Our Lady of Medjugorje Messages containing 'ukombozi'

Total found: 3
Wanangu wapendwa, Roho Mtakatifu, kwa njia ya Baba wa Mbinguni, amenifanya Mama: Mama wa Yesu na, kwa hiyo, Mama yenu vilivile. Kwa hiyo nawajilia niwasikilize, niwafungulie mikono yangu ya kimama, niwapeni Moyo wangu na kuwaalika kukaa pamoja nami, kwa maana kutoka juu ya msalaba Mwanangu amenikabidhi ninyi. Kwa bahati mbaya wanangu wengi hawakujua upendo wa Mwanangu, wengi hawataka kumjua. Loo, wanangu, mabaya mengi yatoka kwa wale ambao hawana budi ya kuona na kuelewa ili kuamini! Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, katika kimya ya moyo wenu sikilizeni sauti ya Mwanangu, ili moyo wenu uwe makazi yake wala usiwe giza na huzuni, bali uangaziwe na mwanga wa Mwanangu. Tafuteni matumaini kwa imani, maana imani ni maisha ya roho. Ninawaalika tena: salini! Salini ili kuishi imani katika unyenyekevu, katika amani ya kiroho na mkiangaziwa na mwanga. Wanangu, msijaribu kuelewa yote mara moja, maana Mimi nami sikuelewa yote mara moja, lakini niliyaamini maneno ya kimungu aliyoyasema Mwanangu, Yeye aliyekuwa mwanga wa kwanza na mwanzo wa Ukombozi. Enyi mitume wa moyo wangu, ninyi mnaosali, mnaojitolea, mnaopenda wala msiohukumu: ninyi nendeni mkaeneze ukweli, maneno ya Mwanangu, Injili. Ninyi kweli, ni Injili iliyo hai, ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu. Mwanangu na mimi tutakuwa karibu nanyi, tutawatia moyo na kuwajaribu. Wanangu, ombeeni daima na hasa baraka ya wale ambao Mwanangu amebariki mikono yao, yaani Wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kwa mapenzi ya Baba wa mbinguni, kama Mama wa Yule anayewapendeni, nipo hapa pamoja nanyi niwasaidieni kumjua, kumfuata. Mwanangu amewaachieni nyayo za hatua zake, ili iwe rahisi zaidi kwenu kumfuata. Msiogope, msiwe na wasiwasi. Mimi nipo pamoja nanyi! Msichoke, maana sala nyingi na sadaka zinahitajiwa kuwasaidia wale wasiomwomba, wasiompenda na wasiomjua Mwanangu. Muwasaidie mkiona ndani yao ndugu zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, sikilizeni sauti yangu ndani yenu, hisieni upendo wangu. Kwa hiyo salini: salini mkitenda, salini mkitoa. Salini kwa upendo, salini kwa matendo na kwa fikira, kwa jina la Mwanangu. Kadiri mtakavyotoa upendo, ndivyo mtakavyoupokea. Upendo utokao katika Upendo huangaza ulimwengu. Ukombozi ni upendo, na upendo hauna mwisho. Wakati Mwanangu atakapokuja tena duniani, atatafuta upendo katika mioyo yenu. Wanangu, Yeye alifanya kwa ajili yenu matendo mengi ya upendo. Ninawafundisha kuyaona, kuyaelewa na kumshukuru mkimpenda na kumsamehe sikuzote na tena jirani yako. Kwa kuwa kumpenda Mwanangu maana yake ni kusamehe. Mwanangu hapendwi, ikiwa hatuwezi kumsamehe jirani yetu, ikiwa hatuwezi kumwelewa jirani yetu, ikiwa tunamhukumu. Wanangu, faida gani kusali, msipopenda wala msiposamehe? Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nikiwatazama hapa mmekusanyika kunizunguka, Mama yenu, ninaona nafsi safi nyingi. Ninawaona wanangu wengi wanaotafuta upendo na faraja lakini hakuna mtu anayewapa. Ninawaona hata wale wanaotenda mabaya maana hawana mifano myema, maana hawajamjua mwanangu. Mwanangu anawatuma ninyi kwangu, Mama, sawa kwa wote, niwafundisheni kupenda, ili muelewe ya kuwa ninyi ni ndugu. Ninatamani kuwasaidia. Mitume wa upendo wangu, kwa mwanangu yamtosha tamaa hai ya imani na upendo na atayakubali, lakini mnapaswa kustahili, kuwa na tamaa na mioyo wazi, Mwanangu huingia katika mioyo wazi. Mimi kama Mama ninatamani kwamba mjue Mwanangu katika kweli: Mungu aliyezaliwa na Mungu, kwamba mjue ukuu wa Upendo wake, ambao mnahitaji. Yeye amezichukua juu yake dhambi zenu, ameupata Ukombozi wenu, na badala yake anaomba mpendane ninyi kwa ninyi. Mwanangu ni upendo, Yeye anawapenda watu wote bila tofauti, watu wote wa nchi zote, wa mataifa yote. Ikiwa ninyi, wanangu, mngeishi upendo wa Mwanangu, ufalme wake ungekwisha kuwa duniani. Kwa hiyo, Mitume wa upendo wangu, salini, salini ili Mwanangu na upendo wake wawe ndani yenu nanyi muweze kuwa mfano wa upendo na muweze kuwasaidia wote wale ambao hawajamjua Mwanangu. Msisahau kamwe kwamba Mwanangu, mmoja na utatu, anawapendeni. Pendeni na wombeeni wachungaji wenu. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`