwenu, maana mnaona giza linalozidi kuongeza karibu yenu pande zote. Wanangu, giza mtalivunja kwa njia ya sala na upendo. Yule anayesali na kupenda haogopi, ana matumaini na upendo wenye huruma: Anaona mwanga, na anamwona Mwanangu. Kama mitume wangu nawaalika mjaribu kuwa mfano wa upendo wenye huruma na wenye matumaini. Salini sikuzote tena kwa ajili ya kupata upendo mwingi kadiri muwezavyo, maana upendo huleta mwanga unaovunja kila giza, na humleta Mwanangu. Msiogope, ninyi si peke yenu: Mimi nipo pamoja nanyi! Ninawasihi waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na upendo kila wakati na wawe na matendo ya upendo kwa Mwanangu, kwa njia yake na kwa kumkumbuka Yeye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nimekuja kwenu, katikati yenu, ili mnipe mahangaiko yenu, niweze kuyaleta mbele ya Mwanangu na kuwaombeeni kwake kwa manufaa yenu. Najua kuwa kila mmoja wenu ana mahangaiko yake, majaribu yake. Kwa hiyo kwa moyo wa kimama nawaalikeni: Njooni kwenye Meza ya Mwanangu! Yeye humega mkate kwa ajili yenu, huwapa Yeye mwenyewe. Huwapa matumaini. Anawaomba kuwa na imani zaidi, matumaini zaidi, utulivu zaidi. Anawaomba mpigane ndani yenu dhidi ya ubinafsi, hukumu na udhaifu wa kibinadamu. Kwa hiyo Mimi, kama Mama, nawaambieni: salini, maana sala huwapa nguvu ya kupigana ndani yenu. Mwanangu, alipokuwa mtoto, aliniambia mara nyingi ya kuwa wengi watanipenda na kuniita "Mama". Mimi hapa, katikati yenu, nasikia upendo na kuwashukuru! Kwa njia ya upendo huu namwomba Mwanangu ili hakuna hata mmoja wenu, wanangu, arudiye nyumbani jinsi alivyokuja. Ili mlete matumaini, rehema na upendo kadiri muwezavyo; ili muwe mitume wa upendo wangu, wanaoshuhudia kwa maisha yao kwamba Baba aliye Mbinguni ni chemchemi ya uzima si ya mauti. Wanangu wapendwa, nawaomba tena kwa moyo wa kimama: waombeeni wateule wa Mwanangu, kwa ajili ya mikono yao iliyobarikiwa, kwa ajili ya wachungaji wenu, ili waweze kumhubiri Mwanangu kwa upendo mwingi wawezavyo, na hivyo kusababisha wongofu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kama vile katika mahali pengine nilipokuja, vivyo hivyo hapa pia nawaalika kusali. Salini kwa ajili ya wale wasiomjua Mwanangu, kwa ajili ya wale ambao hawajaujua upendo wa Mungu, dhidi ya dhambi, kwa ajili ya waliowekwa wakfu, kwa ajili ya wale ambao Mwanangu aliwaita ili wawe na upendo na roho yenye nguvu, kwa ajili yenu na kwa ajili ya Kanisa. Mwombeni Mwanangu, na upendo mnaohisi kwa ajili ya ukaribu, utawapa nguvu na utawatayarisha kwa matendo mema mtakayofanya kwa Jina lake. Wanangu muwe tayari. Wakati huu ni njia panda ya maisha. Kwa hiyo nawaalika tena kwa imani na matumaini, ninawaonyesha njia ya kushika. Hayo ni maneno ya Injili: Mitume wangu, ulimwengu unahitaji sana mikono yenu iliyoinuliwa mbinguni, kuelekea kwa Mwanangu na kwa Baba wa mbinguni. Ni lazima kuwa na unyenyekevu mwingi na usafi wa moyo. Mumwamini Mwanangu na jueni ya kuwa mnaweza kuwa bora zaidi daima. Moyo wangu wa kimama unatamani kwamba ninyi, mitume wa upendo wangu, muwe sikuzote mianga midogo ya ulimwengu. Mtie nuru pale giza inapotaka kutawala na kwa sala yenu na upendo wenu, muonyeshe sikuzote njia ya kweli, ziokoeni nafsi. Mimi nipo pamoja nanyi. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninyi ambao Mwanangu anawapenda, ninyi ambao mimi ninawapenda, msiruhusu ubinafsi, kujipenda wenyewe, zitawale duniani. Msiache upendo na wema zifichwe. Ninyi mnaopendwa, mliojua upendo wa Mwanangu, kumbukeni ya kuwa kupendwa maana yake ni kupenda. Wanangu, muwe na imani! Mnapokuwa na imani mnafurahi na mkaeneza amani, nafsi yenu inaruka kwa shangwe: katika nafsi ile yumo Mwanangu. Mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya imani, mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya upendo, mnapowafanyia watu wengine mema, Mwanangu hutabasamu katika nafsi yenu. Mitume wa upendo wangu, mimi, kama Mama, ninawaelekea, ninawakusanya kunizunguka na ninataka kuwaongozeni katika njia ya upendo na imani, katika njia ya kufika kwenye Nuru ya ulimwengu. Nipo hapa kwa upendo na kwa imani, kwa maana, kwa baraka yangu ya kimama, nataka kuwapeni matumaini na nguvu katika mwendo wenu, kwa sababu njia ya kuongoza kwa Mwanangu si rahisi: imejaa matendo ya kujinyima, ya kujitolea, ya kujidhabihu, ya kusamehe na ya upendo, upendo mwingi. Njia ile, lakini, hupata amani na furaha. Wanangu, msisadiki sauti za uongo zinazosemesha kwa maneno yasiyo na ukweli, mwanga usio wa ukweli. Ninyi wanangu rudini kwa Maandiko! Ninawaangalieni kwa upendo kupita kiasi na, kwa neema ya Mungu, ninajidhihirisha kwenu. Wanangu, njoni pamoja nami, nafsi yenu iruke kwa shangwe! Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`