Our Lady of Medjugorje Messages containing 'nami'

Total found: 28
Wanangu wapendwa, inasikitisha kwamba katikati yenu, wanangu, yapo mashindano mengi, chuki, masilahi yenu wenyewe na ubinafsi. Wanangu, hivi kwa urahisi mnamsahau Mwanangu, maneno Yake na upendo Wake. Imani inazimika katika roho nyingi na mioyo imetekwa na vitu vya ulimwenguni. Lakini moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa katikati yenu kuna wale wanaoamini na kupenda, wale ambao wanajaribu kumkaribia Mwanangu zaidi na zaidi, ambao wanamtafuta bila kuchoka na namna hii, wananitafuta hata mimi. Hawa ndio wanyenyekevu na wapole ambao, pamoja na maumivu na mateso wanayoyachukua katika kimya, pamoja na tumaini lao na hasa pamoja na imani yao, ni mitume wa upendo wangu. Wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawafundisha ya kuwa Mwanangu hatafuti sala tu pasipo kuchoka bali hata matendo na hisia. Salini ili katika sala mpate kuzidi katika imani na katika upendo. Mpendane wenyewe kwa wenyewe: hilo ndilo analotaka Yeye, hiyo ndiyo ni njia ya uzima wa milele. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu ameleta mwanga kwa ulimwengu huu. Ameuleta kwa wale ambao walitaka kuuona na kuupokea. Hawa muwe ninyi, maana huu ndio mwanga wa ukweli, wa amani na wa upendo. Mimi ninawaongoza kama mama kumwabudu Mwanangu, kumpenda pamoja nami. Fikira zenu, maneno na matendo yenu yamwelekee Mwanangu, yawe katika jina Lake: hapo tu moyo wangu utajazwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, upendo na wema wa Baba wa mbinguni yanatoa mafunuo ili kwamba imani ikue, iweze kuelezwa, ilete amani, salama na matumaini. Hivi mimi nami, wanangu, kwa ajili ya upendo wenye rehema wa Baba wa mbinguni ninawaonyesha sikuzote tena njia ya kwenda kwa Mwanangu, kwa wokovu wa milele; kwa bahati mbaya, lakini, wanangu wengi hawataki kunisikiliza. Wanangu wengi wanasita. Lakini mimi, mimi, katika wakati na zaidi ya wakati, sikuzote nimemtukuza Bwana kwa mambo yale yote aliyoyatenda ndani yangu na kwa njia yangu. Mwanangu anajitolea kwenu, anamega mkate pamoja nanyi, anawaambieni maneno ya uzima wa milele ili muweze kuwaletea watu wote. Nanyi, wanangu, mitume wa upendo wangu, mnaogopa nini, ikiwa Mwanangu ni pamoja nanyi? Mwonyesheni nafsi zenu, ili Yeye aweze kuwa ndani yao na aweze kuwafanyeni kuwa vyombo vya imani, vyombo vya upendo. Wanangu, ishini Injili, ishini upendo wenye rehema kuelekea mwenzenu; lakini hasa ishini upendo kuelekea Baba wa mbinguni. Wanangu, hamkuungana kwa bahati tu. Baba wa mbinguni haunganishi watu kwa bahati tu. Mwanangu anaongea na nafsi zenu, nami ninaongea moyoni mwenu. Kama Mama ninawaambia: tembeeni nami! Pendaneni, na kutoa shuhuda! Hampasi kuogopa kulinda Ukweli, ambao ni Neno la Mungu, lililo la milele na lisilogeuka kamwe, kwa mifano yenu. Wanangu, yule anayetenda kazi katika mwanga wa upendo wenye rehema na ukweli, anasaidiwa sikuzote na Mbingu na hayuko peke yake. Mitume wa upendo wangu, waweze kuwatambua sikuzote katikati ya wengine wote katika maficho, upendo na utulivu wenu. Mimi nipo pamoja nanyi. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, mapenzi na upendo wa Baba wa mbinguni hufanya mimi niwe katikati yenu, ili kusaidia kwa upendo wa kimama ukuaji wa imani katika mioyo yenu, ili kwamba muweze hakika kuelewa lengo la maisha ya kidunia na ukuu wa yale ya kimbingu. Wanangu, maisha ya kidunia ndiyo njia kuelekea umilele, kuelekea ukweli na uzima: kuelekea kwa Mwanangu. Kwa njia hii nataka kuwaongoza. Ninyi, wanangu, ninyi wenye sikuzote kiu ya upendo mkubwa zaidi, ukweli na imani, mjue ya kuwa moja tu ni chemchemi mnakoweza kunywa: imani katika Baba wa mbinguni, imani katika upendo wake. Mtegemee kabisa mapenzi yake wala msiogope: kila lililo bora kwa ajili yenu, kila linalowachukua kwenye uzima wa milele, mtapewa! Mtaelewa ya kuwa lengo la maisha si sikuzote kutaka na kutwaa, lakini kupenda na kutoa; mtakuwa na amani ya kweli na upendo wa kweli, mtakuwa mitume wa upendo. Kwa mfano wenu, mtawafanya wale wanangu wasiomjua Mwanangu na upendo wake watake kumjua. Wanangu, mitume wa upendo wangu, mwabuduni Mwanangu pamoja nami, na mpendeni juu ya vyote. Jaribuni sikuzote kuishi katika ukweli wake. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, najua kuwepo katika maisha yenu na mioyo yenu. Nahisi upendo wenu, nasikia sala zenu na kuzipeleka kwa Mwanangu. Lakini, wanangu, mimi nataka kwa njia ya upendo wa kimama, kuwepo katika maisha ya wanangu wote. Nataka kukusanya karibu yangu wanangu wangu wote, chini ya joho langu la kimama. Kwa hiyo ninawaalika ninyi na kuwaiteni mitume wa upendo wangu, il mnisaidie. Wanangu, Mwanangu aliyatamka maneno haya: "Baba yetu”, Baba yetu uliye popote na katika mioyo yetu, kwa sababu ataka kuwafundisha kusali kwa maneno na kwa hisia zenu. Ataka muwe bora zaidi kila siku, muishi upendo wenye rehema ulio sala na sadaka isiyo na mipaka kwa ajili ya wengine. Wanangu mpeni Mwanangu upendo kwa jirani; mpeni jirani wenu maneno ya faraja, ya huruma na matendo ya haki. Yote mliyoyatoa kwa wengine, enyi mitume wa upendo wangu, Mwanangu anayapokea kama zawadi. Nami ni pamoja nanyi kwa sababu Mwanangu ataka kwamba upendo wangu, ulio kama mwali wa nuru, uzihuishe nafsi zenu, uwasaidie katika kutafuta amani na uheri wa milele. Kwa hiyo, wanangu, pendaneni, na muunganishwe kwa njia ya Mwanangu, ili muwe wana wa Mungu ambao wote pamoja kwa moyo uliojaa, wazi na safi mkisema kwa pamoja “Baba yetu” pasipo kuogopa! Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, Salini pamoja Nami kwa maisha mapya ya ninyi nyote. Wanangu, katika mioyo yenu mnajua ni nini lazima kibadilike: rudini kwa Mungu na kwa Amri Zake ili Roho Mtakatifu aweze kugeuza maisha yenu na uso wa dunia hii, inayohitaji kufanywa upya katika Roho. Wanangu, muwe sala kwa wale wote wasiosali, muwe furaha kwa wale wote wasioona njia ya kutokea, muwe waletaji mwanga katika giza za wakati huu wa wasiwasi. Salini na ombeni msaada na ulinzi wa watakatifu ili ninyi pia muweze kutamani mbingu na mambo halisi ya kimbingu. Mimi nipo pamoja nanyi nikiwalinda na kuwabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Huu ni wakati wa upendo, wa uchangamfu, wa sala na wa furaha. Salini, wanangu, ili Mtoto Yesu azaliwe katika mioyo yenu. Fungueni mioyo yenu kwa Yesu anayejitoa kwa kila mmoja wenu. Mungu amenialika ili mimi niwe furaha na matumaini katika wakati huu nami ninawaambia: bila Mtoto Yesu hamna wala huruma wala hisia ya Mbingu, zinazofichika katika yule Mtoto mchanga. Kwa hiyo, wanangu, fanyeni kazi juu ya nafsi zenu wenyewe. Mkisoma Maandiko Matakatifu, mtagundua kuzaliwa kwa Yesu na furaha kama ile ya siku za kwanza ya matokeo ya Medjugorje iliyotolea kwa ubinadamu. Historia itakuwa ukweli, ambao hata leo unajirudia ndani yenu na kuwazunguka. Fanyeni kazi na jengeni amani kwa njia ya sakramenti ya Kitubio. Jipatanisheni na Mungu, wanangu, na mtaona miujiza inawazunguka. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ombeni, shuhudieni na mfurahi pamoja nami kwa sababu Mwenyezi Aliye Juu ananituma tena kuwaongoza katika njia ya utakatifu. Mjitambue, wanangu, kwamba maisha yenu ni mafupi na umilele unawasubiri ili kwamba pamoja na watakatifu wote mmtukuze Mungu kwa nafsi yenu. Msiwe na wasiwasi, wanangu, kwa mambo ya kidunia lakini tamanini Mbingu. Mbingu itakuwa lengo lenu na furaha itatawala moyoni mwenu. Niko pamoja nanyi na ninawabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ombeni pamoja nami kwa ajili ya amani maana shetani anataka vita na chuki katika mioyo na mataifa. Kwa hiyo salini na, katika siku zenu, toeni sadaka kwa kufunga na kutubu ili Mungu awape amani. Wakati ujao uko kwenye njia panda kwa sababu mwanadamu wa kisasa hataki Mungu. Kwa hiyo ubinadamu unaelekea kwenye upotevu. Ninyi, wanangu, ni tumaini langu. Ombeni pamoja nami kwamba niliyoyaanza Fatima na hapa yatimie. Ombeni na mshuhudie amani katika mazingira yenu na muwe watu wa amani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`