Our Lady of Medjugorje Messages containing 'ninawaalika'

Total found: 50
Wanangu wapendwa! Hata leo ninawaalika: ishini katika sala mwito wenu. Leo, kama bado haijatokea awali, Shetani atamani kumfunga pumzi binadamu na roho yake kwa njia ya upepo wake unaoambukiza chukio na hofu. Katika mioyo mingi hakuna furaha kwa sababu hakuna Mungu wala sala. Uadui na vita zinaongezeka siku hata siku. Ninawaalika, wanangu, anzisheni upya kwa ari mwelekeo wa kutafuta utakatifu na upendo kwa maana nimekuja katikati yenu kwa ajili hiyo. Tuwe upendo na msamaha kwa wale wote wanaofahamu na kutaka kupenda kwa mapendo ya kibinadamu tu wala siyo kwa ule upendo mkubwa sana wa kimungu ambao Mungu anatualikia. Wanangu, matumaini ya kesho iliyo bora zaidi yawe daima mioyoni mwenu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema ninawaalika nyote: salini zaidi na muongee kidogo. Katika kusali tafuteni mapenzi ya Mungu na yaishini kadiri ya amri ambazo Mungu anawaalika kuziishi. Mimi nipo pamoja nanyi na kusali pamoja nanyi. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, hata leo kwa furaha nipo pamoja nanyi na ninawaalika wote, wanangu, salini, salini, salini, ili muweze kuelewa upendo nilio nao kwenu. Upendo wangu una nguvu kuliko uovu, kwa hiyo wanangu mjongeeni Mungu ili muweze kuonja furaha yangu kwa Mungu. Pasipo Mungu, wanangu, hamtakuwa na wakati ujao, wala tumaini, wala wokovu, kwa hiyo acheni uovu na chagueni wema: Mimi nipo pamoja nanyi na pamoja nanyi namwomba Mungu kwa mahitaji yenu yote. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, hata leo ninawaalika: muwe sala. Sala iwe mabawa kwa ajili ya mkutano kati yenu na Mungu. Ulimwengu upo katika wakati wa kujaribiwa, kwa maana umemsahau na kumwacha Mungu. Kwa hiyo wanangu, muwe wale wanaomtafuta na kupenda Mungu kuliko yote. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaongoza kwa Mwanangu, lakini ninyi hamna budi kunena "NDIYO" yenu katika uhuru wa wana wa Mungu. Nawaombeeni na kuwapenda, wanangu, kwa upendo usio na mwisho. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, wapendwa mitume wangu wa upendo, waletaji wangu wa ukweli, ninawaalika tena na ninawakusanya karibu nami ili mnisaidie, ili muwasaidie wanangu wote wenye kiu ya upendo na ukweli, wenye kiu ya Mwanangu. Mimi ndimi neema ya Baba wa Mbinguni iliyotumwa kuwasaidieni kuishi neno la Mwanangu. Pendaneni. Nimeyaishi maisha yenu duniani. Najua kwamba si kitu rahisi kila mara lakini, mkipendana, mtasali kwa moyo, mtafikia vilele vya maisha ya roho, na njia ya kwenda mbinguni itafunguliwa mbele yenu. Pale nawangojea mimi, Mama yenu, kwa maana mimi nipo pale. Muwe waaminifu kwa Mwanangu na muwafundishe wengine uaminifu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwasaidia. Nitawafundisha imani, ili muweze kuwafikishia wengine kwa njia sahihi. Nitawafundisha ukweli, ili muweze kuufahamu. Nitawafundisha upendo, ili mjue upendo wa kweli ni kitu gani. Wanangu, Mwanangu atafanya yote ili aongee kwa njia ya maneno na matendo yenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, leo ninawaalika nyote: salini kwa ajili ya nia zangu. Amani ipo hatarini kwa hiyo wanangu, salini na muwe waletaji wa amani na matumani katika ulimwengu huu wa wasiwasi ambamo shetani anashambulia na kuleta majaribu ya kila aina. Wanangu muwe thabiti katika sala na imara katika imani. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi nyote mbele ya Mwanangu, Yesu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Leo pia nawaletea Mwanangu Yesu katika mikono yangu, na kwa mikono hiyo nawapeni amani Yake na hamu ya Mbinguni. Ninasali pamoja nanyi kwa ajili ya amani na ninawaalika muwe amani. Nawabariki wote kwa baraka yangu ya kimama na ya amani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, nimewaalika na ninawaalika tena kumjua Mwanangu, kuujua ukweli. Mimi nipo pamoja nanyi na ninasali ili mfanikiwe. Wanangu, yawapasa kusali sana ili kupata upendo na uvumilivu mwingi kadiri muwezavyo, ili kuweza kuvumilia sadaka na kuwa maskini rohoni. Mwanangu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, yu