Our Lady of Medjugorje Messages by month Machi

Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema nawaalika nyote kufungua mioyo yenu kwa huruma ya Mungu ili kwa ajili ya sala, toba na maamuzi kwa ajili ya utakatifu muanze maisha mapya. Majira haya ya kuchipua yanawaita, katika mawazo yenu na mioyo yenu, kuishi maisha mapya, kujifanya upya. Kwa hiyo, wanangu, mimi nipo pamoja nanyi niwasaidie ili mkatakati wa kukata shauri muweze kusema NDIYO kwa Mungu na amri za Mungu. Ninyi si peke yenu, mimi nipo pamoja nanyi kwa njia ya neema ambayo Yeye Aliye juu hunijalia kwa ajili yenu na kwa uzao wenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama naja kuwasaidieni kuwa na upendo zaidi, maana yake imani zaidi. Naja kuwasaidieni kuishi kwa upendo maneno ya Mwanangu, ili ulimwengu uwe tofauti. Kwa sababu hiyo nawakusanya, mitume wa mapendo yangu, karibu nami. Niangalieni kwa upendo, ongeeni nami kama vile na Mama kuhusu mateso yenu, maumivu yenu, furaha zenu. Ombeni ili nisali Mwanangu kwa ajili yenu. Mwanangu ni mwenye rehema na haki. Moyo wangu wa kimama ungependa ninyi pia muwe hivyo. Moyo wangu wa kimama ungependa ya kuwa ninyi, mitume wa mapendo yangu, mngeongea kwa maisha yetu juu ya Mwanangu na juu yangu pamoja na watu wote walio karibu nanyi, ili ulimwengu uwe tofauti, ili wairudie imani na tumaini. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini kwa moyo. Salini kwa upendo, salini kwa matendo mema. Salini ili wote wamjue Mwanangu, ili ulimwengu ugeuke, ulimwengu uokoke. Ishini kwa upendo maneno ya Mwanangu. Msihukumu, lakini mpendaneni, ili Moyo wangu uweze kushinda. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Leo ninawaletea upendo wangu. Mungu ameniruhusu kuwapenda ninyi na kwa upendo nawaalika mwongoke. Wanangu, ninyi ni maskini katika upendo, na wala hamjaelewa bado ya kuwa Mwanangu Yesu ametolea maisha Yake ili awaokoeni na kuwapa uzima wa milele. Kwa hiyo salini wanangu, salini ili muweze kuelewa katika sala upendo wa Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ujio wangu kwenu ni zawadi ya Baba wa Mbinguni kwa ajili yenu. Kwa njia ya upendo wake ninakuja kuwasaidieni kupata njia inayowangoza kwenye ukweli, na kupata njia inayowaongoza kwa Mwanangu. Ninakuja kuwathibitishia ukweli. Nataka kuwakumbushia maneno ya Mwanangu. Yeye aliyatamka maneno ya wokovu kwa ulimwengu wote, maneno ya upendo kwa watu wote, ule upendo aliouonyesha kwa kujitolea kwake sadaka. Lakini hata leo wanangu wengi hawamjui, hawataki kumjua, hawamjali. Kwa sababu ya kutokujali kwao, moyo wangu unateseka kwa uchungu. Mwanangu amekuwa daima katika Baba. Alipozaliwa duniani, ametuletea Umungu, wakati kutoka kwangu ameuchukua ubinadamu. Kwa njia yake Neno limefika katikati yetu. Kwa njia yake Mwanga, ambao hupenyeza mioyoni, huiangaza, huijaza upendo na faraja, umeingia ulimwenguni. Wanangu, wanaweza kumwona Mwanangu wale wote wanaompenda, kwa kuwa uso wake huonekana kwa njia ya mioyo inayojaa mapendo kumwelekea Yeye. Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, mnisikilize! Acheni uovu na ubinafsi. Msiishi tu kwa ajili ya vitu vya ulimwengu, vinavyoharibika. Mpendeni Mwanangu na muwawezeshe wengine kuutambua uso kwa njia ya mapendo mliyo nayo kwake. Mimi nitawasaidia kumjua zaidi. Mimi nitawaeleza kuhusu Yeye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Hata leo pia Yeye Aliye Juu ameniruhusu kuwa pamoja nanyi na kuwaongoza katika njia ya uwongofu. Mioyo mingi imejifunga kwa neema wala haitaki kusikiliza mwaliko wangu. Ninyi wanangu salini na pambaneni na kishawishi na mipango yote ya uovu ambayo anayowapatia shetani kwa njia ya mambo ya kisasa. Muwe hodari katika kusali na mkishika msalaba mikononi salini ili maovu yasiwatumie wala kuwashinda. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa, ninyi ni nguvu yangu. Ninyi, mitume wangu, ambao, kwa upendo wenu, unyenyekevu na sala ya kimya kimya, mnamwezesha Mwanangu ajulikane. Ninyi mnaishi ndani yangu. Ninyi mnanibeba mioyoni mwenu. Ninyi mnajua ya kuwa mna Mama awapendaye na aliyekuja kuwaletea upendo. Nawatazama katika Baba wa Mbinguni, natazama fikira zenu, maumivu yenu, mateso yenu na kuyaleta kwa Mwanangu. Msiogope! Msipoteze matumaini, maana Mwanangu humsikiliza Mama yake. Yeye hupenda tangu alipozaliwa, na ndio furaha yangu ya kuwa wanangu wote wajue upendo huo; na wote wale ambao, kwa sababu ya maumivu yao na kutoelewa kwao, walimwacha waweze kurudi kwake, na wote wao wasiomjua wamjue. Kwa sababu hiyo ninyi hapa ni mitume wangu, nami pia pamoja nanyi kama Mama yenu. Salini ili kuwa imara katika imani, maana upendo na rehema hutoka katika imani imara. Kwa njia ya upendo na rehema mtawasaidia wale wote wasiofahamu ya kuwa wanachagua giza badala ya nuru. Salini kwa ajili ya wachungaji wenu, maana wao ni nguvu ya Kanisa ambayo Mwanangu aliwaachieni. Kwa njia ya Mwanangu wao ni wachungaji wa roho. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Nawaalikeni tena: anzeni kupambana na dhambi kama vile katika siku za mwanzo, nendeni kuungama dhambi zenu na kateni shauri ya kuwa watakatifu. Kwa njia yenu upendo wa Mungu utaenea ulimwenguni na amani itatawala mioyoni mwenu na baraka ya Mungu itawajaza. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombeeni mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Naja kwenu kama Mama na ninatamani kuwa kwangu kama Mama mtapata maskani, faraja na mapumziko. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, salini! Salini kwa moyo mkunjufu, utii na uaminifu kamili kwa Baba wa Mbinguni. Muwe na uaminifu, kama vile mimi pia nilivyokuwa mwaminifu nilipoambiwa ya kuwa nitachukua baraka za ahadi. Basi kutoka mioyo yenu yafike siku zote midomoni mwenu maneno haya "Utakalo lifanyike". Kwa hiyo muwe na uaminifu na salini, ili mimi niweze kuwaombeeni kwa Bwana, ili awape Baraka ya Mbinguni na kuwajaza Roho Mtakatifu. Hapo mtaweza kuwasaidia wale wote wasiomjua Bwana. Ninyi, mitume wa upendo wangu, mtawasaidia kumwita "Baba" kwa uaminifu wote. Salini kwa ajili ya wachungaji wenu na mujiaminishe katika mikono yao iliyobarikiwa. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`