Our Lady of Medjugorje Messages containing 'wanyenyekevu'

Total found: 6
Wanangu wapendwa, nawapendeni, ninyi nyote, watoto wangu nyote, muwe wote moyoni mwangu, ninyi nyote mmepata upendo wangu wa kimama na ninatamani kuwaongoza nyote ili mjue furaha ya Mungu. Kwa hiyo nawaalikeni: nahitaji mitume wanyenyekevu ambao, kwa moyo mkunjufu, wanapokea Neno la Mungu na ambao wako tayari kuwasaidia watu wengine ili, kwa njia ya Neno la Mungu, waelewe maana ya maisha yao. Ili muweze kufanya hayo, wanangu, yawapasa, kwa njia ya kusali na kufunga, kusikiliza kwa moyo mkunjufu na kujifunza kujidhili au kujinyenyekesha. Yawapasa kujifunza kukataa yote yanayowatenganisha na Neno la Mungu na kutamani tu yanayowakaribisha. Msiogope, mimi nipo hapa. Ninyi si peke yenu. Namwomba Roho Mtakatifu ili awafanye wapya, ili awaimarishe. Namwomba Roho Mtakatifu, ili mkisaidia wengine, muweze kujiponya nyinyi wenyewe. Naomba ili, kwa njia yake, muwe wana wa Mungu na mitume wangu.
Kisha kwa mahangaiko makubwa Bikira Maria alisema:
Kwa ajili ya Yesu, kwa ajili ya mwanangu, pendeni wale ambao Yeye aliwaita mkitamani baraka ya mikono ile ambayo Yeye tu ameyaweka wakfu. Msiyaruhusu maovu yatawale. Nawaalikeni tena: ni kwa njia ya wachungaji wangu tu moyo wangu utashinda. Msiyaruhusu maovu yawatenganisheni na wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nawaalika kusali pasipo kuomba, bali mkitoa sadaka, mkijitolea wenyewe. Nawaalika kuleta habari ya ukweli na upendo wenye rehema. Ninamwomba Mwanangu kwa ajili yenu, kwa imani yenu, inayoendelea kupunguka katika mioyo yenu. Ninamwomba awasaidieni kwa Roho ya Mungu, kama vile mimi nami ninavyotaka kuwasaidieni kwa roho ya kimama. Wanangu, itawabidi kujiboresha! Wale tu walio safi, wanyenyekevu na wamliojaa upendo wanautegemeza ulimwengu, wanaokoa ulimwengu na wao wenyewe. Wanangu, Mwanangu ndiye moyo wa ulimwengu: lazima kumpenda na kumwomba, na si kumsaliti daima tena. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, mstawishe imani katika mioyo ya watu kwa mfano wenu, kwa sala yenu na kwa upendo wenye rehema. Mimi nipo karibu nanyi na nitawasaidia. Salini ili wachungaji wenu wapate mwanga zaidi kadiri wawezavyo, ili waweze kuangaza wale wote wanaoishi gizani. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nawashukuru kwa kuitikia miito yangu na kukusanyika karibu nami, Mama yenu wa mbinguni. Najua kwamba mnanifikiri kwa upendo na matumaini. Mimi ninawapendeni nyote kama vile anavyowapendeni Mwanangu ambaye, kwa upendo wake wenye huruma, ananituma nije kwenu, mara nyingi pia. Yeye, aliyekuwa mtu na aliye Mungu, Mmoja na Utatu; Yeye aliyeteswa kwa ajili yenu mwilini na nafsini. Yeye aliyejifanya Mkate ailishe nafsi zenu na hivyo kuziokoa. Wanangu, nawafundisha jinsi ya kustahili upendo wake, kumwelekeza mawazo yenu, kumwishi Mwanangu. Mitume wa upendo wangu, ninawafunika kwa joho langu kwa sababu, kama Mama yenu, nataka kuwalinda. Nawasihi: mwuombee ulimwengu wote: moyo wangu unateswa. Dhambi zinaongezeka, ni nyingi mno. Lakini kwa msaada wenu – mlio wanyenyekevu, wanyofu, wenye upendo, watawa na watakatifu – moyo wangu utashinda. Mpendeni Mwanangu kupita wote na ulimwengu wote kwa njia yake. Msisahau kabisa ya kuwa kila ndugu yenu ana ndani yake kitu cha thamani: nafsi. Kwa hiyo, wanangu, pendeni wale wote wasiomjua Mwanangu ili kwa njia ya maombi na upendo utokao katika maombi, wawe wema zaidi. Ili wema uweze kushinda ndani yao. Ili nafsi zao ziweze kuokoka na kupata uzima wa milele. Enyi mitume wangu, wanangu. Mwanangu aliwaambieni mpendane. Hiyo iandikwe mioyoni mwenu na kwa kusali jaribuni kuishi upendo