Our Lady of Medjugorje Messages by month Oktoba

Wanangu wapendwa! Pepo za uovu, chuki na wasiwasi huvuma duniani kote kuharibu maisha yote. Kwa hiyo Aliye Juu amenituma kwenu ili niwaongoze kwenye njia ya amani na ushirika na Mungu na wanadamu. Ninyi, wanangu, ni mikono yangu iliyopanuliwa: ombeni, mfunge na toeni sadaka kwa ajili ya amani, hazina ambayo kila moyo unatamani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Aliye juu aliniruhusu niwe pamoja nanyi; kuwa furaha kwenu na njia katika matumaini kwa sababu ubinadamu umeamua kifo. Kwa hiyo amenituma niwaelekeze kwamba bila Mungu hamna wakati ujao. Wanangu, muwe vyombo vya upendo kwa wale wote ambao hawajamjua Mungu wa upendo. Kwa furaha toeni ushuhuda wa imani yenu na msipoteze matumaini katika mabadiliko ya moyo wa mwanadamu. Niko pamoja nanyi na ninawabariki kwa baraka yangu ya mama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Rudieni kusali maana wanaosali hawaogopi wakati ujao. Wale wanaosali wako wazi kwa uzima na wanaheshimu maisha ya wengine. Yeyote anayesali, wanangu, anahisi uhuru wa wana wa Mungu na kwa moyo wa furaha hutumikia kwa manufaa ya ndugu yake. Kwa sababu Mungu ni upendo na uhuru. Kwa hiyo, wanangu, wanapotaka kuwafunga kwa minyororo na kuwatumia hilo halitoki kwa Mungu maana Mungu ni upendo na humpa kila kiumbe amani yake. Kwa hiyo amenituma niwasaidie ninyi kukua katika njia ya utakatifu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu ninawaita kumrudia Mungu na sala. Waiteni watakatifu wote wawasaidie ili wawe mfano na msaada kwenu. Shetani ni mwenye nguvu na anapigania kuivutia kwake mioyo mingi zaidi awezavyo. Anataka vita na chuki. Kwa sababu hiyo Mimi ni pamoja nanyi muda mrefu ili niwaongoze kwenye njia ya wokovu, kwa Yule aliye njia, kweli na uzima. Wanangu, rudini kwa upendo kumwelekea Mungu naye atakuwa nguvu yenu na kimbilio lenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Leo ninawaalika kusali. Sala iwe manukato kwa roho zenu kwani tunda la sala ni furaha, kutoa, kumshuhudia Mungu kwa wengine kwa njia ya maisha yenu. Wanangu, mkimtegemea Mungu kabisa, Yeye atashughulika yote, atawabariki na sadaka zenu zitapata maana. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, mapenzi na upendo wa Baba wa mbinguni hufanya mimi niwe katikati yenu, ili kusaidia kwa upendo wa kimama ukuaji wa imani katika mioyo yenu, ili kwamba muweze hakika kuelewa lengo la maisha ya kidunia na ukuu wa yale ya kimbingu. Wanangu, maisha ya kidunia ndiyo njia kuelekea umilele, kuelekea ukweli na uzima: kuelekea kwa Mwanangu. Kwa njia hii nataka kuwaongoza. Ninyi, wanangu, ninyi wenye sikuzote kiu ya upendo mkubwa zaidi, ukweli na imani, mjue ya kuwa moja tu ni chemchemi mnakoweza kunywa: imani katika Baba wa mbinguni, imani katika upendo wake. Mtegemee kabisa mapenzi yake wala msiogope: kila lililo bora kwa ajili yenu, kila linalowachukua kwenye uzima wa milele, mtapewa! Mtaelewa ya kuwa lengo la maisha si sikuzote kutaka na kutwaa, lakini kupenda na kutoa; mtakuwa na amani ya kweli na upendo wa kweli, mtakuwa mitume wa upendo. Kwa mfano wenu, mtawafanya wale wanangu wasiomjua Mwanangu na upendo wake watake kumjua. Wanangu, mitume wa upendo wangu, mwabuduni Mwanangu pamoja nami, na mpendeni juu ya vyote. Jaribuni sikuzote kuishi katika ukweli wake. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa! Ninyi mna neema kubwa ya kuitwa kwa maisha mapya kwa njia ya ujumbe ninaowapeni. Wanangu, huu ni wakati wa neema, wakati na wiko kwa wongofu wenu na kwa vizazi vya wakati ujao. Kwa hiyo ninawaalika, wanangu, kusali zaidi na kumfunulia Mwanangu Yesu moyo wenu. Mimi nipo pamoja nanyi, ninawapenda wote na kubariki kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu, ninawaomba kuwa hodari wala kutowayawaya, maana hata mema madogo zaidi, ishara ya upendo mdogo zaidi hushinda maovu yanayoonekana zaidi na zaidi. Wanangu nisikilizeni ili mema yashinde, ili muweze kujua upendo wa Mwanangu ulio furaha mkubwa zaidi kuliko zote. Mikono ya mwanangu inawakumbatia, Yeye, apendaye nafsi, Yeye ambaye amejitolea kwa ajili yenu na kunajitolea sikuzote tena katika Ekaristi, Yeye aliye na maneno ya Uzima wa milele; kujua upendo wake, kufuata hatua zake, maana yake ni kuwa na mali ya kiroho. Huo ni utajiri unaojaza hisia iliyo njema, na unaoona upendo na mema popote. Mitume wa upendo wangu, wanangu, muwe kama mionzi ya jua ambayo kwa joto la upendo wa Mwanangu inawapasha joto wote wale wanaoizunguka. Wanangu, ulimwengu unahitaji mitume wa upendo, ulimwengu unahitaji sala nyingi, lakini sala zinazosaliwa kwa moyo na roho, si kwa midomo tu. Wanangu, muwe na hamu ya utakatifu mkiwa na unyenyekevu unaomwezesha Mwanangu kufanya kazi kwa njia yenu, kama Yeye apendavyo. Wanangu, sala zenu, fikira zenu na matendo yenu, haya yote yawafungulia ama kuwafungia mlango wa Ufalme wa Mbinguni. Mwanangu aliwaonyesha njia na kuwapa tumaini, mimi ninawafariji na kuwapa moyo maana, wanangu, mimi nilijua maumivu, lakini nilikuwa na imani na tumaini, sasa nimepata thawabu ya uzima katika Ufalme wa Mwanangu. Kwa hiyo, nisikilizeni, jipeni moyo, msiwayawaye. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Katika kipindi hiki cha neema ninawaalika kuwa sala. Wote mna matatizo, taabu, maumivu na wasiwasi. Watakatifu wawe kwenu mfano na onyo kwa utakatifu, Mungu atakuwa karibu nanyi na mtakuwa wapya kwa utafiti na wongofu wa binafsi. Imani itakuwa kwenu tumaini, na furaha itazaliwa katika mioyo yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ninaongea nanyi kama Mama, kwa maneno rahisi, lakini yamejaa wingi wa upendo na wa bidii kwa wanangu, ambao kwa njia ya Mwanangu wamekabidhiwa kwangu. Mwanangu, ambaye anakuja kutoka umilele na hata sasa, anaongea nanyi kwa maneno ya uzima na anapanda upendo katika mioyo wazi. Kwa hiyo nawaomba, mitume wa upendo wangu: muwe na mioyo iliyo wazi sikuzote kurehemu na kusamehe. Wasameheni sikuzote wenzenu kama Mwanangu, kwa vile hivyo amani itakuwa ndani yenu. Wanangu, lindeni nafsi yenu, maana hiyo ndiyo ukweli wa pekee ulio wenu bila shaka. Mmeanza kusahau umuhimu wa familia. Familia haipaswi kuwa mahali pa mateso na maumivu, bali mahali pa uelewano na huruma. Familia wanaojaribu kuishi kama apendavyo Mwanangu, wanaishi wakipendana. Tangu alipokuwa angali mtoto, Mwanangu aliniambia ya kuwa watu wote kwake ni ndugu zake. Kwa hiyo kumbukeni, enyi mitume wa upendo wangu, watu wote mnaowaona ni kwenu familia yenu, ndugu kama apendavyo Mwanangu. Wanangu, msipoteze muda kufikiria na kuhangaikia mambo yajayo. Kitu chenu kimoja cha kuhangaikia kwenu kiwe vipi kuishi vema kila dakika kadiri ya Mwanangu, na tazama hiyo ndiyo ni amani! Wanangu, msisahau kabisa kuwaombea wachungaji wenu. Salini ili waweze kupokea watu wote kama wanao, ili, kama apendavyo Mwanangu, wawe kwao kama baba za kiroho. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose
1 2 Next>>

For God to live in your hearts, you must love.

`