Monthly Medjugorje Messages - Karibuni of year 2014

Wanangu wapendwa! Leo kwa namna ya pekee nawaalikeni msali. Salini, wanangu, ili muweze kutambua ninyi ni akina nani na ni wapi mnayopaswa kwenda. Muwe watangazaji wa Habari Njema na watu wa matumaini. Muwe upendo kwa wale wote wasio na upendo. Wanangu, mtakuwa yote na kuyatimiza yote iwapo tu mkisali na mkiwa tayari kupokea mapenzi ya Mungu, Mungu ambaye anatamani kuwaongoza katika maisha ya uzima wa milele. Mimi nipo pamoja nanyi na siku hata siku ninawaombeeni kwa Mwanangu Yesu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Salini katika kipindi hiki cha neema na ombeni maombezi ya Watakatifu wote ambao wapo tayari katika mwanga. Wao wawe mfano na kichocheo kwenu siku hata siku, katika njia ya uwongofu wenu. Wanangu, mfahamu ya kuwa maisha yenu ni mafupi na ya kupita upesi. Kwa hiyo tamanini uzima wa milele na mtayarishe mioyo yenu katika sala. Mimi nipo pamoja nanyi na ninamwomba Mwanangu kwa ajili ya kila mmoja wenu, hasa kwa wale waliojiweka wakfu kwangu na kwa Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Leo pia nawaalika ili ninyi muwe kama nyota ambazo kwa mwangaza wake zinatoa nuru na uzuri kwa watu ili wafurahishwe. Wanangu, ninyi pia muwe nuru, uzuri, furaha na amani na hasa sala kwa wale wote walio mbali na upendo wangu na upendo wa Mwanangu Yesu. Wanangu, ishuhudieni imani yenu na sala yenu katika furaha, katika furaha iliyo mioyoni mwenu na salini kwa ajili ya amani iliyo thawabu bora ya Mungu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Salini kwa nia zangu maana Shetani ataka kuangamiza mpango wangu nilio nao hapa na kuwaibia amani: Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini ili Mungu aweze kutenda kazi kwa njia ya kila mmoja wenu. Mioyo yenu iwe wazi kupokea mapenzi ya Mungu. Mimi nawapendeni na kubariki kwa baraka ya kimama. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Ninyi hamjui neema ya namna gani mnayoishi katika wakati huu ambapo Yeye Aliye Juu awapeni ishara ili mjifungue na kutubu. Mwelekeeni Mungu na kusali; sala itawale katika mioyo yenu, familia na jamaa zenu ili Roho Mtakatifu awaongoze na kuhimiza kila siku mjifungue kufanya mapenzi ya Mungu na mpango wake kwa kila mmoja wenu. Mimi nipo pamoja nanyi, na nawaombeeni pamoja na malaika na watakatifu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Yeye Aliye Juu ananipa neema ya kuweza kuwa tena pamoja nanyi na kuwaongoza katika sala kuelekea njia ya amani. Mioyo yenu na roho zenu zina kiu ya amani na upendo, ya Mungu na ya furaha yake. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini na katika sala mtapata hekima ya kuishi. Nawabarikieni na kukuombeeni mbele ya Mwanangu Yesu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Salini na mfahamu ya kwamba pasipo Mungu ninyi ni mavumbi. Kwa hiyo geuzeni fikira zenu na mioyo yenu kwa Mungu na kwa sala. Tegemeeni upendo Wake. Katika Roho ya Mungu ninyi nyote mnaalikwa kuwa mashahidi. Ninyi mna thamani mbele ya Mungu, nami nawaalika, wanangu, kuwa watakatifu, ili mweze kupata uzima wa milele. Kwa hiyo mfahamu ya kwamba maisha haya hupita. Nawapendeni na kuwaalika kwa maisha mapya ya kutubu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Fungueni mioyo yenu kwa neema ambayo Mungu anawapa kwa njia yangu kama vile ua linalojifungua kwa miali ya joto la jua. Muwe sala na upendo kwa wale wote walio mbali na Mungu na upendo Wake. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawaombea nyote kwa Mwanangu Yesu na ninawapenda kwa upendo usio na mipaka. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Nawaalikeni tena: anzeni kupambana na dhambi kama vile katika siku za mwanzo, nendeni kuungama dhambi zenu na kateni shauri ya kuwa watakatifu. Kwa njia yenu upendo wa Mungu utaenea ulimwenguni na amani itatawala mioyoni mwenu na baraka ya Mungu itawajaza. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombeeni mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Mnaona, mnasikia na kuhisi kwamba katika mioyo ya watu wengi hakuna Mungu. Hawamtaki kwa maana wapo mbali na sala na hawana amani mioyoni. Ninyi, wanangu, salini, na isheni kadiri ya amri za Mungu. Muwe sala, enyi mlioitikia "naam" tangu mwanzo wa mwaliko wangu. Mshuhudieni Mungu na mtambue uwepo wangu wala msisahau, wanangu, ya kuwa mimi ni pamoja nanyi na ninawapenda. Siku hata siku nawachukua kwa Mwanangu Yesu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
Wanangu wapendwa! Salini, salini, salini ili mionzi ya sala yenu iwaguse watu wote mnaokutana nao. Wekeni Biblia Takatifu mahali pa kuonekana katika familia zenu, mkaisome ili maneno ya amani yatiririke ndani ya mioyo yenu. Nasali pamoja nanyi na kwa ajili yenu, wanangu, ili siku hata siku mzidi kuyapokea mapenzi ya Mungu. Asanteni kwa kuitikia mwaliko wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`