Our Lady of Medjugorje Messages containing 'maombi'

Total found: 17
Wanangu wapendwa, nawashukuru kwa kuitikia miito yangu na kukusanyika karibu nami, Mama yenu wa mbinguni. Najua kwamba mnanifikiri kwa upendo na matumaini. Mimi ninawapendeni nyote kama vile anavyowapendeni Mwanangu ambaye, kwa upendo wake wenye huruma, ananituma nije kwenu, mara nyingi pia. Yeye, aliyekuwa mtu na aliye Mungu, Mmoja na Utatu; Yeye aliyeteswa kwa ajili yenu mwilini na nafsini. Yeye aliyejifanya Mkate ailishe nafsi zenu na hivyo kuziokoa. Wanangu, nawafundisha jinsi ya kustahili upendo wake, kumwelekeza mawazo yenu, kumwishi Mwanangu. Mitume wa upendo wangu, ninawafunika kwa joho langu kwa sababu, kama Mama yenu, nataka kuwalinda. Nawasihi: mwuombee ulimwengu wote: moyo wangu unateswa. Dhambi zinaongezeka, ni nyingi mno. Lakini kwa msaada wenu – mlio wanyenyekevu, wanyofu, wenye upendo, watawa na watakatifu – moyo wangu utashinda. Mpendeni Mwanangu kupita wote na ulimwengu wote kwa njia yake. Msisahau kabisa ya kuwa kila ndugu yenu ana ndani yake kitu cha thamani: nafsi. Kwa hiyo, wanangu, pendeni wale wote wasiomjua Mwanangu ili kwa njia ya maombi na upendo utokao katika maombi, wawe wema zaidi. Ili wema uweze kushinda ndani yao. Ili nafsi zao ziweze kuokoka na kupata uzima wa milele. Enyi mitume wangu, wanangu. Mwanangu aliwaambieni mpendane. Hiyo iandikwe mioyoni mwenu na kwa kusali jaribuni kuishi upendo huu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninawaelekea ninyi kama Mama yenu, Mama wa wenye haki, Mama wa wale wanaopenda na kuteseka, Mama wa watakatifu. Wanangu, ninyi pia mnaweza kuwa watakatifu: ni juu yenu. Watakatifu ni wale wanaompenda Baba wa Mbinguni kupita kiasi, wale wanaompenda kupita chochote. Kwa hivyo, wanangu, jaribuni daima kuboreka. Kama ninyi mnajaribu kuwa wema, mtaweza kuwa watakatifu, hata kama hamfikiri hiyo juu yenu. Kama mnafikiri kuwa wema, ninyi sio wanyenyekevu na kiburi huwatenga kutoka utakatifu. Katika ulimwengu huu wa wasiwasi, umejaa vitisho, mikono yako, mitume wa upendo wangu, inapaswa kuwa imenyoshwa katika maombi na rehema. Kwangu, wanangu, nipeni zawadi ya Rozari, mawaridi ninayopenda sana! Mawaridi yangu ni maombi yenu msemayo kwa moyo wote, na sio yale msemayo kwa midomo yenu tu. Mawaridi yangu ni matendo yenu ya maombi, imani na upendo. Wakati alipokuwa mtoto, mwanangu aliniambia kwamba watoto wangu watakuwa wengi na wataniletea mawaridi mengi. Sikuelewa, sasa najua kwamba ninyi ni watoto wale, wanaoniletea mawaridi wakati mnapompenda mwanangu kupita yote, wakati mnaposali kwa moyo wote, wakati mnapowasaidia walio maskini zaidi. Hayo ndiyo mawaridi yangu! Hii ndiyo imani, inayosababisha kila kitu katika maisha kifanyike kwa upendo; na kiburi hakijulikani; na muwe tayari daima, kusamehe upesi, bila kuhukumu na daima mjaribu kuelewa ndugu yako. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, muwaombeeni wale wasiojua kupenda, wale wasiowapenda, wale waliowatenda mabaya, wale ambao hawakujua upendo wa Mwanangu. Wanangu, ninawaomba haya, kwa sababu kumbukeni: kuomba maana yake ni kupenda na kusamehe. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, moyo safi na wazi tu utawawezesha ninyi kumjua kweli Mwanangu, na wale wote wasiojua upendo wake kuujua kwa njia yenu. Upendo tu utawawezesha kuelewa kuwa ni wenye nguvu kuliko kifo, maana upendo wa kweli umeshinda kifo na umefanya hata kifo hakipo tena. Wanangu, msamaha ni mtindo bora wa upendo. Ninyi, kama mitume wa upendo wangu, yawapasa kusali kwa kuwa wenye nguvu katika roho na kuweza kuelewa na kusamehe. Ninyi, mitume wa upendo wangu, kwa njia ya ufahamu na msamaha, mnatoa mfano wa upendo na rehema. Kuweza kuelewa na kusamehe ni karama inayotokana na maombi na yatupasa kuitunza. Mkisamehe ninyi mnaonyesha ya kuwa mnajua kupenda. Tazameni, wanangu, kama Baba wa mbinguni anavyowapenda kwa upendo mkubwa, kwa ufahamu, kwa uelewa, msamaha na haki. Kama anavyowatolea mimi, Mama wa mioyo yenu. Na tazama: mimi nipo katikati yenu ili kuwabariki kwa baraka ya kimama; ili kuwaalika kusali na kufunga; ili kuwasihi kuamini, kutumaini, kusamehe, kuwaombea wachungaji wenu na hasa kupenda bila mipaka. Wanangu, nifuateni! Njia yangu ni njia ya amani na upendo, njia ya Mwanangu. Ndiyo njia ya kuongoza katika ushindi wa Moyo wangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, katika miaka hii yote mimi nipo pamoja nanyi ili kuwaongoza kwenye njia ya wokovu. Rudieni kwa Mwanangu, rudieni katika sala na mfungo. Wanangu, mwachieni Mungu aongee na mioyo yenu kwa sababu shetani anatawala na anatamani kuangamiza maisha yenu na dunia mnamotembelea. Muwe na ujasiri na amueni kuwa watakatifu. Mtaona wongofu katika mioyo yenu na katika familia zenu, sala itasikilizwa, Mungu atayapokea maombi yenu na kuwapa amani. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ninasikiliza maombi yenu na sala zenu na ninawaombea kwa mwanangu Yesu aliye njia, kweli na uzima. Wanangu, rudieni kusali na fungueni mioyo yenu katika wakati huu wa neema na shikeni njia ya wongofu. Maisha yenu yanapita na hayana maana bila Mungu. Kwa hiyo mimi ni pamoja nanyi niwaongoze kuelekea utakatifu wa maisha ili kila mmoja wenu agundue furaha ya kuishi. Wanangu, ninawapenda wote na kuwabariki kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Mimi ni pamoja nanyi kwa muda mrefu kwa maana Mungu ni mkuu katika upendo wake na katika uwepo wangu. Wanangu, ninawaalika kurudi kwa Mungu na kwa sala. Kipimo cha kuishi kwenu kiwe upendo na msisahau, wanangu, kwamba maombi na kufunga hufanya miujiza ndani yenu na kuwazunguka. Yote mnayoyafanya yawe kwa ajili ya utukufu wa Mungu na hapo Mbingu itajaza moyo wenu na furaha mkahisi ya kuwa Mungu anawapenda na kunituma ili kuokoa ninyi na Dunia ambayo juu yake mnaishi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Nipo pamoja nanyi na tusali pamoja. Wanangu nisaidieni kwa maombi ili shetani asishinde. Nguvu yake ya mauti, chuki na woga imeitembelea Dunia. Kwa hiyo wanangu, mrudieni Mungu katika maombi na katika kufunga na kuwanyima kwa ajili ya wote waliokanyagwa, maskini na wasio na sauti katika dunia hii pasipo Mungu. Watoto wadogo, msipomrudia Mungu na amri zake, hamna wakati ujao. Kwa hiyo amenituma kwenu ili niwaongoze. Leo ninawaalika mrudi kwenye sala ya kibinafsi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ninasikiliza kilio chenu na maombi ya amani. Shetani amekuwa akipigania vita kwa miaka mingi. Kwa hiyo Mungu amenituma kati yenu ili niwaongoze katika njia ya utakatifu, kwa sababu ubinadamu uko kwenye njia panda. Nawaalikeni: mrudieni Mungu na amri za Mungu mkae vizuri hapa duniani na mtoke katika janga hili ambalo mmeingia kwa sababu humsikii Mungu anayewapenda na anayetaka kuwaokoa na kuwaongoza kuelekea maisha mapya. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ninawatazama na ninamshukuru Mungu kwa kila mmoja wenu, kwa sababu ameniruhusu niwe nanyi tena ili kuwasihi katika utakatifu. Wanangu amani inavurugika na shetani anataka mahangaiko. Kwa hiyo maombi yenu yawe na nguvu zaidi ili kila roho chafu ya utengano na vita itulie. Iweni wajenzi wa amani na wachukuaji wa Aliyefufuka ndani yenu na karibu nanyi ili mema yapate kushinda katika kila mtu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ongokeni na mvae mavazi ya toba na maombi ya kina ya kibinafsi na kwa unyenyekevu mwombe Aliye Juu amani. Katika wakati huu wa neema Shetani anataka kuwapotosha ninyi, nanyi wanangu, mwangalieni Mwanangu na kumfuata kuelekea Kalvari, kwa kujikana na kufunga. Niko pamoja nanyi kwa sababu Aliye Juu ameniruhusu niwapende ninyi na kuwaongoza kuelekea furaha ya moyo, katika imani inayokua ndani ya wale wote wanaompenda Mungu zaidi ya vitu vyote. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ninawaalika ninyi nyote kuwa waletaji wa amani na furaha ya Yesu Mfufuka kwa wale wote walio mbali na maombi ili kwa njia ya maisha yenu, upendo wa Yesu uwabadilishe na kuwa katika maisha mapya, maisha ya wongofu na utakatifu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Aliye Juu ameniruhusu niwe miongoni mwenu, niwaombee, niwe Mama yenu na kimbilio lenu. Ninawaalika wanangu, mrudieni Mungu na kwenye maombi na Mungu atawabariki kwa wingi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema ninawaalika ninyi kwenye maombi kwa moyo. Mioyo yenu, wanangu, igeuzwe kuelekea mbinguni kwa maombi, ili mioyo yenu ipate kuhisi Mungu wa upendo anayewaponya na kuwapenda kwa upendo mkuu. Mimi niko pamoja nanyi kuwaongoza kwenye njia ya uongofu wa moyo. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ninawaalika kwenye maombi ya nguvu. Umamboleo unataka kuingia katika mawazo yenu na kuwaibia furaha ya maombi na kukutana na Yesu. Kwa hiyo, wanangu wapendwa, fanyeni upya sala katika familia zenu ili moyo wangu wa kimama ufurahi kama siku za kwanza nilipowachagua ninyi na jibu lilikuwa ni maombi mchana na usiku na mbingu haikunyamaza bali ilitolea kwa mahali hapa neema, amani na baraka kwa wingi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ninawaletea Mwanangu ili aijaze mioyo yenu amani kwa sababu Yeye ni amani. Wanangu, mtafuteni Yesu katika ukimya wa mioyo yenu ili azaliwe upya. Ulimwengu unamhitaji Yesu, hivyo wanangu, mtafuteni kwa maombi maana anajitoa kila siku kwa kila mmoja wenu.
Mama yetu alikuja leo akiwa amevalia mavazi ya heshima akiwa na mtoto Yesu mikononi mwake. Yesu alinyoosha mkono wake kama ishara ya baraka na Mama yetu alituombea kwa lugha ya aramaika.
Wanangu wapendwa! Wakati huu uwe wakati wa maombi.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema, ombeni pamoja nami ili mema yapate kushinda ndani yenu na karibu nanyi. Hasa, wanangu, ombeni kwa umoja na Yesu katika njia yake ya msalaba. Wekeni katika maombi yenu ubinadamu huu unaotangatanga bila Mungu na bila upendo wake. Muwe maombi, muwe mwanga na mashahidi kwa wale wote mnaokutana nao, enyi wanangu, ili Mungu wa rehema awarehemu.. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`