Our Lady of Medjugorje Messages containing 'ndio'

Total found: 12
Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu kama Mama atakaye kuwasaidia kuujua ukweli. Nilipokuwa nikiishi maisha kama yenu duniani, nilikuwa nikijua ukweli na kwa hivyo kuwa na kipande cha Mbinguni duniani. Kwa hiyo, wanangu, nataka ninyi pia muwe washiriki wa hali hivyo. Baba wa Mbinguni ataka mioyo minyofu, ijaayo ujuzi wa ukweli: Ataka muwapende wote mnaokutana nao, maana mimi pia nampenda Mwanangu katika ninyi nyote. Huo ndio mwanzo wa ujuzi wa ukweli. Mtapewa kweli nyingi za uongo. Mtazitambua kwa mioyo iliyotakaswa kwa kufunga, kusali, kwa kufanya toba pamoja na kuishika Injili: Huo ndiyo ukweli wa pekee, nao ni ule ambao Mwanangu aliwaachieni. Msiufanyie utafiti mwingi sana: mnaombwa kuupenda na kuutoa, kama vile nilivyofanya mimi pia. Wanangu, mkipenda, mioyo yenu itakuwa maskani ya Mwanangu na yangu, na maneno ya Mwanangu yatakuwa mwongozo wa maisha yenu. Wanangu, nitawatumia, ninyi mitume wa upendo, kusaidia wanangu wote kuujua ukweli. Wanangu, mimi nimeliombea sikuzote Kanisa la Mwanangu, kwa hiyo nawasihi ninyi pia kufanya vile vile. Salini ili wachungaji wenu waangazwe kwa upendo wa Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninyi ni nguvu yangu. Ninyi, mitume wangu, ambao, kwa upendo wenu, unyenyekevu na sala ya kimya kimya, mnamwezesha Mwanangu ajulikane. Ninyi mnaishi ndani yangu. Ninyi mnanibeba mioyoni mwenu. Ninyi mnajua ya kuwa mna Mama awapendaye na aliyekuja kuwaletea upendo. Nawatazama katika Baba wa Mbinguni, natazama fikira zenu, maumivu yenu, mateso yenu na kuyaleta kwa Mwanangu. Msiogope! Msipoteze matumaini, maana Mwanangu humsikiliza Mama yake. Yeye hupenda tangu alipozaliwa, na ndio furaha yangu ya kuwa wanangu wote wajue upendo huo; na wote wale ambao, kwa sababu ya maumivu yao na kutoelewa kwao, walimwacha waweze kurudi kwake, na wote wao wasiomjua wamjue. Kwa sababu hiyo ninyi hapa ni mitume wangu, nami pia pamoja nanyi kama Mama yenu. Salini ili kuwa imara katika imani, maana upendo na rehema hutoka katika imani imara. Kwa njia ya upendo na rehema mtawasaidia wale wote wasiofahamu ya kuwa wanachagua giza badala ya nuru. Salini kwa ajili ya wachungaji wenu, maana wao ni nguvu ya Kanisa ambayo Mwanangu aliwaachieni. Kwa njia ya Mwanangu wao ni wachungaji wa roho. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nataka kufanya kazi kwa njia yenu, wanangu, mitume wangu, ili mwishowe niweze kukusanya wanangu wote pale ambapo pameandaliwa tayari kwa ajili ya furaha yenu. Nawaombea, kusudi kwa matendo yenu muweze kugeuza, kwani muda umefika kwa matendo ya kweli, kwa ajili ya Mwanangu. Upendo wangu utafanya kazi ndani mwenu, nitawatumia ninyi. Muwe na imani nami, kwani yote ninayotamani, ninayatamani kwa ajili yenu, wema wa milele, ulioumbwa kwa njia ya Baba wa Mbinguni. Ninyi, wanangu, mitume wangu, muishi maisha ya duniani pamoja na wanangu ambao hawafahamu upendo wa Mwanangu, wale ambao hawaniiti mama. Lakini msiogope kushuhudia ukweli, kwa maana ikiwa ninyi hamtaogopa na kushuhudia ukweli kwa uhodari, ukweli utashinda kimuujiza. Kumbukeni: nguvu iko katika upendo. Wanangu, upendo ndio kutubu, kusamehe, kusali, kujitoa sadaka na rehema, maana mkijua kupenda kwa matendo mtawabadilisha na wengine, mtawezesha mwanga wa Mwanangu uingie katika mioyo yao. Nawashukuru. Muwaombee wachungaji wenu, wao ni mali ya Mwanangu. Yeye aliwaita. Salini ili wawe siku zote na nguvu na uhodari wa kung'aa kwa nuru ya Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nawaalika kueneza imani katika Mwanangu, imani yenu. Ninyi wanangu, mlioangazwa na Roho