Our Lady of Medjugorje Messages containing 'pendeni'

Total found: 9
Wanangu wapendwa, katika wakati huu wa wasiwasi nawaalikeni tena kutembea nyuma ya Mwanangu, na kumfuata. Nayajua maumivu, mateso na taabu zenu, lakini katika Mwanangu mtapumzika, ndani yake mtapata amani na wokovu. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu amewakomboa ninyi kwa msalaba wake akawajalieni kuwa tena wana wa Mungu na kuwafundisha kumwita tena "Baba" yenu, Mungu aliye mbinguni. Ili muwe wapenzi wa Mungu Baba, basi muwe na mapendo na msamaha, kwa kuwa Baba yenu ni upendo na msamaha. Salini na fungeni, kwa maana hii ndiyo njia ya kujua na kumfahamu Baba aliye mbinguni. Mtakapomjua huyo Baba, mtafahamu ya kuwa Yeye tu ni muhimu kwenu (Maria Mtakatifu amenena hayo kwa nguvu na amkazo sana). Mimi, nikiwa Mama, nataka wanangu wawe watu wenye umoja ambamo Neno la Mungu husikilizwa na kutekelezwa. Kwa hiyo, enyi wanangu, mfuateni Mwanangu, muwe kitu kimoja naye, muwe wana wa Mungu. Pendeni wachungaji wenu kama vile Mwanangu alivyowapenda alipowaita kuwatumikia ninyi. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa, tafadhali muelewe, muwe tayari wote, kwa matumaini makuu, kufungua mioyo yenu; hivyo mngeelewa yote, mngeelewa kwa upendo gani nawaiteni, kwa upendo gani nataka kuwageuza, ili kuwafurahisha, kwa upendo gani nataka kuwafanya wafuasi wa Mwanangu na kuwapa amani katika ukamilifu wa Mwanangu. Mngeelewa ukuu wa moyo wangu wa kimama, kwa hiyo, wanangu, salini, maana kwa njia ya kusali tu imani yenu hukua na upendo wenu huzaliwa, upendo ambao utapunguza uzito wa msalaba kwa maana hamtakuwa peke yenu kuubeba. Katika umoja na Mwanangu, tukuzeni jina la Baba wa Mbinguni. Salini, salini mpate tuzo la upendo, maana upendo ni ukweli wa pekee, upendo husamehe yote, hutumikia wote na kuwaona wote kama ndugu. Enyi wanangu, mitume wangu, udhamini ambao Baba wa Mbinguni amewawekeni, kwa njia yangu, mtumishi Wake, ni kitu kikubwa, ili kusaidia wale wasiomjua, kusudi zapatanishwe naye, kusudi wamfuate, kwa hiyo nawafundisheni kupenda, maana mkiwa na upendo tu mnaweza kumjibu. Nawaalikeni tena: pendeni wachungaji wenu, salini ili katika wakati huu wa shida jina la Mwanangu atukuzwe kwa njia ya mwongozo wao. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nawapendeni, ninyi nyote, watoto wangu nyote, muwe wote moyoni mwangu, ninyi nyote mmepata upendo wangu wa kimama na ninatamani kuwaongoza nyote ili mjue furaha ya Mungu. Kwa hiyo nawaalikeni: nahitaji mitume wanyenyekevu ambao, kwa moyo mkunjufu, wanapokea Neno la Mungu na ambao wako tayari kuwasaidia watu wengine ili, kwa njia ya Neno la Mungu, waelewe maana ya maisha yao. Ili muweze kufanya hayo, wanangu, yawapasa, kwa njia ya kusali na kufunga, kusikiliza kwa moyo mkunjufu na kujifunza kujidhili au kujinyenyekesha. Yawapasa kujifunza kukataa yote yanayowatenganisha na Neno la Mungu na kutamani tu yanayowakaribisha. Msiogope, mimi nipo hapa. Ninyi si peke yenu. Namwomba Roho Mtakatifu ili awafanye wapya, ili awaimarishe. Namwomba Roho Mtakatifu, ili mkisaidia wengine, muweze kujiponya nyinyi wenyewe. Naomba ili, kwa njia yake, muwe wana wa Mungu na mitume wangu.
