Our Lady of Medjugorje Messages by month Aprili

Wanangu wapendwa, msiwe na mioyo migumu, iliyofungwa na iliyojaa hofu. Pokeeni upendo wangu wa kimama uiangaze na kuijaza mioyo yenu upendo na matumaini, ili, kama Mama, niyalainishe maumivu yenu: ninayajua, na nimeyaonja. Maumivu huinua nayo ni sala kuu kuliko zote. Mwanangu huwapenda hasa wanaopokea maumivu. Alinituma Mimi niyalainishe na kuwaletea matumaini. Mumwamini Yeye. Najua kuwa ni vigumu kwenu, maana mnaona giza linalozidi kuongeza karibu yenu pande zote. Wanangu, giza mtalivunja kwa njia ya sala na upendo. Yule anayesali na kupenda haogopi, ana matumaini na upendo wenye huruma: Anaona mwanga, na anamwona Mwanangu. Kama mitume wangu nawaalika mjaribu kuwa mfano wa upendo wenye huruma na wenye matumaini. Salini sikuzote tena kwa ajili ya kupata upendo mwingi kadiri muwezavyo, maana upendo huleta mwanga unaovunja kila giza, na humleta Mwanangu. Msiogope, ninyi si peke yenu: Mimi nipo pamoja nanyi! Ninawasihi waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na upendo kila wakati na wawe na matendo ya upendo kwa Mwanangu, kwa njia yake na kwa kumkumbuka Yeye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Mimi nipo pamoja nanyi hata leo niwaongozeni kwenye wokovu. Moyo wenu una wasiwasi maana roho yenu ni dhaifu na imechoka kwa mambo yote ya dunia. Ninyi wanangu, ombeni Roho Mtakatifu awageuze na kuwajaza nguvu yake ya imani na tumaini ili muweze kuwa imara katika kupambana kwenu na maovu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea kwenye Mwanangu Yesu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, nimewachagua ninyi, mitume wangu, kwa maana kila mmoja wenu huchukua ndani yake jambo njema. Ninyi mnaweza kunisaidia ili ule upendo ambao kwao Mwanangu amekufa, na kufufuka baadaye, ushinde tena. Kwa hiyo nawaalika, mitume wangu, kujaribu kuona katika kila kiumbe cha Mungu, katika wanangu wote, kitu chema na kujitahidi kuwaelewa. Wanangu, ninyi nyote ni kaka na dada kwa njia ya huyo Roho Mtakatifu. Ninyi mliojaa upendo kwa ajili ya Mwanangu, mnaweza kuwaeleza wote ambao hawajui cho chote kuhusu upendo huo, yote mnayoyafahamu. Ninyi mmejua upendo wa Mwanangu, mnaelewa ufufuko wake, na mnamgeuzia macho kwa furaha. Haja yangu ya kimama ni kwamba wanangu wote waungane katika upendo wa Yesu. Kwa hiyo nawaalika, mitume wangu, kuishi kwa furaha Ekaristi maana, katika Ekaristi, mwanangu anajitoa kwa ajili yenu tena na tena, na kwa mfano wake, anawaonyesha namna ya kutoa upendo na sadaka kwa jirani. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Fungueni mioyo yenu kwa neema ambayo Mungu anawapa kwa njia yangu kama vile ua linalojifungua kwa miali ya joto la jua. Muwe sala na upendo kwa wale wote walio mbali na Mungu na upendo Wake. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawaombea nyote kwa Mwanangu Yesu na ninawapenda kwa upendo usio na mipaka. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Kwa upendo wa kimama nataka kuwasaidia ili maisha yenu ya kusali na kutubu iwe juhudi ya kweli ya kumjongea Mwanangu na nuru yake ya kimungu, ili muweze kutengana na dhambi. Kila sala, kila Misa na kila mfungo ni juhudi ya kumjongea Mwanangu, msukumo kwa utukufu wake na kuepukana na dhambi. Ni njia ya muungano mpya wa Baba mwema na wanao. Kwa hiyo, wanangu wapendwa, kwa unyofu wa moyo uliojaa upendo mliite jina la Baba wa Mbinguni, ili awatie nuru ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu mtakuwa chemchemi ya upendo wa Mungu: kwenye chemchemi hiyo wale wote wasiomjua Mwanangu watakunywa, wote wenye kiu ya upendo na amani ya Mwanangu. Nawashukuru! Salini kwa ajili ya wachungaji wenu. Mimi nawaombee na nataka waonje siku zote baraka ya mikono yangu na tegemeo la Moyo wangu wa kimama.
Wanangu wapendwa! Salini, salini, mwendelee kusali ili mioyo yenu ifungukie kupokea imani jinsi ua linavyofunguka kuelekea mianga ya joto la jua. Huo ni wakati wa neema ambao Mungu anawajalia kwa njia ya uwepo wangu, lakini ninyi mpo mbali na moyo wangu. Kwa hiyo nawaalikeni kwa uongofu binafsi na kwenye sala katika familia zenu. Maandiko matakatifu yawe daima kichocheo chenu. Nawabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`