Our Lady of Medjugorje Messages containing 'umoja'

Total found: 6
Wanangu wapendwa, katika wakati huu wa wasiwasi nawaalikeni tena kutembea nyuma ya Mwanangu, na kumfuata. Nayajua maumivu, mateso na taabu zenu, lakini katika Mwanangu mtapumzika, ndani yake mtapata amani na wokovu. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu amewakomboa ninyi kwa msalaba wake akawajalieni kuwa tena wana wa Mungu na kuwafundisha kumwita tena "Baba" yenu, Mungu aliye mbinguni. Ili muwe wapenzi wa Mungu Baba, basi muwe na mapendo na msamaha, kwa kuwa Baba yenu ni upendo na msamaha. Salini na fungeni, kwa maana hii ndiyo njia ya kujua na kumfahamu Baba aliye mbinguni. Mtakapomjua huyo Baba, mtafahamu ya kuwa Yeye tu ni muhimu kwenu (Maria Mtakatifu amenena hayo kwa nguvu na amkazo sana). Mimi, nikiwa Mama, nataka wanangu wawe watu wenye umoja ambamo Neno la Mungu husikilizwa na kutekelezwa. Kwa hiyo, enyi wanangu, mfuateni Mwanangu, muwe kitu kimoja naye, muwe wana wa Mungu. Pendeni wachungaji wenu kama vile Mwanangu alivyowapenda alipowaita kuwatumikia ninyi. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, tafadhali muelewe, muwe tayari wote, kwa matumaini makuu, kufungua mioyo yenu; hivyo mngeelewa yote, mngeelewa kwa upendo gani nawaiteni, kwa upendo gani nataka kuwageuza, ili kuwafurahisha, kwa upendo gani nataka kuwafanya wafuasi wa Mwanangu na kuwapa amani katika ukamilifu wa Mwanangu. Mngeelewa ukuu wa moyo wangu wa kimama, kwa hiyo, wanangu, salini, maana kwa njia ya kusali tu imani yenu hukua na upendo wenu huzaliwa, upendo ambao utapunguza uzito wa msalaba kwa maana hamtakuwa peke yenu kuubeba. Katika umoja na Mwanangu, tukuzeni jina la Baba wa Mbinguni. Salini, salini mpate tuzo la upendo, maana upendo ni ukweli wa pekee, upendo husamehe yote, hutumikia wote na kuwaona wote kama ndugu. Enyi wanangu, mitume wangu, udhamini ambao Baba wa Mbinguni amewawekeni, kwa njia yangu, mtumishi Wake, ni kitu kikubwa, ili kusaidia wale wasiomjua, kusudi zapatanishwe naye, kusudi wamfuate, kwa hiyo nawafundisheni kupenda, maana mkiwa na upendo tu mnaweza kumjibu. Nawaalikeni tena: pendeni wachungaji wenu, salini ili katika wakati huu wa shida jina la Mwanangu atukuzwe kwa njia ya mwongozo wao. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Sababu ya kukaa kwangu pamoja nanyi, utume wangu, ni kuwasaidieni ili wema ushinde, hata kama kwa sasa haya yaonekana ni kitu kigumu sana. Najua kwamba mambo mengi hamyaelewi, kama vile sikuelewa mengi ambayo Mwanangu alinifundisha akiwa alipokua pamoja nami, lakini mimi nilimsadiki na kumfuata. Haya nawaombea ninyi pia, kunisadiki na kunifuata, lakini, wanangu, kunifuata maana yake ni kupenda mwanangu kuliko wote, kumpenda katika kila mtu pasipo ubaguzi. Ili kuweza kufanya haya yote nawaalikeni tena kujinyima, kusali na kufunga. Nawaalikeni ili maisha ya roho yenu yawe ni Ekaristi. Nawaalikeni muwe mitume wangu wa mwanga, ambao wataueneza upendo na rehema ulimwenguni. Wanangu, maisha yenu ni mpigo tu wa moyo mbele ya uzima wa milele. Mtakapokuwa mbele ya Mwanangu, Yeye ataona katika mioyo yenu kiasi cha upendo mliokuwa nao. Ili kuweza kueneza kwa njia ya haki upendo nitamwomba Mwanangu kusudi kwa njia ya upendo awapeni umoja kati yenu na umoja kati yenu na wachungaji wenu. Mwanangu daima anajitoa upya kwa njia yao na anafanya mioyo yenu mipya. Msisahau hilo. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, kwa njia ya upendo mkubwa wa Baba wa Mbinguni, mimi ni pamoja nanyi kama Mama yenu nanyi ni pamoja nami kama wanangu, kama mitume wa upendo wangu ambao ninakusanya daima karibu nami. Wanangu, ninyi ni wale ambao, mkisali, yawapasa kujitolea kabisa kwa Mwanangu, ili kwamba si ninyi tena mnaoishi, bali ni Mwanangu ndani yenu; ili wale wote wasiomjua wamwone ndani yenu na watake kumjua. Salini ili waone ndani yenu unyenyekevu thabiti na wema, utayari kuwatumikia wengine; waone kwamba mnaishi kwa moyo wito wenu duniani, mkishirikiana na Mwanangu. Waone ndani yenu upole, rehema na upendo kuelekea Mwanangu, kama vile kuelekea ndugu na dada zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, hamna budi kusali sana na kutakasa mioyo yenu, ili ninyi muwe wale wa kwanza waendao katika njia ya Mwanangu; ili ninyi muwe wale wenye haki wanaoungana na haki ya Mwanangu. Wanangu, kama mitume wangu lazima muungane na ushirika utokao katika Mwanangu, ili wanangu wasiomjua Mwanangu watambue ushirika wa upendo na watake kutembea katika njia ya uzima, njia ya umoja na Mwanangu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kama Mama ambaye anajua wana wake, ninajua ya kuwa mnamtamani Mwanangu. Ninajua ya kuwa mnatamani ukweli, amani, na kilicho chema wala si uovu. Kwa sababu hiyo mimi, kama Mama, kwa njia ya upendo wa Mungu ninawaita ninyi na kuwaalika ili, mkisali kwa moyo safi na wazi, mmtambue ninyi wenyewe Mwanangu, upendo wake, na Moyo wake wenye rehema. Mwanangu alikuwa akiona uzuri katika vitu vyote. Yeye anatafuta mema, hata yale mema madogo yanayofichika, katika roho zote, ili kusamehe maovu. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawaalika kumwabudu, kumshukuru daima na kumstahili. Maana yeye aliwaambieni maneno ya kimungu, maneno ya Mungu, maneno yaliyo kwa watu wote na hata milele. Kwa hiyo, wanangu, ishini uchangamfu, umakini, umoja na muwe na mapenzi baina yenu. Haya mnapaswa kuwa nayo katika ulimwengu wa leo: hivyo mtakuwa mitume wa upendo wangu, hivyo mtashuhudia Mwanangu kwa jinsi ya haki. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Mwanangu mpenzi alimwomba sikuzote na kumtukuza Baba wa Mbinguni. Sikuzote alikuwa amemwambia yote na kujiachia katika mapenzi yake. Hivyo mnapaswa kufanya hata ninyi, wanangu, maana Baba wa Mbinguni anawasikiliza sikuzote wanawe. Moyo wa umoja katika moyo mmoja: upendo, mwanga na uhai. Baba wa Mbinguni amejitolea kwa njia ya sura ya kibinadamu, na sura ile ndiyo sura ya Mwanangu. Ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnapaswa sikuzote kupokea sura ya Mwanangu katika mioyo yenu na katika fikira zenu. Ninyi mnapaswa sikuzote kuufikiria upendo wake na sadaka yake. Mnapaswa kusali ili kusudi mwone uwepo wake sikuzote. Maana, enyi mitume wa upendo wangu, hii ni jinsi ya kuwasaidia wale wote wasiomjua Mwanangu, wale ambao hawajajua upendo wake. Wanangu, someni kitabu cha Injili: ni sikuzote kitu kipya, ni kinachowaunganisha na Mwanangu, aliyezaliwa kwa kuwaletea maneno ya uzima wanangu wote na kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya wote. Mitume wa upendo wangu, mkisukumwa na upendo kumwelekea Mwanangu, leteni upendo na amani kwa ndugu zenu wote. Msimhukumu mtu, pendeni kila mtu kwa njia ya upendo kwa kumwelekea Mwanangu. Hivyo mtashughulika hata na roho zenu, nayo ni yenye thamani kuliko kitu chochote mlicho nacho. Ninawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`