Kisha kwa mahangaiko makubwa Bikira Maria alisema:
Kwa ajili ya Yesu, kwa ajili ya mwanangu, pendeni wale ambao Yeye aliwaita mkitamani baraka ya mikono ile ambayo Yeye tu ameyaweka wakfu. Msiyaruhusu maovu yatawale. Nawaalikeni tena: ni kwa njia ya wachungaji wangu tu moyo wangu utashinda. Msiyaruhusu maovu yawatenganisheni na wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa! Nawaalika na kupokea ninyi nyote kama wanangu. Ninasali ili mnipokee na kunipenda kama Mama yenu. Nimewaunga ninyi nyote katika moyo wangu, nimeshuka katikati yenu na kuwabariki. Najua kwamba mnataka kwangu faraja na tumaini, kwa sababu nawapenda na kuwaombea. Nawaomba kujiunga nami katika Mwanangu na kuwa mitume wangu. Ili muweze kutenda hivyo nawaalika tena kupenda. Hakuna upendo pasipo sala, hakuna sala pasipo msamaha, maana upendo ni sala, na msamaha ni upendo. Wanangu, Mungu aliwaumba ili mpende, pendeni ili muweze kusamehe! Kila sala itokayo katika upendo huwaunganisha na Mwanangu na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu awaangaze na kuwafanya mitume wangu: mitume ambao, kila watendalo, watalifanya kwa jina la Bwana. Wao watasali kwa matendo na siyo kwa maneno tu, kwa maana wanampenda Mwanangu na kufahamu njia ya ukweli iongozayo kwenye uzima wa milele. Waombeeni wachungaji wenu, ili waweze kuwaongoza daima kwa moyo safi katika njia ya ukweli na upendo, ndiyo njia ya Mwanangu. Nawashukuru!
Wanangu wapendwa! Pendeni, salini na shuhudieni uwepo wangu kwa ajili ya wale wote walio mbali. Kwa njia ya ushuhuda wenu na mfano wenu mnaweza kuvuta mioyo iliyo mbali na Mungu na neema yake. Mimi nipo pamoja nanyi na kukuombeeni kila mmoja wenu ili kwa upendo na uhodari muweze kushuhudia na kuwahimiza wale wote walio mbali na Moyo wangu usio na doa. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, nawashukuru kwa kuitikia miito yangu na kukusanyika karibu nami, Mama yenu wa mbinguni. Najua kwamba mnanifikiri kwa upendo na matumaini. Mimi ninawapendeni nyote kama vile anavyowapendeni Mwanangu ambaye, kwa upendo wake wenye huruma, ananituma nije kwenu, mara nyingi pia. Yeye, aliyekuwa mtu na aliye Mungu, Mmoja na Utatu; Yeye aliyeteswa kwa ajili yenu mwilini na nafsini. Yeye aliyejifanya Mkate ailishe nafsi zenu na hivyo kuziokoa. Wanangu, nawafundisha jinsi ya kustahili upendo wake, kumwelekeza mawazo yenu, kumwishi Mwanangu. Mitume wa upendo wangu, ninawafunika kwa joho langu kwa sababu, kama Mama yenu, nataka kuwalinda. Nawasihi: mwuombee ulimwengu wote: moyo wangu unateswa. Dhambi zinaongezeka, ni nyingi mno. Lakini kwa msaada wenu – mlio wanyenyekevu, wanyofu, wenye upendo, watawa na watakatifu – moyo wangu utashinda. Mpendeni Mwanangu kupita wote na ulimwengu wote kwa njia yake. Msisahau kabisa ya kuwa kila ndugu yenu ana ndani yake kitu cha thamani: nafsi. Kwa hiyo, wanangu, pendeni wale wote wasiomjua Mwanangu ili kwa njia ya maombi na upendo utokao katika maombi, wawe wema zaidi. Ili wema uweze kushinda ndani yao. Ili nafsi zao ziweze kuokoka na kupata uzima wa milele. Enyi mitume wangu, wanangu. Mwanangu aliwaambieni mpendane. Hiyo iandikwe mioyoni mwenu na kwa kusali jaribuni kuishi upendo huu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, nikiwatazama hapa mmekusanyika kunizunguka, Mama yenu, ninaona nafsi safi nyingi. Ninawaona wanangu wengi wanaotafuta upendo na faraja lakini hakuna mtu anayewapa. Ninawaona hata wale wanaotenda mabaya maana hawana mifano myema, maana hawajamjua mwanangu. Mwanangu anawatuma ninyi kwangu, Mama, sawa kwa wote, niwafundisheni kupenda, ili muelewe ya kuwa ninyi ni ndugu. Ninatamani kuwasaidia. Mitume wa upendo wangu, kwa mwanangu yamtosha tamaa hai ya imani na upendo na atayakubali, lakini mnapaswa kustahili, kuwa na tamaa na mioyo wazi, Mwanangu huingia katika mioyo wazi. Mimi kama Mama ninatamani kwamba mjue Mwanangu katika kweli: Mungu aliyezaliwa na Mungu, kwamba mjue ukuu wa Upendo wake, ambao mnahitaji. Yeye amezichukua juu yake dhambi zenu, ameupata Ukombozi wenu, na badala yake anaomba mpendane ninyi kwa ninyi. Mwanangu ni upendo, Yeye anawapenda watu wote bila tofauti, watu wote wa nchi zote, wa mataifa yote. Ikiwa ninyi, wanangu, mngeishi upendo wa Mwanangu, ufalme wake ungekwisha kuwa duniani. Kwa hiyo, Mitume wa upendo wangu, salini, salini ili Mwanangu na upendo wake wawe ndani yenu nanyi muweze kuwa mfano wa upendo na muweze kuwasaidia wote wale ambao hawajamjua Mwanangu. Msisahau kamwe kwamba Mwanangu, mmoja na utatu, anawapendeni. Pendeni na wombeeni wachungaji wenu. Nawashukuru.