sikuzote pamoja nanyi. Kanisa lake huzaliwa katika kila moyo unaomjua. Salini ili muweze kumjua Mwanangu, salini ili roho yenu iwe kitu kimoja pamoja naye. Hiyo ndiyo sala na huo ndio upendo wa kuwavutia wengine na kuwafanyeni kuwa mitume wangu. Ninawatazama kwa upendo, kwa upendo wa kimama. Ninawajua, najua maumivu yenu na mateso yenu, kwa maana Mimi nami niliteswa kimya. Imani yangu ilinipa upendo na tumaini. Ninawaambieni tena: Ufufuo wa Mwanangu na Kupokewa kwangu mbinguni ni tumaini na upendo kwa ajili yenu. Kwa hiyo, wanangu, salini ili kujua ukweli, ili kupata imani thabiti, ya kuongoza mioyo yenu na kuweza kugeuza mateso yenu na maumivu yenu kuwa upendo na tumaini. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Roho Mtakatifu, kwa njia ya Baba wa Mbinguni, amenifanya Mama: Mama wa Yesu na, kwa hiyo, Mama yenu vilivile. Kwa hiyo nawajilia niwasikilize, niwafungulie mikono yangu ya kimama, niwapeni Moyo wangu na kuwaalika kukaa pamoja nami, kwa maana kutoka juu ya msalaba Mwanangu amenikabidhi ninyi. Kwa bahati mbaya wanangu wengi hawakujua upendo wa Mwanangu, wengi hawataka kumjua. Loo, wanangu, mabaya mengi yatoka kwa wale ambao hawana budi ya kuona na kuelewa ili kuamini! Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, katika kimya ya moyo wenu sikilizeni sauti ya Mwanangu, ili moyo wenu uwe makazi yake wala usiwe giza na huzuni, bali uangaziwe na mwanga wa Mwanangu. Tafuteni matumaini kwa imani, maana imani ni maisha ya roho. Ninawaalika tena: salini! Salini ili kuishi imani katika unyenyekevu, katika amani ya kiroho na mkiangaziwa na mwanga. Wanangu, msijaribu kuelewa yote mara moja, maana Mimi nami sikuelewa yote mara moja, lakini niliyaamini maneno ya kimungu aliyoyasema Mwanangu, Yeye aliyekuwa mwanga wa kwanza na mwanzo wa Ukombozi. Enyi mitume wa moyo wangu, ninyi mnaosali, mnaojitolea, mnaopenda wala msiohukumu: ninyi nendeni mkaeneze ukweli, maneno ya Mwanangu, Injili. Ninyi kweli, ni Injili iliyo hai, ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu. Mwanangu na mimi tutakuwa karibu nanyi, tutawatia moyo na kuwajaribu. Wanangu, ombeeni daima na hasa baraka ya wale ambao Mwanangu amebariki mikono yao, yaani Wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! leo ninawaalika kuwa watu wa sala. Salini mpaka hata sala itakapokuwa kwenu furaha na mkutano na Yeye aliye juu. Yeye atageuza moyo wenu nanyi mtakuwa watu wa upendo na wa amani. Wanangu, msisahau kwamba shetani ni mwenye nguvu na anataka kuwaachisha kusali. Ninyi, msisahau kwamba sala ni kifunguo cha siri cha mkutano pamoja na Mungu. Kwa hiyo Mimi nipo pamoja nanyi, niwaongoze. Msiache kusali. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! leo ninawaalika kuwa makarimu katika kujinyima, katika kufunga na katika sala kwa ajili ya wale wote wanaojaribiwa, nao ni ndugu zenu kina kaka na kina dada. Na hasa ninawaomba kusali kwa ajili ya makuhani na kwa wote waliojiweka wakfu ili kwa ari zaidi wampende Yesu, ili Roho Mtakatifu aijaze mioyo yao kwa furaha, ili watoe ushuhuda wa Mbingu na mafumbo ya kimbingu. Roho nyingi ipo katika dhambi kwa sababu hakuna wale wanaojitoa sadaka na kusali kwa wongofu wao. Mimi nipo pamoja nanyi nikiwaombeeni ili mioyo yenu ijazwe furaha. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Katika kipindi hiki cha neema ninawaalika kuwa sala. Wote mna matatizo, taabu, maumivu na wasiwasi. Watakatifu wawe kwenu mfano na onyo kwa utakatifu, Mungu atakuwa karibu nanyi na mtakuwa wapya kwa utafiti na wongofu wa binafsi. Imani itakuwa kwenu tumaini, na furaha itazaliwa katika mioyo yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Katika kipindi hiki cha neema ninawaalika kusali. Salini na tafuteni amani, wanangu. Yeye aliyekuja hapa duniani awatoe amani, pasipo kuwabagua kuwa ninyi ni nani na ni kitu gani - Yeye, Mwanangu, ndugu yenu, kwa njia yangu anawaalika kuongoka maana pasipo Mungu hamna baadaye wala uzima wa milele. Kwa hiyo aminini, salini na isheni katika neema na mkingojea mkutano wenu wa binafsi pamoja naye. