Our Lady of Medjugorje Messages by month Agosti

Wanangu wapendwa! Leo nataka kushirikiana pamoja nanyi furaha ya mbinguni. Ninyi wanangu fungueni mlango wa moyo ili katika moyo wenu matumaini, amani na mapendo ambazo Mungu peke yake anaweza kutoa ziweze kukua. Wanangu, mnapenda mno dunia na mambo ya dunia, kwa hiyo Shetani huwatikisa kama upepo ufanyavyo na mawimbi ya bahari. Kwa hiyo mnyororo wa maisha yenu uwe sala ya moyo na kumwabudu Mwanangu Yesu. Kwake mtolee maisha yenu yajayo ili muwe ndani Yake furaha na mfano kwa watu wengine kwa njia ya matendo yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, nimekuja kwenu, katikati yenu, ili mnipe mahangaiko yenu, niweze kuyaleta mbele ya Mwanangu na kuwaombeeni kwake kwa manufaa yenu. Najua kuwa kila mmoja wenu ana mahangaiko yake, majaribu yake. Kwa hiyo kwa moyo wa kimama nawaalikeni: Njooni kwenye Meza ya Mwanangu! Yeye humega mkate kwa ajili yenu, huwapa Yeye mwenyewe. Huwapa matumaini. Anawaomba kuwa na imani zaidi, matumaini zaidi, utulivu zaidi. Anawaomba mpigane ndani yenu dhidi ya ubinafsi, hukumu na udhaifu wa kibinadamu. Kwa hiyo Mimi, kama Mama, nawaambieni: salini, maana sala huwapa nguvu ya kupigana ndani yenu. Mwanangu, alipokuwa mtoto, aliniambia mara nyingi ya kuwa wengi watanipenda na kuniita "Mama". Mimi hapa, katikati yenu, nasikia upendo na kuwashukuru! Kwa njia ya upendo huu namwomba Mwanangu ili hakuna hata mmoja wenu, wanangu, arudiye nyumbani jinsi alivyokuja. Ili mlete matumaini, rehema na upendo kadiri muwezavyo; ili muwe mitume wa upendo wangu, wanaoshuhudia kwa maisha yao kwamba Baba aliye Mbinguni ni chemchemi ya uzima si ya mauti. Wanangu wapendwa, nawaomba tena kwa moyo wa kimama: waombeeni wateule wa Mwanangu, kwa ajili ya mikono yao iliyobarikiwa, kwa ajili ya wachungaji wenu, ili waweze kumhubiri Mwanangu kwa upendo mwingi wawezavyo, na hivyo kusababisha wongofu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, hata leo ninawaalika: muwe sala. Sala iwe mabawa kwa ajili ya mkutano kati yenu na Mungu. Ulimwengu upo katika wakati wa kujaribiwa, kwa maana umemsahau na kumwacha Mungu. Kwa hiyo wanangu, muwe wale wanaomtafuta na kupenda Mungu kuliko yote. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaongoza kwa Mwanangu, lakini ninyi hamna budi kunena "NDIYO" yenu katika uhuru wa wana wa Mungu. Nawaombeeni na kuwapenda, wanangu, kwa upendo usio na mwisho. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, mimi, kama Mama apendaye wanawe, natambua jinsi ulivyo mgumu muda huu mnaouishi. Naona mateso yenu, lakini jueni kwamba hamko peke yenu: Mwanangu yu pamoja nanyi! Yeye yupo popote, asiyeonekana, lakini mtaweza kumwona ikiwa mtamwishi. Yeye ndiye nuru inayoangaza roho yenu na kuleta amani. Yeye ndiye Kanisa, mnalopaswa kulipenda, kuliombea na kulilinda daima: si kwa maneno tu, bali kwa matendo ya upendo. Wanangu, fanyeni yote ili Mwanangu ajulikane kwa watu wote, na aweze kupendwa, kwa maana ukweli ni katika Mwanangu, aliyezaliwa na Mungu, Mwana wa Mungu. Msipoteze muda kwa kufikiri mno; mtajitenganisha na ukweli. Pokeeni Neno lake kwa moyo mnyofu na kuliishi. Mkiishi Neno lake, mtasali. Mkiishi Neno lake, mtapenda kwa upendo wenye huruma, na mtapendana. Kwa kadiri mtakavyokuwa na upendo hivyo ndivyo mtakavyokuwa mbali na kifo. Kwa wale watakaoishi na kulipenda Neno la Mwanangu, kifo kitakuwa uhai kwao. Nawashukuru! Salini kwa ajili ya kuweza kuona Mwanangu katika wachungaji wenu. Salini kwa ajili ya kuweza kumkumbatia katika wao.