huu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninawaelekea ninyi kama Mama yenu, Mama wa wenye haki, Mama wa wale wanaopenda na kuteseka, Mama wa watakatifu. Wanangu, ninyi pia mnaweza kuwa watakatifu: ni juu yenu. Watakatifu ni wale wanaompenda Baba wa Mbinguni kupita kiasi, wale wanaompenda kupita chochote. Kwa hivyo, wanangu, jaribuni daima kuboreka. Kama ninyi mnajaribu kuwa wema, mtaweza kuwa watakatifu, hata kama hamfikiri hiyo juu yenu. Kama mnafikiri kuwa wema, ninyi sio wanyenyekevu na kiburi huwatenga kutoka utakatifu. Katika ulimwengu huu wa wasiwasi, umejaa vitisho, mikono yako, mitume wa upendo wangu, inapaswa kuwa imenyoshwa katika maombi na rehema. Kwangu, wanangu, nipeni zawadi ya Rozari, mawaridi ninayopenda sana! Mawaridi yangu ni maombi yenu msemayo kwa moyo wote, na sio yale msemayo kwa midomo yenu tu. Mawaridi yangu ni matendo yenu ya maombi, imani na upendo. Wakati alipokuwa mtoto, mwanangu aliniambia kwamba watoto wangu watakuwa wengi na wataniletea mawaridi mengi. Sikuelewa, sasa najua kwamba ninyi ni watoto wale, wanaoniletea mawaridi wakati mnapompenda mwanangu kupita yote, wakati mnaposali kwa moyo wote, wakati mnapowasaidia walio maskini zaidi. Hayo ndiyo mawaridi yangu! Hii ndiyo imani, inayosababisha kila kitu katika maisha kifanyike kwa upendo; na kiburi hakijulikani; na muwe tayari daima, kusamehe upesi, bila kuhukumu na daima mjaribu kuelewa ndugu yako. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, muwaombeeni wale wasiojua kupenda, wale wasiowapenda, wale waliowatenda mabaya, wale ambao hawakujua upendo wa Mwanangu. Wanangu, ninawaomba haya, kwa sababu kumbukeni: kuomba maana yake ni kupenda na kusamehe. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, inasikitisha kwamba katikati yenu, wanangu, yapo mashindano mengi, chuki, masilahi yenu wenyewe na ubinafsi. Wanangu, hivi kwa urahisi mnamsahau Mwanangu, maneno Yake na upendo Wake. Imani inazimika katika roho nyingi na mioyo imetekwa na vitu vya ulimwenguni. Lakini moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa katikati yenu kuna wale wanaoamini na kupenda, wale ambao wanajaribu kumkaribia Mwanangu zaidi na zaidi, ambao wanamtafuta bila kuchoka na namna hii, wananitafuta hata mimi. Hawa ndio wanyenyekevu na wapole ambao, pamoja na maumivu na mateso wanayoyachukua katika kimya, pamoja na tumaini lao na hasa pamoja na imani yao, ni mitume wa upendo wangu. Wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawafundisha ya kuwa Mwanangu hatafuti sala tu pasipo kuchoka bali hata matendo na hisia. Salini ili katika sala mpate kuzidi katika imani na katika upendo. Mpendane wenyewe kwa wenyewe: hilo ndilo analotaka Yeye, hiyo ndiyo ni njia ya uzima wa milele. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu ameleta mwanga kwa ulimwengu huu. Ameuleta kwa wale ambao walitaka kuuona na kuupokea. Hawa muwe ninyi, maana huu ndio mwanga wa ukweli, wa amani na wa upendo. Mimi ninawaongoza kama mama kumwabudu Mwanangu, kumpenda pamoja nami. Fikira zenu, maneno na matendo yenu yamwelekee Mwanangu, yawe katika jina Lake: hapo tu moyo wangu utajazwa. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Hata leo mimi ni pamoja nanyi ili kuwaambieni: wanangu, yule anayesali hana hofu ya wakati ujao wala hapotezi tumaini. Mmechaguliwa kwa kuleta furaha na amani, kwa maana ni wangu. Nimekuja hapa pamoja na jina: Malkia wa Amani kwa sababu ibilisi anataka kuleta wasiwasi na vita, anataka kuijaza mioyo yenu kwa hofu ya wakati ujao na wakati ujao ni wa Mungu. Kwa hiyo muwe wanyenyekevu, salini na acheni yote katika mikono ya Yeye aliye Juu aliyewaumba. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`