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Leo ninawaletea Mwanangu Yesu, ili awajalieni amani Yake na baraka Yake. Wanangu wapendwa, ninawaalika ninyi nyote kuishi na kushuhudia neema na zawadi mlizozipokea. Msiogope!Salini ili Roho Mtakatifu awapeni nguvu ya kuwa mashahidi wenye furaha na watu wa amani na matumaini. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Katika kipindi hiki cha neema ninawaalika nyote kujifungua na kuishi amri ambazo Mungu aliwapeni ili, kwa njia ya sakramenti, ziwaongoze katika njia ya wongofu. Ulimwengu na vishawishi vya ulimwengu vinawajaribu; ninyi, wanangu, angalieni viumbe vya Mungu ambavyo katika uzuri na unyenyekevu Yeye aliwapa, na mpendeni Mungu, enyi wanangu, kuliko kila kitu naye atawaongoza katika njia ya wokovu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ninawaalika kukaa pamoja nami katika kusali, wakati huu wa neema, ambapo giza linapigana na mwagaza. Wanangu, salini, muungame dhambi zenu mkaanzishe maisha mapya katika neema. Kateni shauri kwa Mungu naye atawaongoza kuelekea utakatifu na msalaba utakuwa kwenu ishara ya ushindi na matumaini. Mjivunie kubatizwa na mshukuruni moyoni mwenu kushika mpango wa Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, leo pia ninawaalika kuishi pamoja na Yesu maisha yenu mapya. Bwana Mfufuka awape nguvu ili muwe daima mashujaa katika majaribu ya maisha, na waaminifu na mdumu katika kusali, maana Yesu aliwaokoeni kwa majeraha Yake na kwa njia ya Ufufuko Wake aliwapa maisha mapya. Salini, wanangu na msipoteze matumaini. Katika mioyo yenu na ziwe furaha na amani, muwe mashahidi ya furaha ya kuwa wangu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwapenda nyote kwa upendo wangu wa kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, katika wakati huo wa wasiwasi ninawaalika kumwamini zaidi Mungu aliye Baba yenu mbinguni na anayenituma kuwaongozeni kwake. Ninyi, mfungulieni mioyo yenu kwa zawadi ambazo Yeye ataka kuwapeni na katika kimya ya moyo wenu mwabuduni Mwanangu, aliyetolea maisha Yake ili muishi katika milele anakotaka kuwaongoza. Matumaini yenu na yawe furaha ya kukutana na Yule Aliye juu katika maisha ya kila siku. Kwa hiyo ninawaalika: msiache sala maana sala hutenda miujiza. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ninawaalika kupokea kwa unyofu wa moyo maneno yangu, ninayowaambieni kama Mama ili muende katika njia ya mwanga kamili, wa usafi, wa upendo wa pekee wa Mwanangu, mtu na Mungu. Raha, mwanga usioelezeka kwa maneno ya kibinadamu utaingia nafsini mwenu, na mtashikwa na amani na upendo wa Mwanangu. Ninataka hayo kwa wanangu wote. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnaojua kupenda na kusamehe, ninyi msiohukumu, ninyi ambao mimi ninahimiza, muwe mfano kwa wale wote wasiokwenda katika njia ya mwanga na upendo au waliotengana nayo. Kwa njia ya maisha yenu waonyesheni ukweli, waonyesheni upendo, maana upendo hushinda matatizo yote, na wanangu wote wana kiu ya upendo. Ushirika wenu wa upendo ni zawadi kwa Mwanangu na kwangu. Lakini, wanangu, kumbukeni ya kuwa kupenda maana yake ni kupenda mwenzako na kutakia wongofu wa nafsi yake. Ninapowatazama mmekusanyika karibu nami, moyo wangu unahuzunika kwa sababu ninaona upendo haba wa kidugu, upendo wenye huruma. Wanangu, Ekaristi, Mwanangu hai katikati yenu, na maneno yake yatawasaidia kuelewa. Neno lake, kweli, ni uhai, Neno lake huburudisha nafsi, Neno lake huwajulisha upendo. Wanangu wapenzi, ninawaombeni tena, kama Mama apendaye wana wake: wapendeni wachungaji wenu, waombeeni… Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! Mungu aliniita ili niwaongozeni kwake, maana Yeye ndiye nguvu yenu. Kwa hiyo ninawaalika kumwomba na kumtegemea, maana Yeye ndiye kimbizo lenu kutoka kila uovu uliokaribu na kupeleka mioyo mbali kutoka neema na furaha mnakoitwa. Wanangu isheni Mbingu hapa duniani ili mkae vizuri na amri za Mungu ziwe mwanga katika njia yenu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwapenda nyote kwa upendo wa kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose
1 2 3 Next>>

For God to live in your hearts, you must love.

`