Monthly Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa! Kwa furaha kubwa leo nawaletea Mwanangu Yesu ili Yeye awapeni amani Yake. Wanangu, fungueni mioyo yenu na muwe wafurahivu, ili muweze kuipokea. Mbingu ni pamoja nanyi na zinapambana kwa ajili ya amani mioyoni mwenu, katika jamaa na ulimwenguni na ninyi, wanangu, msaidieni kwa sala zenu ili iwe hivyo. Ninawabariki pamoja na Mwanangu Yesu na kuwaomba msikose matumaini, na mtazamo wenu na moyo wenu yaelekee daima mbinguni na uzima wa milele. Hivyo mtafunguliwa kwa Mungu na mipango Yake. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Leo pia nawaalika kurudi katika sala. Katika wakati huu wa neema, Mungu amenijalia kuwaongoza kuelekea utakatifu na maisha ya unyofu, ili katika mambo madogo muweze kumtambua Mungu Mwumbaji, kumpenda na ili maisha yenu yawe shukrani kwa Mungu Mkuu kwa yote aliyowajalia. Wanangu, maisha yenu yawe zawadi kwa wengine katika upendo naye Mungu atawabariki. Nanyi, mumshuhudie bila kutafuata faida, kwa ajili ya upendo kwa Mungu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi nyote mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Leo nawaalika: ombeni amani! Acheni ubinafsi na ishini ujumbe ninaowapa. Bila hizo ujumbe hamwezi kubadili maisha yenu. Mkiwa watu wa sala mtakuwa na amani. Mkiishi katika amani mtaona hitaji la kutoa ushuhuda maana mtamtambua Mungu mnayemhisi sasa kama yu mbali. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini, na mkamwache Mungu aingie mioyoni mwenu. Rudieni kufunga na kuungama, ili muweze kushinda uovu ulio ndani yenu na kandokando yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Leo nawaalika kusali. Sala na iwe maisha kwenu. Hivyo tu moyo wenu utajaa amani na furaha. Mungu atakuwa karibu nanyi, nanyi mtamhisi moyoni mwenu kama rafiki. Mtaongea naye kama na mmoja mjuaye na, wanangu, mtaona hitaji la kutoa ushuhuda maana Yesu atakuwa moyoni mwenu na ninyi mtaambatana naye. Mimi ni pamoja nanyi na kuwapenda nyote kwa upendo wangu wa kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Leo nataka kushirikiana pamoja nanyi furaha ya mbinguni. Ninyi wanangu fungueni mlango wa moyo ili katika moyo wenu matumaini, amani na mapendo ambazo Mungu peke yake anaweza kutoa ziweze kukua. Wanangu, mnapenda mno dunia na mambo ya dunia, kwa hiyo Shetani huwatikisa kama upepo ufanyavyo na mawimbi ya bahari. Kwa hiyo mnyororo wa maisha yenu uwe sala ya moyo na kumwabudu Mwanangu Yesu. Kwake mtolee maisha yenu yajayo ili muwe ndani Yake furaha na mfano kwa watu wengine kwa njia ya matendo yenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Ninawaangalia na ninawaona mmepotea, hamna wala sala wala furaha ndani ya mioyo yenu. Rudini, wanangu, kusali na wekeni Mungu katika mahali pa kwanza na si mtu. Msipoteze tumaini ninalowaletea. Wanangu, wakati huu uwe kwenu kila siku kumtafuta Mungu katika kimya ya moyo wenu na salini, salini, salini mpaka sala iwe furaha kwenu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Mshukuruni Mungu kwa zawadi ya kuwepo kwangu pamoja nanyi. Salini, wanangu, mkaishi amri za Mungu mweze kuwa na heri duniani. Leo, katika siku hii ya neema nataka kuwapeni baraka yangu ya kimama ya amani na ya upendo wangu. Ninawaombeeni kwa Mwanangu na kuwaalika kudumu katika sala ili pamoja nanyi niweze kutimiza mipango yangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Uwepo wangu ni zawadi ya Mungu na kichocheo cha uwongofu wenu. Shetani ana nguvu na anataka kutia moyoni na fikirani mwenu fujo na wasiwasi. Kwa hiyo, ninyi wanangu salini ili Roho Mtakatifu awaongoze katika njia iliyonyoka ya furaha na amani. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea ninyi mbele ya Mwanangu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Moyo wangu usio na doa unatoka damu nikiwaangalieni katika dhambi na mazoea mabaya. Nawaalika: mrudieni Mungu na salini ili mpate kufanikiwa duniani. Mungu anawaalika kwa njia yangu ili mioyo yenu iwe tumaini na furaha kwa wale wote walio mbali. Ombi langu liwe kwenu manukato kwa nafsi na moyo ili mtukuze Mungu Mwumbaji anayewapenda na kuwaalika kwa mambo ya milele. Wanangu, maisha ni mafupi, mtumie nafasi hii kwa ajili ya kutenda mema. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Leo ninawaletea upendo wangu. Mungu ameniruhusu kuwapenda ninyi na kwa upendo nawaalika mwongoke. Wanangu, ninyi ni maskini katika upendo, na wala hamjaelewa bado ya kuwa Mwanangu Yesu ametolea maisha Yake ili awaokoeni na kuwapa uzima wa milele. Kwa hiyo salini wanangu, salini ili muweze kuelewa katika sala upendo wa Mungu. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa! Katika wakati huu wa neema nawaalikeni nyote kuongoka. Wanangu, mnapenda kidogo, na bado mnasali kidogo. Mmepotea wala hamjui lengo lenu ni nini. Chukueni msalaba wenu, mwangalieni Yesu mumfuate. Yeye anajitoa kwenu hata kufa msalabani maana anawapenda. Wanangu, nawaalikeni kurudia kusali kwa moyo kwa maana katika sala mnaweza kupata matumaini na maana ya uwepo wenu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwaombea. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, hata leo nawaalika kusali. Pasipo sala hamwezi kuishi maana sala ndiyo mnyororo unaowawezesha kumkaribia Mungu. Kwa hiyo wanangu, kwa unyenyekevu wa moyo mrudieni Mungu na Amri zake ili muweze kusema kwa moyo wote: kama mbinguni lifanyike hata duniani. Wanangu, ninyi ni huru kuamua katika uhuru kuwa wa Mungu ama dhidi yake. Tazameni kama shetani anavyotaka kuwaingiza katika dhambi na utumwa. Kwa hiyo, wanangu, rudini kwa Moyo Wangu ili Mimi niweze kuwaongoza kwa Mwanangu Yesu aliye Njia, na Ukweli na Uzima. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
   




To compare Medjugorje messages with another language versions choose

For God to live in your hearts, you must love.

`