Wanangu wapendwa! Salini kwa nia zangu maana Shetani ataka kuangamiza mpango wangu nilio nao hapa na kuwaibia amani: Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini ili Mungu aweze kutenda kazi kwa njia ya kila mmoja wenu. Mioyo yenu iwe wazi kupokea mapenzi ya Mungu. Mimi nawapendeni na kubariki kwa baraka ya kimama. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Sababu ya kukaa kwangu pamoja nanyi, utume wangu, ni kuwasaidieni ili wema ushinde, hata kama kwa sasa haya yaonekana ni kitu kigumu sana. Najua kwamba mambo mengi hamyaelewi, kama vile sikuelewa mengi ambayo Mwanangu alinifundisha akiwa alipokua pamoja nami, lakini mimi nilimsadiki na kumfuata. Haya nawaombea ninyi pia, kunisadiki na kunifuata, lakini, wanangu, kunifuata maana yake ni kupenda mwanangu kuliko wote, kumpenda katika kila mtu pasipo ubaguzi. Ili kuweza kufanya haya yote nawaalikeni tena kujinyima, kusali na kufunga. Nawaalikeni ili maisha ya roho yenu yawe ni Ekaristi. Nawaalikeni muwe mitume wangu wa mwanga, ambao wataueneza upendo na rehema ulimwenguni. Wanangu, maisha yenu ni mpigo tu wa moyo mbele ya uzima wa milele. Mtakapokuwa mbele ya Mwanangu, Yeye ataona katika mioyo yenu kiasi cha upendo mliokuwa nao. Ili kuweza kueneza kwa njia ya haki upendo nitamwomba Mwanangu kusudi kwa njia ya upendo awapeni umoja kati yenu na umoja kati yenu na wachungaji wenu. Mwanangu daima anajitoa upya kwa njia yao na anafanya mioyo yenu mipya. Msisahau hilo. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! Leo pia Yeye Aliye Juu anijalia neema ya kuwa pamoja nanyi na kuwaongoza mpate kutubu. Siku hata siku Mimi napanda mbegu na kuwaalika kutubu ili muweze kuwa sala, amani, upendo na ngano ambayo ikifa huzaa mara mia. Sipendi, wanangu wapendwa, mpate kujuta kwa yote mliyoweza kufanya wala hamkufanya. Kwa hiyo, enyi wanangu, tena kwa moyo wa furaha semeni: “ Nataka kuwa ishara kwa watu wengine”. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, tafadhali muelewe, muwe tayari wote, kwa matumaini makuu, kufungua mioyo yenu; hivyo mngeelewa yote, mngeelewa kwa upendo gani nawaiteni, kwa upendo gani nataka kuwageuza, ili kuwafurahisha, kwa upendo gani nataka kuwafanya wafuasi wa Mwanangu na kuwapa amani katika ukamilifu wa Mwanangu. Mngeelewa ukuu wa moyo wangu wa kimama, kwa hiyo, wanangu, salini, maana kwa njia ya kusali tu imani yenu hukua na upendo wenu huzaliwa, upendo ambao utapunguza uzito wa msalaba kwa maana hamtakuwa peke yenu kuubeba. Katika umoja na Mwanangu, tukuzeni jina la Baba wa Mbinguni. Salini, salini mpate tuzo la upendo, maana upendo ni ukweli wa pekee, upendo husamehe yote, hutumikia wote na kuwaona wote kama ndugu. Enyi wanangu, mitume wangu, udhamini ambao Baba wa Mbinguni amewawekeni, kwa njia yangu, mtumishi Wake, ni kitu kikubwa, ili kusaidia wale wasiomjua, kusudi zapatanishwe naye, kusudi wamfuate, kwa hiyo nawafundisheni kupenda, maana mkiwa na upendo tu mnaweza kumjibu. Nawaalikeni tena: pendeni wachungaji wenu, salini ili katika wakati huu wa shida jina la Mwanangu atukuzwe kwa njia ya mwongozo wao. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`