Our Lady of Medjugorje Messages containing 'mpendane'

Total found: 4
Wanangu wapendwa, nawashukuru kwa kuitikia miito yangu na kukusanyika karibu nami, Mama yenu wa mbinguni. Najua kwamba mnanifikiri kwa upendo na matumaini. Mimi ninawapendeni nyote kama vile anavyowapendeni Mwanangu ambaye, kwa upendo wake wenye huruma, ananituma nije kwenu, mara nyingi pia. Yeye, aliyekuwa mtu na aliye Mungu, Mmoja na Utatu; Yeye aliyeteswa kwa ajili yenu mwilini na nafsini. Yeye aliyejifanya Mkate ailishe nafsi zenu na hivyo kuziokoa. Wanangu, nawafundisha jinsi ya kustahili upendo wake, kumwelekeza mawazo yenu, kumwishi Mwanangu. Mitume wa upendo wangu, ninawafunika kwa joho langu kwa sababu, kama Mama yenu, nataka kuwalinda. Nawasihi: mwuombee ulimwengu wote: moyo wangu unateswa. Dhambi zinaongezeka, ni nyingi mno. Lakini kwa msaada wenu – mlio wanyenyekevu, wanyofu, wenye upendo, watawa na watakatifu – moyo wangu utashinda. Mpendeni Mwanangu kupita wote na ulimwengu wote kwa njia yake. Msisahau kabisa ya kuwa kila ndugu yenu ana ndani yake kitu cha thamani: nafsi. Kwa hiyo, wanangu, pendeni wale wote wasiomjua Mwanangu ili kwa njia ya maombi na upendo utokao katika maombi, wawe wema zaidi. Ili wema uweze kushinda ndani yao. Ili nafsi zao ziweze kuokoka na kupata uzima wa milele. Enyi mitume wangu, wanangu. Mwanangu aliwaambieni mpendane. Hiyo iandikwe mioyoni mwenu na kwa kusali jaribuni kuishi upendo huu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nikiwatazama hapa mmekusanyika kunizunguka, Mama yenu, ninaona nafsi safi nyingi. Ninawaona wanangu wengi wanaotafuta upendo na faraja lakini hakuna mtu anayewapa. Ninawaona hata wale wanaotenda mabaya maana hawana mifano myema, maana hawajamjua mwanangu. Mwanangu anawatuma ninyi kwangu, Mama, sawa kwa wote, niwafundisheni kupenda, ili muelewe ya kuwa ninyi ni ndugu. Ninatamani kuwasaidia. Mitume wa upendo wangu, kwa mwanangu yamtosha tamaa hai ya imani na upendo na atayakubali, lakini mnapaswa kustahili, kuwa na tamaa na mioyo wazi, Mwanangu huingia katika mioyo wazi. Mimi kama Mama ninatamani kwamba mjue Mwanangu katika kweli: Mungu aliyezaliwa na Mungu, kwamba mjue ukuu wa Upendo wake, ambao mnahitaji. Yeye amezichukua juu yake dhambi zenu, ameupata Ukombozi wenu, na badala yake anaomba mpendane ninyi kwa ninyi. Mwanangu ni upendo, Yeye anawapenda watu wote bila tofauti, watu wote wa nchi zote, wa mataifa yote. Ikiwa ninyi, wanangu, mngeishi upendo wa Mwanangu, ufalme wake ungekwisha kuwa duniani. Kwa hiyo, Mitume wa upendo wangu, salini, salini ili Mwanangu na upendo wake wawe ndani yenu nanyi muweze kuwa mfano wa upendo na muweze kuwasaidia wote wale ambao hawajamjua Mwanangu. Msisahau kamwe kwamba Mwanangu, mmoja na utatu, anawapendeni. Pendeni na wombeeni wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, wakati duniani upendo unapopunguka, wakati njia ya wokovu haipatikani, Mimi, Mama yenu, naja kuwasaidieni kujua imani ya kweli, iliyo hai na ya kina, na kuwasaidieni kupenda kabisa. Kama Mama ninatamani mpendane, muwe wema na safi. Ni hamu yangu muwe wenye haki na mpendane. Wanangu, muwe wafurahivu rohoni, muwe safi, muwe watoto. Mwanangu alisema kwamba anapenda kukaa kati ya wenye mioyo safi, maana wenye mioyo safi ni daima vijana na wafurahivu. Mwanangu aliwaambieni msameheane na mpendane. Najua kwamba si rahisi sikuzote. Mateso husababisha kukua rohoni. Ili kukua rohoni kadiri iwezekanavyo, lazima msamehe na kupenda kwa dhati na kwa kweli. Wana wangu wengi duniani hawamjui Mwanangu, hawampendi. Lakini ninyi mnaompenda Mwanangu na kumchukua moyoni salini, salini, na mkisali mumhisi Mwanangu karibu yenu. Nafsi yenu ipumue Roho yake! Mimi nipo kati yenu na kuongea juu ya mambo madogo na makubwa. Sitachoka kuwasimulieni habari ya Mwanangu, aliye upendo wa kweli. Kwa hiyo, wanangu, nifungulieni mioyo yenu, acheni niwaongoze kama mama. Muwe mitume wa upendo wa Mwanangu na wangu. Kama Mama nawasihi: msisahau wale walioitwa na Mwanangu wawaongoze. Wachukueni moyoni na muwaombee. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, inasikitisha kwamba katikati yenu, wanangu, yapo mashindano mengi, chuki, masilahi yenu wenyewe na ubinafsi. Wanangu, hivi kwa urahisi mnamsahau Mwanangu, maneno Yake na upendo Wake. Imani inazimika katika roho nyingi na mioyo imetekwa na vitu vya ulimwenguni. Lakini moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa katikati yenu kuna wale wanaoamini na kupenda, wale ambao wanajaribu kumkaribia Mwanangu zaidi na zaidi, ambao wanamtafuta bila kuchoka na namna hii, wananitafuta hata mimi. Hawa ndio wanyenyekevu na wapole ambao, pamoja na maumivu na mateso wanayoyachukua katika kimya, pamoja na tumaini lao na hasa pamoja na imani yao, ni mitume wa upendo wangu. Wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawafundisha ya kuwa Mwanangu hatafuti sala tu pasipo kuchoka bali hata matendo na hisia. Salini ili katika sala mpate kuzidi katika imani na katika upendo. Mpendane wenyewe kwa wenyewe: hilo ndilo analotaka Yeye, hiyo ndiyo ni njia ya uzima wa milele. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu ameleta mwanga kwa ulimwengu huu. Ameuleta kwa wale ambao walitaka kuuona na kuupokea. Hawa muwe ninyi, maana huu ndio mwanga wa ukweli, wa amani na wa upendo. Mimi ninawaongoza kama mama kumwabudu Mwanangu, kumpenda pamoja nami. Fikira zenu, maneno na matendo yenu yamwelekee Mwanangu, yawe katika jina Lake: hapo tu moyo wangu utajazwa. Nawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`