Our Lady of Medjugorje Messages containing 'sauti'

Total found: 5
Wanangu wapendwa, Roho Mtakatifu, kwa njia ya Baba wa Mbinguni, amenifanya Mama: Mama wa Yesu na, kwa hiyo, Mama yenu vilivile. Kwa hiyo nawajilia niwasikilize, niwafungulie mikono yangu ya kimama, niwapeni Moyo wangu na kuwaalika kukaa pamoja nami, kwa maana kutoka juu ya msalaba Mwanangu amenikabidhi ninyi. Kwa bahati mbaya wanangu wengi hawakujua upendo wa Mwanangu, wengi hawataka kumjua. Loo, wanangu, mabaya mengi yatoka kwa wale ambao hawana budi ya kuona na kuelewa ili kuamini! Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, katika kimya ya moyo wenu sikilizeni sauti ya Mwanangu, ili moyo wenu uwe makazi yake wala usiwe giza na huzuni, bali uangaziwe na mwanga wa Mwanangu. Tafuteni matumaini kwa imani, maana imani ni maisha ya roho. Ninawaalika tena: salini! Salini ili kuishi imani katika unyenyekevu, katika amani ya kiroho na mkiangaziwa na mwanga. Wanangu, msijaribu kuelewa yote mara moja, maana Mimi nami sikuelewa yote mara moja, lakini niliyaamini maneno ya kimungu aliyoyasema Mwanangu, Yeye aliyekuwa mwanga wa kwanza na mwanzo wa Ukombozi. Enyi mitume wa moyo wangu, ninyi mnaosali, mnaojitolea, mnaopenda wala msiohukumu: ninyi nendeni mkaeneze ukweli, maneno ya Mwanangu, Injili. Ninyi kweli, ni Injili iliyo hai, ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu. Mwanangu na mimi tutakuwa karibu nanyi, tutawatia moyo na kuwajaribu. Wanangu, ombeeni daima na hasa baraka ya wale ambao Mwanangu amebariki mikono yao, yaani Wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, kwa mapenzi ya Baba wa mbinguni, kama Mama wa Yule anayewapendeni, nipo hapa pamoja nanyi niwasaidieni kumjua, kumfuata. Mwanangu amewaachieni nyayo za hatua zake, ili iwe rahisi zaidi kwenu kumfuata. Msiogope, msiwe na wasiwasi. Mimi nipo pamoja nanyi! Msichoke, maana sala nyingi na sadaka zinahitajiwa kuwasaidia wale wasiomwomba, wasiompenda na wasiomjua Mwanangu. Muwasaidie mkiona ndani yao ndugu zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, sikilizeni sauti yangu ndani yenu, hisieni upendo wangu. Kwa hiyo salini: salini mkitenda, salini mkitoa. Salini kwa upendo, salini kwa matendo na kwa fikira, kwa jina la Mwanangu. Kadiri mtakavyotoa upendo, ndivyo mtakavyoupokea. Upendo utokao katika Upendo huangaza ulimwengu. Ukombozi ni upendo, na upendo hauna mwisho. Wakati Mwanangu atakapokuja tena duniani, atatafuta upendo katika mioyo yenu. Wanangu, Yeye alifanya kwa ajili yenu matendo mengi ya upendo. Ninawafundisha kuyaona, kuyaelewa na kumshukuru mkimpenda na kumsamehe sikuzote na tena jirani yako. Kwa kuwa kumpenda Mwanangu maana yake ni kusamehe. Mwanangu hapendwi, ikiwa hatuwezi kumsamehe jirani yetu, ikiwa hatuwezi kumwelewa jirani yetu, ikiwa tunamhukumu. Wanangu, faida gani kusali, msipopenda wala msiposamehe? Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, ninyi ambao Mwanangu anawapenda, ninyi ambao mimi ninawapenda, msiruhusu ubinafsi, kujipenda wenyewe, zitawale duniani. Msiache upendo na wema zifichwe. Ninyi mnaopendwa, mliojua upendo wa Mwanangu, kumbukeni ya kuwa kupendwa maana yake ni kupenda. Wanangu, muwe na imani! Mnapokuwa na imani mnafurahi na mkaeneza amani, nafsi yenu inaruka kwa shangwe: katika nafsi ile yumo Mwanangu. Mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya imani, mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya upendo, mnapowafanyia watu wengine mema, Mwanangu hutabasamu katika nafsi yenu. Mitume wa upendo wangu, mimi, kama Mama, ninawaelekea, ninawakusanya kunizunguka na ninataka kuwaongozeni katika njia ya upendo na imani, katika njia ya kufika kwenye Nuru ya ulimwengu. Nipo hapa kwa upendo na kwa imani, kwa maana, kwa baraka yangu ya kimama, nataka kuwapeni matumaini na nguvu katika mwendo wenu, kwa sababu njia ya kuongoza kwa Mwanangu si rahisi: imejaa matendo ya kujinyima, ya kujitolea, ya kujidhabihu, ya kusamehe na ya upendo, upendo mwingi. Njia ile, lakini, hupata amani na furaha. Wanangu, msisadiki sauti za uongo zinazosemesha kwa maneno yasiyo na ukweli, mwanga usio wa ukweli. Ninyi wanangu rudini kwa Maandiko! Ninawaangalieni kwa upendo kupita kiasi na, kwa neema ya Mungu, ninajidhihirisha kwenu. Wanangu, njoni pamoja nami, nafsi yenu iruke kwa shangwe! Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Baba wa Mbinguni amenifanyia makuu, jinsi anavyowafanyia wale wote wanaompenda sana na kwa wema na uaminifu na wanaomtumikia kwa ibada. Wanangu, Baba wa Mbinguni anawapenda na kwa ajili ya upendo wake mimi nipo hapa pamoja nanyi. Ninasema nanyi: kwa nini hamtaki kuona ishara? Pamoja naye yote ni rahisi zaidi: hata mateso, tunayoishi pamoja naye, ni mepesi zaidi, maana kuna imani. Imani husaidia mateso, na maumivu pasipo imani huongoza katika kukata tamaa. Mateso tunayoyaishi na kuyatolea kwa Mungu, huinua mtu. Je, Mwanangu hakuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso yake makali? Mimi, kama mama yake, katika maumivu na mateso nilikaa pamoja naye, kama vile ninavyokaa pamoja nanyi. Wanangu, mimi nipo pamoja nanyi katika maisha: katika maumivu na mateso, katika furaha na upendo. Kwa hiyo muwe na matumaini: matumaini ndiyo yanayotuwezesha kuelewa ya kuwa hapa, kwenye mateso, ni uhai. Wanangu, mimi nasema nanyi; sauti yangu inasema na nafsi yenu, Moyo wangu unasema na moyo wenu: Enyi, mitume wa upendo wangu, Moyo wangu wa kimama jinsi gani unavyowapenda. Mambo haya nataka kuwafundisha. Jinsi gani Moyo wangu unataka muwe wakamilifu, lakini mtakuwa hivyo tu wakati nafsi, mwili na upendo yatakapoungana ndani yenu. Kama wanangu nawaombeni: salini sana kwa ajili ya Kanisa na kwa wahudumu wake, kwa wachungaji wenu, ili Kanisa liwe kama Mwanangu anavyolitaka: safi kama maji ya chemchemi na limejaa upendo. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Nipo pamoja nanyi na tusali pamoja. Wanangu nisaidieni kwa maombi ili shetani asishinde. Nguvu yake ya mauti, chuki na woga imeitembelea Dunia. Kwa hiyo wanangu, mrudieni Mungu katika maombi na katika kufunga na kuwanyima kwa ajili ya wote waliokanyagwa, maskini na wasio na sauti katika dunia hii pasipo Mungu. Watoto wadogo, msipomrudia Mungu na amri zake, hamna wakati ujao. Kwa hiyo amenituma kwenu ili niwaongoze. Leo ninawaalika mrudi kwenye sala ya kibinafsi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`