Mtakatifu, mitume wangu, itangazeni imani kwa watu wengine, yaani kwa wasiosadiki, wasioijua na wasiotaka kuijua. Kwa sababu hiyo yawapasa kusali sana kwa ajili ya zawadi ya upendo, maana upendo ndio alama maalum ya imani ya kweli, na ninyi mtakuwa mitume wa upendo wangu. Upendo hufanya upya daima maumivu na furaha ya Ekaristi, hufanya upya maumivu ya Mateso ya Mwanangu, aliyewaonyesha upendo usio na kifani; hufanya upya furaha ya tendo la kuwaachia Mwili wake na Damu yake kwa ajili ya kuwalisha na hivyo kuwa kitu kimoja nanyi. Nikiwaangalia kwa wema nahisi upendo pasipo kiasi, ulioniimarisha katika hamu yangu ya kuwaongoza katika imani thabiti. Imani thabiti itawapa furaha na uchangamfu duniani, na mwishowe kuwaunganisha na Mwanangu. Hiyo ndiyo hamu yake. Kwa hiyo mwishi katika Yeye, na katika upendo, isheni katika nuru iliyowaangaza daima katika Ekaristi. Nawaombeni kusali sana kwa wachungaji wenu, kusali ili kupata upendo mkubwa kwa ajili yao, kwa maana Mwanangu aliwapeni ili waweze kuwalisha kwa Mwili wake na kuwafundisha upendo. Kwa hiyo wapendeni ninyi pia! Lakini, wanangu, kumbukeni: upendo maana yake ni kuvumilia na kutoa na kutohukumu kamwe. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nimewaalika na ninawaalika tena kumjua Mwanangu, kuujua ukweli. Mimi nipo pamoja nanyi na ninasali ili mfanikiwe. Wanangu, yawapasa kusali sana ili kupata upendo na uvumilivu mwingi kadiri muwezavyo, ili kuweza kuvumilia sadaka na kuwa maskini rohoni. Mwanangu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, yu sikuzote pamoja nanyi. Kanisa lake huzaliwa katika kila moyo unaomjua. Salini ili muweze kumjua Mwanangu, salini ili roho yenu iwe kitu kimoja pamoja naye. Hiyo ndiyo sala na huo ndio upendo wa kuwavutia wengine na kuwafanyeni kuwa mitume wangu. Ninawatazama kwa upendo, kwa upendo wa kimama. Ninawajua, najua maumivu yenu na mateso yenu, kwa maana Mimi nami niliteswa kimya. Imani yangu ilinipa upendo na tumaini. Ninawaambieni tena: Ufufuo wa Mwanangu na Kupokewa kwangu mbinguni ni tumaini na upendo kwa ajili yenu. Kwa hiyo, wanangu, salini ili kujua ukweli, ili kupata imani thabiti, ya kuongoza mioyo yenu na kuweza kugeuza mateso yenu na maumivu yenu kuwa upendo na tumaini. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, mitume wa upendo wangu, inawapasa ninyi kuujulisha upendo wa Mwanangu kwa wale wote ambao hawakumjua. Inawapasa ninyi, mianga midogo ya ulimwengu, ambao mimi ninaifunza kwa upendo wa kimama ili ing'ae waziwazi kwa mwangaza kamili. Sala itawasaidia, maana sala huwaokoa ninyi, sala huuokoa ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini kwa maneno, kwa moyo, kwa upendo wenye huruma na kwa sadaka. Mwanangu aliwaonyesha njia: Yeye aliyejimwilisha na kunifanya kuwa kalisi ya kwanza; Yeye ambaye kwa sadaka yake isiyo na kifani aliwaonyesha kama inavyopaswa kupenda. Kwa hiyo, wanangu, msiogope kusema kweli. Msiogope kujigeuza wenyewe na ulimwengu ili kueneza mapendo, mkitenda kila jinsi kusudi Mwanangu aweze kujulikana na kupendwa kwa kuwapenda wengine kwa ajili yake. Mimi, kama mama, nipo daima pamoja nanyi. Namwomba Mwanangu awasaidie ili katika maisha yenu upendo utawale: upendo uishio, upendo uvutao, upendo utoao uzima. Huo ndio upendo ninaowafundisha, upendo safi. Inawapasa ninyi, mitume wangu, kuutambua, kuuishi, kuueneza. Waombeeni wachungaji wenu kwa moyo, ili waweze kumshuhudia Mwanangu kwa upendo. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Huu ndio wakati wa neema. Wanangu, salini zaidi, semeni kidogo mkamwache Mungu awaongoze katika njia ya kutubu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwapenda kwa upendo wa kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Wakati huu ndio wakati wa neema na sala, wakati wa kungojea na wa majitoleo. Mungu anajitolea kwenu ili mumpende juu ya kila jambo. Kwa hiyo, wanangu, fumbueni mioyo yenu na jamaa zenu ili kungojea huko kugeuke kuwa sala na upendo na hasa majitoleo. Mimi nipo pamoja nanyi, wanangu, na ninawasihi msiache mema maana matunda yaonekana, yasikika, na yafika mbali. Kwa hiyo adui amekasirika na anafanya kila njia kuwaondoa ninyi katika sala. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, inasikitisha kwamba katikati yenu, wanangu, yapo mashindano mengi, chuki, masilahi yenu wenyewe na ubinafsi. Wanangu, hivi kwa urahisi mnamsahau Mwanangu, maneno Yake na upendo Wake. Imani inazimika katika roho nyingi na mioyo imetekwa na vitu vya ulimwenguni. Lakini moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa katikati yenu kuna wale wanaoamini na kupenda, wale ambao wanajaribu kumkaribia Mwanangu zaidi na zaidi, ambao wanamtafuta bila kuchoka na namna hii, wananitafuta hata mimi. Hawa ndio wanyenyekevu na wapole ambao, pamoja na maumivu na mateso wanayoyachukua katika kimya, pamoja na tumaini lao na hasa pamoja na imani yao, ni mitume wa upendo wangu. Wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawafundisha ya kuwa Mwanangu hatafuti sala tu pasipo kuchoka bali hata matendo na hisia. Salini ili katika sala mpate kuzidi katika imani na katika upendo. Mpendane wenyewe kwa wenyewe: hilo ndilo analotaka Yeye, hiyo ndiyo ni njia ya uzima wa milele. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu ameleta mwanga kwa ulimwengu huu. Ameuleta kwa wale ambao walitaka kuuona na kuupokea. Hawa muwe ninyi, maana huu ndio mwanga wa ukweli, wa amani na wa upendo. Mimi ninawaongoza kama mama kumwabudu Mwanangu, kumpenda pamoja nami. Fikira zenu, maneno na matendo yenu yamwelekee Mwanangu, yawe katika jina Lake: hapo tu moyo wangu utajazwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Wakati huu ndio wakati wa neema. Kama vile maumbile huhuisha kwa maisha mapya nanyi pia mnaalikwa kugeuka. Kateni shauri kwa ajili ya Mungu. Wanangu, ninyi ni watupu wala hamna furaha maana hamko na Mungu. Kwa hiyo salini ili sala iwe maisha kwenu. Maporini mtafuteni Mungu aliyewaumbeni maana mapori ya asili yanaongea na kupigana kwa ajili ya maisha wala si kwa ajili ya kifo. Vita vinatawala katika mioyo yenu na katika watu maana hamna amani na wala hamuoni, wanangu, ndugu yenu ndani ya jirani yako. Kwa hiyo mrudieni Mungu na kusali. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Wakati huu ndio wakati wa neema, wakati wa rehema kwa kila mmoja wenu. Wanangu, msiruhusu upepo wa chukio na hofu utawale ndani yenu na karibu nanyi. Ninyi, wanangu, mmealikwa kuwa upendo na sala. Ibilisi ataka hofu na fujo lakini ninyi, wanangu, muwe furaha ya Yesu Mfufuka ambaye amekufa na kufufuka kwa ajili ya kila mmoja wenu. Yeye ameshinda kifo kwa kuwapeni uzima, uzima wa milele. Kwa hiyo, wanangu, mshuhudieni na muwe wenye fahari kwa kufufuliwa katika Yeye. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Wakati huu ndio wakati wa neema. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaalika tena, wanangu, mrudieni Mungu na kwa kusali ili sala iwe furaha kwenu. Enyi wanangu hamtakuwa na wakati ujao wala amani mpaka katika maisha yenu mtakapoanza kuishi maongezi ya binafsi na badiliko katika mema. Maovu yatakoma na amani itatawala katika mioyo yenu na katika ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawaombea kwa mwanangu Yesu kwa ajili ya kila mmoja wenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`