Wanangu wapendwa, Mimi ni Mama wa ninyi nyote na kwa hiyo msiogope kwa sababu mimi ninasikia sala zenu, najua kwamba mnanitafuta na kwa hiyo ninamwomba Mwanangu kwa ajili yenu; Mwanangu ambaye yu katika mwuungo pamoja na Baba wa mbinguni na pamoja na Roho Mfariji, Mwanangu anayewaongoza roho katika Ufalme alikotoka, ambao ni Ufalme wa amani na wa mwanga. Wanangu, mmepewa uhuru wa kuchagua, kwa hiyo mimi kama Mama ninawasihi mchague uhuru kwa mema, na kwa moyo safi na mnyofu mnaelewa, ingawa pengine hamwelewi maneno yote, ndani yenu mng'amue ukweli ni nini. Wanangu, msipoteze ukweli na maisha ya kweli kwa kufuata maneno ya uongo. Kwa njia ya maisha ya kweli Ufalme wa mbinguni huingia katika mioyo yenu, ni Ufalme wa upendo, wa amani na wa maelewano. Katika Ufalme ule, wanangu, hautakuwa na ubinafsi wa kuwaondoa kutoka kwa Mwanangu, kutakuwa na upendo na maelewano na jirani yako. Kwa hiyo kumbukeni, ninawaambieni tena, kusali maana yake ni kuwapenda wengine, kumpenda jirani yako, kujitoa kwa ajili yao; pendeni na toeni kwa jina la Mwanangu, hapo Yeye atatenda kazi ndani yenu na kwa ajili yenu. Wanangu, fikirini daima juu ya Mwanangu, mpendeni bila kipimo na hapo mtakuwa na maisha ya kweli, yatakayokuwa ya milele. Nawashukuru enyi Mitume wa upendo wangu!
Wanangu wapendwa, Mwanangu mpenzi alimwomba sikuzote na kumtukuza Baba wa Mbinguni. Sikuzote alikuwa amemwambia yote na kujiachia katika mapenzi yake. Hivyo mnapaswa kufanya hata ninyi, wanangu, maana Baba wa Mbinguni anawasikiliza sikuzote wanawe. Moyo wa umoja katika moyo mmoja: upendo, mwanga na uhai. Baba wa Mbinguni amejitolea kwa njia ya sura ya kibinadamu, na sura ile ndiyo sura ya Mwanangu. Ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnapaswa sikuzote kupokea sura ya Mwanangu katika mioyo yenu na katika fikira zenu. Ninyi mnapaswa sikuzote kuufikiria upendo wake na sadaka yake. Mnapaswa kusali ili kusudi mwone uwepo wake sikuzote. Maana, enyi mitume wa upendo wangu, hii ni jinsi ya kuwasaidia wale wote wasiomjua Mwanangu, wale ambao hawajajua upendo wake. Wanangu, someni kitabu cha Injili: ni sikuzote kitu kipya, ni kinachowaunganisha na Mwanangu, aliyezaliwa kwa kuwaletea maneno ya uzima wanangu wote na kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya wote. Mitume wa upendo wangu, mkisukumwa na upendo kumwelekea Mwanangu, leteni upendo na amani kwa ndugu zenu wote. Msimhukumu mtu, pendeni kila mtu kwa njia ya upendo kwa kumwelekea Mwanangu. Hivyo mtashughulika hata na roho zenu, nayo ni yenye thamani kuliko kitu chochote mlicho nacho. Ninawashukuru.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`