Monthly Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa, Nawaletea ninyi Mwanangu Yesu ili awabariki na kuwafunulia Upendo wake utokao mbinguni. Moyo wenu unatamani amani inayopungua zaidi na zaidi duniani. Kwa sababu hiyo watu wako mbali na Mungu, nafsi zinaumwa na zinaelekea kifo cha kiroho. Mimi nipo pamoja nanyi, wanangu, niwaongoze kwenye njia hii ya wokovu ambayo Mungu anawaiteni. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, wakati huu uwe kwenu wakati wa sala. Bila Mungu hamwezi kuwa na amani. Kwa hiyo, wanangu, salini kwa ajili ya amani katika mioyo yenu na katika familia zenu ili Yesu aweze kuzaliwa ndani yenu na kuwapeni upendo wake na baraka yake. Ulimwengu uko katika vita kwa sababu mioyo imejaa machukio na wivu. Wanangu, wasiwasi unaonekana katika macho yenu kwa sababu hamkuruhusu Yesu kuzaliwa katika maisha yenu. Mtafuteni, ombeni na Yeye atajitoa kwenu katika yule Mtoto aliye furaha na amani. Mimi niko pamoja nanyi na ninasali pamoja nanyi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Leo ninawaalika kusali. Sala iwe manukato kwa roho zenu kwani tunda la sala ni furaha, kutoa, kumshuhudia Mungu kwa wengine kwa njia ya maisha yenu. Wanangu, mkimtegemea Mungu kabisa, Yeye atashughulika yote, atawabariki na sadaka zenu zitapata maana. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Leo ninawaalika kusali kwa ajili ya makusudi yangu ili niweze kuwasaidia. Wanangu, salini Rosari mkitafakari mafumbo ya Rosari maana hata ninyi katika maisha yenu mnapitia furaha na maumivu. Kwa njia hii mtageuza mafumbo katika maisha yenu maana maisha ni fumbo hadi mtakapoyaweka katika mikono ya Mungu. Hivyo mtakuwa na mang'amuzi ya imani kama Petro aliyemkuta Yesu na Roho Mtakatifu aliyoijaza roho yake. Hata ninyi, wanangu, mnaalikwa kushuhudia mkiishi upendo ambao kwao siku kwa siku Mungu anawajaza kwa njia ya uwepo wangu. Kwa hiyo, wanangu, muwe wazi na salini kwa moyo katika imani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Fanyeni kazi na shuhudieni kwa upendo Ufalme wa Mbinguni ili muweze kuwa hamjambo hapa duniani. Wanangu, Mungu atabariki mara mia zaidi juhudi yenu na mtakuwa mashahidi katikati ya watu, roho za wale wasioamini zitahisi neema ya wongofu na Mbingu itazipokea taabu zenu na sadaka zenu. Wanangu, shuhudieni kwa tasbihi mkononi ili muwe wangu na kateni shauri kuwa watakatifu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, mwaliko wangu kwenu ni sala. Sala iwe kwenu furaha na taji la kuwaunganisha na Mungu. Wanangu, majaribu yatakuja nanyi hamtakuwa na nguvu na dhambi itatawala lakini mkiwa wangu, mtashinda maana kimbilio lenu litakuwa Moyo wa Mwanangu Yesu. Kwa hiyo wanangu, rudieni sala ili sala iwe maisha kwenu, mchana na usiku. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Namshukuru Mungu kwa kila mmoja wenu. Hasa, wanangu, asanteni kwa kuitikia wito wangu. Mimi ninawatayarisha kwa nyakati mpya ili muwe imara katika imani na kusali daima, ili Roho Mtakatifu atende kwa njia yenu na afanye upya uso wa nchi. Ninasali pamoja nanyi kwa amani, karama ya thamani kuliko zote, hata ingawa shetani hutaka vita na machukio. Ninyi, wanangu, muwe mikono yangu inayonyoshwa na tembeeni katika kujivunia pamoja na Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Mungu kwa rehema yake alinijalia kuwa pamoja nanyi, ili kuwaelimisha na kuwaongoza kuelekea katika hatua ya wongofu. Wanangu, ninyi nyote mmeitwa kusali kwa moyo wenu wote ili mpango wa wokovu utimilike ndani mwenu na kwa njia yenu. Jueni wanangu, kwamba maisha ni mafupi na uzima wa milele unawangoja kwa kadiri ya mastahili yenu. Kwa hiyo salini, salini, salini ili muweze kuwa vyombo vya kufaa mikononi mwa Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Wakati huu ndio wakati wa neema, wakati wa rehema kwa kila mmoja wenu. Wanangu, msiruhusu upepo wa chukio na hofu utawale ndani yenu na karibu nanyi. Ninyi, wanangu, mmealikwa kuwa upendo na sala. Ibilisi ataka hofu na fujo lakini ninyi, wanangu, muwe furaha ya Yesu Mfufuka ambaye amekufa na kufufuka kwa ajili ya kila mmoja wenu. Yeye ameshinda kifo kwa kuwapeni uzima, uzima wa milele. Kwa hiyo, wanangu, mshuhudieni na muwe wenye fahari kwa kufufuliwa katika Yeye. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Wakati huu ndio wakati wa neema. Kama vile maumbile huhuisha kwa maisha mapya nanyi pia mnaalikwa kugeuka. Kateni shauri kwa ajili ya Mungu. Wanangu, ninyi ni watupu wala hamna furaha maana hamko na Mungu. Kwa hiyo salini ili sala iwe maisha kwenu. Maporini mtafuteni Mungu aliyewaumbeni maana mapori ya asili yanaongea na kupigana kwa ajili ya maisha wala si kwa ajili ya kifo. Vita vinatawala katika mioyo yenu na katika watu maana hamna amani na wala hamuoni, wanangu, ndugu yenu ndani ya jirani yako. Kwa hiyo mrudieni Mungu na kusali. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Leo ninawaalika kwa maisha mapya. Haijalishi miaka yenu ni mingapi, fumbueni mioyo yenu kwa Yesu ambaye atawabadilisha katika wakati huu wa neema nanyi, kama nyasi, mtazaliwa katika maisha mapya katika upendo wa Mungu na mtafumbua mioyo yenu kwa Mbinguni na kwa vitu vya kimbingu. Mimi nipo bado pamoja nanyi maana Mungu aliniruhusu kwa ajili yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! kama mama ninawaalika kutubu. Wakati huu ni kwenu, wanangu, wakati wa ukimya na sala. Kwa hiyo, katika joto la moyo wenu iote chembe ya tumaini na imani na hivyo, ninyi nanyi, wanangu, siku kwa siku mtasikia haja ya kusali zaidi. Maisha yenu yatakuwa ya mpangilio na yenye kuwajibika. Mtaelewa, wanangu, ya kuwa sisi ni wa kupita hapa duniani na ya kuwa mtasikia haja ya kuwa karibu zaidi na Mungu na kwa upendo mtatoa ushuhuda wa mang'amuzi yenu ya kukutana na Mungu, mtakaoushirikisha pamoja na wengine. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawaombeeni, lakini siwezi kufanya hivyo bila 'Ndiyo' yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`